Mzee Mwanakijiji
Platinum Member
- Mar 10, 2006
- 33,771
- 41,027
(Makala hii imetoka kwenye gazeti la Raia Mwema, Jumatano Machi 31, 2021. Picha juu kutoka kwa Michuzi Blog).
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan ana kibarua kigumu. Anakabiliwa na kuridhisha pande nyingi kiasi kwamba upande wowote ambao hatouridhisha au hatoonekana kuuridhisha hautachelewa kumpinga na upande ambao utaonekana unapendelewa utachukiwa na ule upande mwingine. Kama kuna mtu anadhania kuwa Rais Samia atafanya Watanzania wote tushikane mikono na kuanza kuimba kwa pamoja “Ukuti Ukuti” kana kwamba hatuna tofauti za msingi mtu huyo anajidanganya. Tofauti na mtangulizi wake Rais Samia anaingia akiwa anakabiliwa na changamoto ambazo hakuna Rais mwingine yeyote wa Tanzania amewahi kuzipata. Ni katika hili hekima, ujasiri, ubunifu, na uthubutu wake utaenda kupimwa na labda ataangaliwa kwa macho makali zaidi kuliko Rais mwingine yeyote.
Viatu vya Magufuli
Upande wa kwanza anakabiliwa kujaribu kuvivaa viatu vya kiungozi vya Magufuli. Mtu anapojaribu kuvaa viatu vya mtu mwingine anakabiliwa na changamoto; ama vitamtosha, vitambana, au vitampwaya. Kama vitamtosha bado ataangaliwa kama vimemkaa; vinaendana naye au la; kama vitambana swali ni kwa kiasi gani au vipanue au atafute vingine; na kama vitampwaya ni je anahitaji kuongeza nini ili vimtoshe au bado atahitaji kutafuta vile vinavyomtosha tu hadi atakapokuja mwingine ambaye viatu hivyo vitamtosha.
Rais Samia atahukumiwa kwanza kwa kabisa ni kwa kiasi gani ataenda kusimamia miradi mikubwa “ya kimkakati” iliyoanzishwa chini ya Rais Magufuli. Ni kwa kiasi gani mradi wa SGR (treni ya umeme) utaenda kukamilika na kusimamiwa; mradi wa bwawa la umeme la Mwalimu Nyerere, na kuhamia Dodoma. Hii ni baadhi tu ya miradi hiyo. Uzuri ni kuwa kwa vile alikuwa ndani ya serikali hii toka mwanzo mama Samia inawezekana ni mtu pekee anayeilewa na kujua ni kwa kiasi gani inahitajika na hivyo kwake inaweza isiwe ngumu kabisa kufuatilia miradi hii mikubwa, ile ya kati na midogo.
Kama tulivyoshuhudia suala la ubadhirifu, ufisadi na kutokuridhika na utendaji kazi aliouonesha siku ya Jumapili akipokea taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa serikali; Rais Samia atahukumiwa pia ni kwa jinsi gani hatoacha uzembe, kubebana na kupeana “second chances” kutaendelea. Hii ina maana hatoacha wateuliwa wa Rais Magufuli ambao wanapwaya sasa hivi na labda walishaonekana wanapwaya. Je, atatakiwa asubiri hadi arudi ofisini kabla ya kuchukua hatua au atachukua hatua pale pale kwa staili ya Magufuli ya “kutumbua”. Je, tumbua yake itakuwa ni ile ya kupisha uchunguzi ili mtu achunguzwe kabla ya kumfuta mtu kazi papo kwa papo kama alivyokuwa akifanya Magufuli?
