SoC02 Vijana Tabia za Kuepuka

SoC02 Vijana Tabia za Kuepuka

Stories of Change - 2022 Competition

Kwa Imani

Member
Joined
Sep 19, 2021
Posts
10
Reaction score
7
Kijana kama unataka kufanikiwa maishani, epuka tabia zifuatazo:

1: KUKOSA UAMINIFU KAZINI
Vijana wengi sio waaminifu kabisa, wengi wana tamaa ya mali nyingi ndani ya muda mfupi, hata kama ni kwa njia isiyo halali. Kuna vijana kila wakipewa kazi wanawaza namna ya kupiga madili tu kama vile kuiba, udanganyifu kazini, n.k. Ingawa wanalalamika hawana mitaji na hakuna ajira, lakini wakipewa kazi wanajisahau tena, wanaanza upigaji (wizi).

Hivi karibuni (April 2021) tulisikia kwenye vyombo vya habari, Aliyekua Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati huo, Job Ndugai akilalamikia suala la uaminifu kwa vijana. Alisema, “Wawekezaji wengi wamekuwa wakilalamikia suala la uaminifu kwa vijana hasa vijana nchini Tanzania, uaminifu ni mdogo katika miradi ndani ya sekita mbalimbali. Ukiwaweka unajikuta unafilisika… Leo ukiwekeza alafu uje Bungeni umewaachia miezi sita hujawatembelea utakuta umepigwa.”

Ni kweli vijana wengi sio waaminifu. Mfano ukiwa unamiliki gari, bodaboda, bajaji, saluni, mashine, duka au mradi wowote, ukamuajiri kijana unamlipa kila mwisho wa mwezi, bado atakuwa anakuibia nusu ya hela inayopatikana na huku mwisho wa mwezi unamlipa mshahara.

Usijidanganye kwamba utapata mafanikio ya haraka kwa kuiba. Ikiwa utaendelea kukosa uaminifu basi ujue ndo utachelewa sana kufanikiwa. Siku za mwizi ni arobaini, hutapiga madili siku zote, kuna siku dili litagoma au utashtukiwa. Dhuluma hailipi, kuna vijana walikuwa wameshaanza kupiga hatua ila kwa sababu ya kupenda kupiga madili na janja janja kazini, wamejikuta wanapoteza hata ile kazi ndogo waliyopata.

2: KUPENDA KUIGA VIPAJI NA MAWAZO YA WENGINE
Vijana wengi hatutaki kubuni vya kwetu tunapenda kukopi, ukiona mwenzako amefanya biashara au kazi fulani amefanikiwa, na wewe unaenda kuanzisha kitu kile kile. Mfano, kwa sababu Diamond au Alikiba ana kipaji cha kuimba na amefanikiwa kupitia kuimba, basi kila mtu anataka aimbe hata kama kuimba sio kipaji chako. Mwingine akiona mtu fulani amefanikiwa kupitia utangazi, naye anataka awe mtangazaji.

Tabia ya kukopi itakuchelewesha kufanikiwa kwa sababu unaishi maisha ambayo sio yako kwa kufanyia kazi kipaji ambacho huna. Mchungaji David Mmbaga aliwahi kusema, “wengi hawafanikiwi kwa sababu hawafanyii kazi wito wao walioitiwa, bali wanafanyia kazi maoni (ideas) ya watu wengine juu yao.”

3 : KUKOSA JUHUDI NA UMAKINI KAZINI
Vijana wengi tumekua wazembe sana na irresponsible (tusiojali) hata tukipewa kazi hatujitumi. Wengi wanafanya mambo bora liende au kutimiza wajibu. Utakuta mtu anafanya kazi lakini hayupo makini, hajali kazi (careless), yupo yupo tu, hajisikii (hana mood ya kazi), kila muda amechoka utafikri amelazimishwa.

Hata wale ambao wamejiajiri unakuta hawaweki bidii katika kazi. Hakuna customer care (hujali wateja), unajibu jibu tu wateja unavyojisikia, vitu unarusha rusha ovyo, ni mzembe - unapoteza au kuharibu haribu vitu na tabia n.k.

4: KURIDHIKA
Vijana wengi hawana shauku na mambo makubwa, wameridhika na mafanikio kidogo waliyo nayo, hawatamani kuwa watu mashuhuri au kufanya mambo makubwa zaidi katika jamii. Wengi wakipata hela ya kubadilisha mboga na mavazi basi wanaridhika. Hizo zinaitwa juhudi za kuendelea kuwa hai na sio kuleta maendeleo makubwa.

