JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, limesema linaendelea na ukamataji watu wanaosadikiwa kujihusisha na matumizi na biashara ya dawa za kulevya na linawashikilia wasanii wawili wa muziki wa bongo fleva, akiwemo Vanessa Mdee.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum Simon Sirro alisema wasanii hao walikamatwa juzi na wanaendelea na mahojiano ili kubaini kama wanajihusisha na biashara hiyo au la.
Alisema msanii mwingine anajulikana kwa jina la Rumishael ; na taarifa za awali zinaonesha kuwa wasanii hao ni watumiaji na pia wanajihusisha na biashara ya kusambaza dawa hizo.
“Tuko nao tangu juzi na kwa sasa tunaendelea na upelelezi ili kujiridhisha na utakaokamilika watawafikisha mahakamani kwa hatua zaidi, wapo wengi, si hawa tu; na shughuli ya ukamataji inaendelea vizuri,” alisema Kamanda Sirro.
Sirro aliwaomba wananchi, kuendelea kutoa taarifa za watu wanaojihusisha na biashara hiyo, lengo likiwa ni kuhakikisha suala la dawa za kulevya linamalizwa katika mkoa huo.
“ Niwaombe wana Dar es Salaam waendelee kutoa taarifa, lakini ziwe za kweli ili kufanikisha suala hili kwa manufaa ya Watanzania,” aliongeza Sirro.
Mwezi uliopita msanii Vanessa alitajwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuwa anasadikiwa kujihusisha na biashara hiyo, ambapo alitakiwa kufika katika Kituo Kikuu cha Polisi cha Kanda hiyo kwa mahojiano, lakini alishindwa kufika kutokana na kuwepo nchini Afrika Kusini kikazi.
Taarifa katika mitandao mbalimbali ya kijamii, zinasema msanii huyo alijisalimisha katika kituo hicho juzi ; na polisi walimpekua nyumbani kwake, kabla ya kumpeleka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa ajili ya uchunguzi zaidi.