Wakulima wa wilaya ya Taijiang wana desturi ya kucheza mpira wa kikapu. Miongoni mwa vijiji vya wilaya hiyo, kijiji cha Taipan kinajulikana zaidi, kwani kati ya wanakijiji wake zaidi ya 1,100, bila kujali umri au jinsia, theluthi mbili kati yao wanapenda kucheza mpira wa kikapu. Kijiji cha Taipan ndio chanzo cha “VBA”. Mwaka huu mashindano hayo yalishirikisha timu 170, na wachezaji karibu 2,000. Licha ya wachezaji hao, wanakijiji kutoka wazee wenye umri wa zaidi ya miaka 80 hadi watoto wa miaka chini ya 10 walishangilia timu wanazozipenda.
Tukizungumzia “VBA”, inabidi tuzungumzie sera ya China ya kupunguza umaskini na ustawi wa vijiji. Wilaya ya Taijiang ya sehemu inayojiendesha ya makabila ya Wamiao na Wadong ya mkoa wa Guizhou, ina wakazi chini ya 200,000. Kwa kuwa iko kwenye milima mirefu, wilaya hiyo ilikabiliwa na umaskini uliokithiri kwa muda mrefu. Mwaka 2020, kutokana na vita dhidi ya umaskini nchini China, Taijiang ilifanikiwa kuondokana na masikini, na hadi mwaka huu, wastani wa kipato cha watu wa wilaya hiyo umekaribia kiwango cha wastani cha mkoa wa Guizhou. Watu wa Taijiang ambao wanaishi maisha mazuri wameanza kuzingatia afya zao na maisha ya kiroho na kitamaduni.
“VBA” pia imekuwa kivutio cha utalii. Mwaka 2021, utalii katika wilaya ya Taijiang ulikua kwa kasi licha ya janga la UVIKO-19, na ongezeko la upokeaji wa utalii kutoka ndani na nje ya nchi na pato la kitalii lilikuwa asilimia 30.6 na 38.2 mtawalia. “VBA” imeleta nguvu mpya ya ustawi wa utalii wa vijijini. Watalii hutembelea vijiji vya jadi vya kabila la Wamiao wakati wa mchana ili kujionea utamaduni wa asili wa kabila hilo dogo, na usiku wanakwenda kwenye uwanja wa kijiji kutazama michezo ya mpira wa vikapu.
Maisha bora ya vijiji katika wilaya ya Taijiang ni mfano mdogo wa mafanikio makubwa ya sera ya kupunguza umaskini vijijini nchini China. Kutokana sera hiyo, sehemu zilizokuwa maskini na nyuma kimaendeleo zimepata maendeleo makubwa. Hivi leo, kufuatia utekelezaji wa mkakati wa kustawisha vijiji, vipato vya wakulima vinaongezeka kwa kasi, ustawi wa watu umeendelea kuimarika, na maisha yao yanaboreshwa siku hadi siku.