Akiitwa jukwaani katika asubuhi ya baridi, John Mark, kijana mwenye umri wa miaka 19 anayesoma lugha ya Kichina kama somo la ziada, aliwavutia sana waliohudhuria kwenye Sikukuu ya Mwezi iliyoandaliwa na Taasisi ya Confucius katika Chuo Kikuu cha Kenyatta.
Uwezo wake mkubwa wa kutawala jukwaa, umbo lake refu, na sauti yake yenye mvuto vilifanya wimbo wa jadi wenye mtindo wa kisasa uitwao (Mapenzi ni kama Wimbi la Bahari) kuwa hai wakati wa ufunguzi wa hafla ya "Mwezi Mpevu, Maua Yanayostawi" ya mwaka 2026. Akiwa amevalia mavazi nadhifu, Mark aliimba maneno yenye hisia kali yaliyovutia kwenye sherehe hiyo, ambayo mwaka huu huadhimishwa tarehe 25 Septemba. Hafla hiyo ilihudhuriwa na wanadiplomasia, wasomi, na wanafunzi, ikijumuisha muziki, ngoma, kungfu, uandishi wa kaligrafia na kuonja keki tamu za mwezi.
"Ninapenda sana muziki wa Kichina kwa sababu mimi ni mwanamuziki, lakini zaidi ya hayo, ninafurahia utamaduni wao, hasa mitindo ya mavazi. Katika sikukuu hii, ninafurahishwa na uwezo wake wa kutuunganisha licha ya tofauti zetu za kitamaduni," alisema Mark.
Sherehe hiyo ya Mwezi, iliyofanyika katika ukumbi mkubwa, ilijumuisha hotuba, mijadala ya kitaaluma, na maonyesho ya kungfu, nyimbo, ngoma, uchoraji, pamoja na kugawana keki tamu za mwezi. Mamia ya wanafunzi kutoka shule za msingi, sekondari, na vyuo walihudhuria hafla hiyo ya nusu siku, iliyoandaliwa kwa ushirikiano kati ya Taasisi ya Confucius ya Chuo Kikuu cha Kenyatta na Wilaya ya Dingtao ya mji wa Heze katika Mkoa wa Shandong, mashariki mwa China.
Sambamba na kaulimbiu yake ya "Mwezi Mpevu, Maua Yanayostawi," sherehe hiyo ilitumia ua la 'peony' na mwezi kama daraja, ikiunganisha maua maarufu ya 'peony' ya kingo za Mto Majano na haiba pamoja na uchangamfu wa maeneo ya savanna ya Afrika Mashariki, katika jitihada za kusaidia utamaduni wa maua hayo ya China kustawi kote barani Afrika.
Leonard Chacha Mwita, Mkurugenzi wa Taasisi ya Confucius katika Chuo Kikuu cha Kenyatta, alibainisha kuwa sikukuu ya Mwezi ambayo huadhimishwa siku ya 15 ya mwezi wa nane kwa kalenda ya kilimo ya China, ina umuhimu mkubwa barani Afrika, kutokana na msisitizo wake wa kuungana kwa familia, shukrani, na maelewano.
"Hivyo basi, tusherehekee siku hii kama familia moja. Sikuu ya Mwezi inatuleta pamoja kutafakari wakati uliopita na kuwa na uhusiano mbalimbali unaotuunganisha," alisema Chacha.
Tang Jianjun, afisa katika Ubalozi wa China nchini Kenya, alisisitiza umuhimu wa Sikukuu ya Mwezi katika kuziba pengo la kitamaduni na kukuza maelewano na kuishi kwa amani. Aidha, Tang alisema kuwa maadhimisho ya sikukuu hiyo nchini Kenya yanaendana na malengo makuu ya Mwaka wa Mawasiliano baina ya Watu wa China na Afrika wa 2026, ambao ulizinduliwa mapema mwaka huu.
Maadhimisho ya Sikukuu ya Mwezi yaliwavutia vijana wa Kenya, ambao walifurahia shamrashamra na mbwembwe za mojawapo ya sherehe muhimu zaidi za jadi nchini China baada ya Mwaka Mpya wa Jadi wa China. Kwa uchangamfu wake wa ujana ulioonekana wazi, Angela "Tianshi" Moraa, mwanafunzi wa lugha ya Kichina katika Chuo Kikuu cha Kenyatta, alionesha umahiri wa kipekee wakati wa onyesho la pamoja la kungfu na muziki wa asili wa Kichina.
Moraa alisema kuwa maadhimisho ya Sikuu ya Mwezi yametoa fursa kwa vijana nchini kupata uelewa zaidi kuhusu utamaduni wa kale na wa kisasa wa China, pamoja na ushawishi wake katika ustaarabu wa dunia. Ikiwa na asili katika mila za kale za kuabudu mwezi na kusherehekea mavuno, Sikukuu ya Mwezi leo hii ni sikukuu rasmi nchini China na sehemu muhimu ya urithi wa kitamaduni wa taifa hili la Asia.
Kwa mujibu wa Benson Kamau, mwalimu wa lugha ya Kichina katika Chuo Kikuu cha Kenyatta, mbali na sherehe zenyewe, sikukuu hii inatoa fursa ya kuthamini familia, urafiki, furaha, amani na matumaini ya maisha bora ya baadaye.
Halima Saidi, mwanafunzi wa elimu katika Chuo Kikuu cha Kenyatta anayesoma lugha ya Kichina ngazi ya awali, amepata uelewa mzuri kuhusu sikukuu hii. Anathamini mila zake zenye maana, hasa jinsi inavyoleta pamoja familia na jamii ili kuimarisha uhusiano na kusherehekea maisha.