Ataangaliwa kwa jinsi gani analiongoza taifa kuelekea kujitegemea kuliko kurudi kwenye kutegemea. Je, katika hili atatumia lugha tofauti kuliko ile ya Magufuli? Je, katika kujitegemea atajaribu kulitenga taifa na dunia au atajaribu kuliweka taifa katika nafasi yake sahihi ya kushirikiana na dunia. Kwamba, kama Magufuli hatolirudisha taifa katika aibu ya kuombaomba hata kwa vitu visivyoombeka? Je, ataanza safari za kwenda duniani kujitambulisha na kuomba misaada tena? Au ataangalia kimkakati ni wapi Watanzania bado tunaweza? Na katika hili tena alikuwa chini ya mwalimu mzuri. Rais Samia aliona na kuielewa kiu ya Rais Magufuli ya kuona Watanzania wanajiamini na kuwa hawajioni wanyonge; na jinsi gani aliwahusisha Watanzania katika kutekeleza mambo mbalimbali bila kusubiri vibali vya wakubwa wa dunia.
Ni kwa sababu hiyo wapo watakaoangalia na kuona kama amevivaa viatu vya Magufuli au vimemvaa yeye; ama ameingia na viatu vyake na vikapendeza zaidi kuliko vile vya Magufuli. Akaamua kupita alikopita Magufuli lakini kwa hatua zake na kwa mwendo wake. Inawezekana akawa ametengenezewa njia nzuri zaidi ya kupita na Magufuli na yeye akaipita kwa urahisi zaidi kuliko kama mtangulizi wake asingekuwa Magufuli.
Kivuli cha Magufuli
Lakini Rais Samia pia anauamuzi wa kwake mwenyewe. Japo ameingia kuziba pengo la Magufuli na chini ya mwaka mmoja tu wa ngwe yao ya pili kwa kweli si lazima afuate kila alichofanya Magufuli. Si lazima azungumze alivyozungumza Magufuli, si lazima aoneshe ukali kama Magufuli au afanye maamuzi kama alivyofanya Magufuli. Kwa hakika kabisa japo kinadharia hapaswi kwenda nje ya Ilani na ajenda yao na Magufuli lakini pia hafungwi kuanzisha ya kwake na hata kufutilia mbali ajenda ya Magufuli. Lakini vyovyote atakavyoamua kufanya kivuli cha Magufuli kitaendelea kumfunika.
Kundoka kwa Magufuli na kumwachia Samia kunamfanya Samia aingie akiwa na jukumu kubwa la kuonesha siyo tu alikuwa Makamu lakini alikuwa Makamu aliyeweza kuwa Rais kama historia inaita hivyo. Kumuondoa Ronaldo uwanjani kunatoa nafasi kwa mchezaji wa akiba kuonesha kama anastahili kuchukua nafasi ya mchezaji huo nyota. Lakini uchezaji wote utapimwa na kuona kama anaweza kutoa mchango wa kuisaidia timu kushinda. Mama Samia anaingia kuchukua nafasi ya mchezaji nyota; ni jinsi gani ataifungia magoli timu yake na kuisadia kushinda na hivyo kujihakikishia namba ni suala la muda.
Lakini la muhimu ni kuwa si lazima afanye kazi akiwa na kivuli cha Magufuli mgongoni. Japo, anaenda kuibeba ajenda ya Magufuli si lazima aibebe mabegani kama Magu kama ana uwezo wa kuibeba kichwani. Kivuli cha Magufuli kisiwe kizuizi bali kiwe ni daraja la kuvukia kwenda anakotaka kuipeleka Tanzania. NI kwa sababu hiyo asiogope, asifikirie mara mbilimbili, au hata kujishuku endapo ataamua kufanya mabadiliko ya lazima ambayo labda Magufuli asingeyafanya. Kipimo chake sasa siyo Magufuli tena bali ni yeye mwenyewe kama Rais. Kauli yake msibani kuwa aliyesimama pale ni “Rais” itume ujumbe kwa yeyote mwenye shaka na shuku; kwamba siyo tu yeye ni Rais bali pia madaraka aliyokuwa nayo Magufuli ndiyo aliyonayo yeye leo; uwezo aliokuwa nao Magufuli aliopewa na Katiba ndio uwezo ule ule aliopewa yeye. Yeye sasa anatakiwa kutengeneza kivuli chake mwenyewe na akifanya vizuri basi atajitengenezea haki na nafasi ya kutengeneza ajenda yake ya 2025 akitaka kugombea tena.
