KUSHUKURU NI UUNGWANA, ASANTE MHE.RAIS SAMIA SULUHU HASSAN.
Amon Nguma
Tarehe 19 March 2023 tumetimiza miaka miwili ya uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tumefika miaka miwili kwa mafanikio makubwa na matumaini ni makubwa zaidi kwa siku za usoni.
Mafanikio ni makubwa yaliyopatikana katika miaka miwili, yafuatayo ni kwa uchache:
(1) Kulinda tunu ya amani, umoja na mshikamano. Katika kipindi chote Mhe. Rais ameonesha dhamira yake njema ya kulifanya taifa kuwa na amani na mshikamano ikiwa ni turufu ya maendeleo ya taifa lolote lile. Asante Mhe. Rais kwa kudumisha tunu za taifa letu.
(2) Kuendeleza na kuanzisha miradi mikubwa na ya kimkakati yenye tija katika taifa letu. Katika kipindi cha miaka miwili ya Mhe. Rais Samia, tumeona miradi mikubwa ikienda kwa kasi.
Mfano, mpaka sasa, bwawa la Nyerere (Stiglers) limekwisha jazwa maji, uzinduzi wa vipande vinne vya SGR (Makutupora-Tabora-Isaka-Mwanza-Kigoma), kukamilika kwa meli ya MV Mwanza, daraja la Tanzanite, uanzishwaji wa ujenzi wa bandari ya kisasa ya uvuvi-Kilwa ambayo itatumia bilioni 266.7, bandari hii itakayochochea shughuli uvuvi katika Bahari ya Hindi na kutoa ajira nyingi kwa wananchi, kukuza sekta ya anga kwa kujenga viwanja vya ndege ikiwemo cha kimataifa cha Msalato-Dodoma pamoja na viwanja vinavyojengwa kila mkoa sanjari na ununuzi wa ndege mpya tano zinazowasili mwaka huu nchini.
Kwa miradi michache hii kati ya mingi, shukrani Mhe. Rais Samia kwa uongozi unaogusa maisha ya Watanzania.
(3) Asante Mhe. Rais kwa kuifanya sekta ya afya na huduma kuwa za kisasa.
Tangu kuasisiwa kwa taifa letu ni katika kipindi hiki ambapo sekta ya afya imeshuhudia mapinduzi makubwa ya miundombinu na teknolojia ikiwemo - kuongeza vitanda vya ICU kutoka 258 vilivyokuwepo mpaka 1000, ukamilishaji wa hospitali ya rufaa ya kanda ya kusini, hospitali za rufaa katika mikoa ya Katavi, Geita, Mara, Songwe na Shinyanga zenye vifaa na mitambo ya kisasa, uzinduzi wa teknolojia ya kisasa ya upasuaji ubongo pasipo kufungua fuvu, ununuzi wa mitambo ya kisasa (X-Ray 62, CT-Scan 32, MRI 7, mashine za uchunguzi wa moyo 7 na fluoroscopy 2) lengo ni kuleta huduma karibu na wananchi kwa gharama nafuu ikilinganishwa na ilivyokuwa awali, ununuzi wa mitambo 19 ya kuzalisha hewa tiba (oksjeni) ambayo imesimikwa katika hospitali mbalimbali za mikoa na kanda, na ni serikali hii hii ambayo imeajiri watumishi wa kudumu zaidi ya 10000 katika kipindi kifupi ili wakatoe huduma kwetu wananchi. Asante Mhe. Rais Samia kwa kazi kubwa na nzuri kwenye sekta ya afya.
(4) Shukrani na hongera Mhe. Rais kwa kufanya mapinduzi ya kilimo.
Katika kipindi kifupi tumeona mabadiliko makubwa katika sekta ya kilimo kuanzia kwenye bajeti, bajeti ya mwaka huu zaidi ya bilioni 750 ikiwa ni kubwa zaidi kuliko zilizopita, uwezeshaji wa mbegu za kisasa kwa wakulima, ununuzi wa usafiri na vifaa kwa maafisa ugani kwa kilimo zaidi ya 7000, utolewaji wa mbolea ya ruzuku kwa wakulima, utafutaji wa masoko ya uhakika ya mazao ya wakulima, uanzishwaji wa mashamba (block farming) miradi ya umwagiliaji, pamoja na mradi mkubwa wa kilimo kwa vijana kupitia mradi wa (BBT) ambapo mafunzo yameshaanza na mashamba yameshaandaliwa. Shukrani na hongera Mhe. Rais kwa kufanya mapinduzi ya kilimo.
(5) Uendelezaji wa mahusiano ya kimataifa na diplomasia wa uchumi.
Katika kipindi kifupi Mhe. Rais ameonesha uwezo wake mkubwa wa kidiplomasia kwa kuendeleza na kuboresha zaidi mahusiano ya Tanzania na mataifa mengi, jambo ambalo limeendelea kufungua fursa katika taifa letu, ikiwemo masoko ya bidhaa za Tanzania, hususani mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi ambayo yameleta tija kubwa kwa wakulima, pamoja na kuvutia uwekezaji na utalii nchini, ambapo ajira nyingi zimezalishwa.
(6) Shukrani Mhe. Rais Samia kwa mambo mengi uliyolifanyia taifa letu, ikiwemo:
- Kulinda haki za binadamu, demokrasia na utawala bora.
- Kutangaza vivutio vya uwekezaji na utalii kupitia The Royal Tour.
- Kutoa vibali vya ajira na kuajiri watumishi katika sekta ya umma pamoja na ajira nyingine kupitia uwekezaji na miradi.
- Kuboresha huduma na miundombinu ya utoaji haki na usimamizi wa sheria kwa ujenzi wa mahakama katika maeneo mbalimbali nchini.
- Kuinua sekta ya sanaa na michezo kwa uwezeshaji wa kisera, kifedha na wataalamu.
- Ujenzi wa madarasa zaidi ya 20,000 katika kipindi cha miaka miwili.
- Ukamilishaji wa Ikulu ya Chamwino pamoja na ujenzi wa mji wa serikali Dodoma.
- Vita dhidi ya rushwa, ufisadi na uzembe.
Asante Mhe. Rais Samia kwa mengine mengi ambayo hayajaorodheshwa hapa.
Kushukuru na kupongeza pindi mtu anapotimiza wajibu wake kufanya kitu kizuri ama kuleta matokeo chanya ni uungwana. Na kwa uungwana huo, asante na hongera Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa mambo makubwa na mazuri uliyolifanyia taifa letu kama kiongozi mkuu wa nchi yetu.
Tulipo ni pazuri, na tunapokwenda matumaini ni makubwa zaidi chini ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
#MiwiliNaSamia
#KaziIendelee