5: KUKOSA HOFU YA MUNGU
Vijana wengi leo hawana hofu ya Mungu, hawana muda na ibada, hawamuogopi Mungu wala binadamu wenzao. Wengi ni wababe, wana kauli chafu, dharau na wanatukana ovyo ovyo nyumbani, mtaani, mitandaoni n.k.

Rais wa tatu wa Marekani Thomas Jefferson alisema “Nothing can stop the man with the right character from achieving his goal, nothing on earth can help the man with the wrong character”. Kwa kiswahili, hakuna kitu cha kumzuia mtu mwenye tabia njema asifikie lengo lake, na hakuna kitu duniani kinachoweza kumsaidia mtu mwenye tabia mbaya.

MAMBO YA KUZINGATIA

1: UAMINIFU


Jitahidi kuwa kijana mwaminifu, ambaye anaweza hata akaachiwa kuendesha mradi peke yake bila kusimamiwa wakati wote. Acha tamaa, ukipewa kazi tosheka na mshahara wako, usimzunguke bosi wako. Kama malipo hayatoshi ni heri mkae mezani uombe kuongezewa kuliko kumuibia boss.

Unaweza kuwa mzuri sana kitaaluma na una ujuzi mkubwa, lakini kama sio mwaminifu, utaishia kuwa unafukuzwa fukuzwa hata ukipata kazi haidumu. Uaminifu ni mtaji bora kuliko hata pesa.

Uaminifu wa Danieli ndio ulimwezesha kushinda njama za viongozi wenzake walipomwonea wivu kazini. Naomba kunukuu “basi mawaziri na maamiri wakatafuta sana kupata sababu za kumshitaki Danieli kwa habari za mambo ya ufalme, lakini hawakuweza kuona sababu wala kosa, kwa maana alikuwa mwaminifu, wala halikuonekana kosa wala hatia ndani yake.” (Danieli 6:4)

2: UKIPATA KAZI FANYA KWA BIDII
Kama umeajiriwa piga kazi kuvuka hata malengo ya mwajiri wako, hii itafanya ukubalike na mwajiri wako na asikubali kukupoteza kirahisi, hata ikitokea kupandishwa kazi (promotion) ni rahisi kukufikria. Kama umejiajiri, kuwa na juhudi kwenye kazi zako. Chapa kazi kabisa, usifanye mambo nusu nusu, bora liende na kwa ulegevu.

3: FANYIA KAZI KIPAJI CHAKO AU KUWA MBUNIFU
Usipende kukopi biashara na kazi za watu wengine. Tafuta kipaji chako ni kipi na ukiendeleze. Usianzishe biashara fulani kwa kuwa fulani ameifanya na akafanikiwa, usisome taaluma (kozi) fulani kwa sababu fulani aliisoma na amefanikiwa.

4: WAZA KUFANYA MAMBO MAKUBWA
Ukiona mafanikio yoyote, hayakutokea kwa bahati au muujiza, ni watu walidhamiria kuwa nayo. Kwa hiyo na wewe dhamiria kabisa kufikia standards za juu, weka makusudio ya juu. Hii itafaidisha sio wewe tu, bali na jamii nzima, maana utajikuta umetengeneza ajira kibao kwa vijana wenzako. Henry Ford anasema, “whether you think you can or you can’t, you’re right.” Kwamba, “ikiwa unafikri unaweza au huwezi, uko sahihi.”

5: HESHIMU MUNGU NA WATU
Unaambiwa “Ibada na uchaji wa kweli kwa imani yako ndio nuru yako duniani na Mbinguni.” Usiwe tu kijana ambaye haeleweki eleweki, hamuogopi Mungu wala wanadamu wenzake, kijana mbabaishaji, muongo muongo, maneno mengi n.k. Punguza dharau, matusi na ubabe usio na maana.

Heshimu kila mtu hata kama unamzidi elimu, kipato, ujuzi n.k. Wanasema, “degree is just a piece of paper, real education is seen in behavior.” Kwamba “Shahada ni kipande tu cha karatasi, elimu halisi huonekana kwenye tabia.”

Mchungaji Dr. Eliona Kimaro aliwahi kusema, “ni vizuri ukakumbuka kwamba kila mtu unayekutana naye hapa duniani bila kujali muonekano wake, nafasi au cheo chake, anaweza akawa mtu aliyebeba mustakabali wa mafanikio ya ndoto yako. Mtu anayekuja kwako huja kwa kusudi maalum. Kwa hiyo Usimdharau mtu. Pia tunza mahusiano yako na watu.

Asante kwa muda wako.
 
Upvote 1
Back
Top Bottom