Tanzania ya Samia
Ni wazi basi kuwa Watanzania wanapompokea Rais wao mpya wapo wenye matarajio mengi na yenye kutofautiana. Wapo ambao wanatarajia kuwa anaingia na kuwa kama Rais kutoka upinzani ambaye atafutilia mbali jina, historia, mafanikio, na maamuzi yote ya Magufuli na hivyo kutengeneza historia (legacy) yake mwenyewe nje ya Magufuli. Kwamba, akijiweka mbali na Magufuli na ajenda yao basi atakubalika zaidi na wapinzani na wakosoaji wa Magufuli. Kwamba, atake kupendwa na wale waliomchukia Magufuli.
Lakini pia anaweza akajikuta anajitahidi sana kuwa kama Magufuli na kujikuta anatengeneza maadui na wakosoaji wengi zaidi kuliko aliokuwa nao Magufuli na hivyo kuoneakana ni Magufuli 2.0. Changamoto kubwa ya Tanzania hii ya Samia ni kutafuta mizania kati ya alikotoka na Magufuli na anakotaka kwenda bila Magufuli. Je, itakuwa ni Tanzania ya namna gani? Je, watu wake watasimama vipi? Je, atatengeneza taasisi na kuinua watu kwa namna gani? Je, anatamani iwe Tanzania ya namna gani. Swali hili naamini litajibiwa siku si nyingi pale atakaposimama kulihutubia taifa na kutoa mwelekeo wa maono yake kwa taifa na tutaona atakavyoanza kuipanga serikali yake ili kutimiza maono hayo.
Kwa sasa ni wazi kuwa Watanzania bado wamegawanyika na wanasubiria kuona kama mgawanyiko wao utaendelea kuwa ni wa kudumu au utawasogeza karibu karibu au utapanua zaidi mgawanyiko huo. Kwa kweli, siwezi kumuonea wivu katika kibarua hiki. Ninachomtakia ni kila la kheri katika kuliongoza taifa letu na kuwa vyovyote atakavyokuwa historia itaweza kumhukumu si kwa jinsi gani alivyokuwa kama Magufuli au kwa jinsi gani alivyokuwa tofauti na Magufuli; atahukumiwa kwa jinsi gani aliliongoza taifa letu kuelekea mafanikio ya kweli, ubora wa maisha, kuinuliwa kwa tunu zetu mbalimbali za kitaifa kiasi kwamba ije kusemwa Tanzania ya Samia ilikuwa ni Tanzania tuliyoitarajia.
Na ili kuifikia Tanzania hiyo ni lazima tukatae mbinu, majaribio au hata jitihada zozote za kumshusha Rais Samia, kumdhoofisha au kumtendea kana kwamba si Rais “kamili” kwa sababu tu ni mwanamke. Tukatae tena kwa ukali wote unaostahili lugha zote za kinyanyasaji kijinsia ambazo nyingine zimeenea mitandaoni. Tuwakatae wale wote wanaozungumza kana kwamba wanamuunga mkono lakini wanafanya hivyo ati kwa sababu “ni mama” kana kwamba umama wake ni kitu cha kumdhoofisha.
Tujue kuwa anaingia madarakani akiwa na nguvu zote kama Rais wa Tanzania bila kujali jinsia yake. Lakini pia inatupa nafasi ya kuwa na kiongozi ambaye ana mtazamo tofauti kuliko wengine na hivyo labda ataweza kuwainua pia wanawake wengi wenye uwezo ambao labda hawakupata nafasi zozote za juu za uongozi kwa sababu ya mitazamo mibaya ya kijinsia (gender biases).
Lakini pia naamini atawapa nuru mabinti zetu kutamani kufikia nafasi yoyote ya uongozi wa nchi yetu na kuwa wale wote wenye nafasi za uongozi wafanye hivyo kwa weledi mkubwa zaidi bila kuonekana wanajikomba kwa mwanamme yeyote. Na kama nitakavyoonesha wiki ijayo kuna mambo ambayo naamini Rais Samia ni LAZIMA ayafanye tofauti na Magufuli.
Katika Tanzania ya Samia hakuna cha kuhofia.
Niandikie: klhnews@gmail.com