Ndani ya karakana iliyojaa watu wengi kando ya pwani ya Bahari Nyekundu ya Misri, Kareem Gaber, meneja wa vifaa katika kampuni ya Jushi Egypt Fiberglass Co., Ltd., amesimama karibu na kigari cha kunyanyua mizigo, akikagua kwa makini vifurushi vya plastiki ya fiberglass.
"Kwa siku tunaweza kupakia hadi kreti 160 za bidhaa za plasitiki ya fiberglass," Gaber aliiambia Xinhua. "Bidhaa hizi zenye matumizi mengi, kuanzia matumizi ya usafirishaji na ujenzi hadi petrokemikali, hutoka moja kwa moja kwenye kituo hiki hadi kwenye masoko makubwa ya kimataifa ikiwa ni pamoja na Ulaya, Marekani, na India."
Gaber alianza kufanya kazi ya kutafsiri kwenye kampuni hii ya Kichina, na sasa anasimamia timu ya watu zaidi ya 60.
"Nimepata uzoefu mkubwa wa kiufundi na kujifunza mbinu za usimamizi kutoka kwa wenzangu wa China," alisema.
Mwelekeo wake binafsi unaakisi ukuaji wa kampuni.
Wakati Gaber alipojiunga na kampuni hiyo mwaka 2013, kiwanda hicho hakikuwa na chochote zaidi ya kafeteria na mabweni tu. Leo, kimepanuka na kuwa kiwanda cha kisasa chenye zaidi ya mita za mraba 430,000.
Akinufaika na mpango wa kampuni unaotuma wafanyakazi wa Misri kwenye makao makuu ya Jushi nchini China kwa ajili ya mafunzo, Gaber amekuja nchini China kwa safari tatu tofauti za masomo.
"Mwanzoni, nilikuwa sijazoea mtindo wa kazi wa haraka na wenye ufanisi mkubwa wa wenzangu Wachina," Gaber alikumbuka huku akitabasamu. "Lakini baada ya kukaa nao pamoja kwa muda, polepole nilianza kujifunza, na pia niliwaonesha tabia nzuri za kufanya kazi za Misri."
Mshikamano huu mkubwa wa kitamaduni umeonekana moja kwa moja na Jin Yiqun, mhandisi wa teknolojia ya bidhaa ambaye alijiunga na kampuni tanzu ya Misri mwaka 2016.
Alipofika tu, Jin alifurahi sana alipogundua kuwa wasimamizi wawili wakuu wa karakana hiyo ni wanafunzi wa zamani ambao aliwahi kuwafundisha binafsi huko China.
"Leo, wote wamekuwa nguzo kuu zinazoweza kujisimamia. Jambo hili mara moja lilinipa hisia kubwa ya kufahamiana na uchangamfu huku nikifanya kazi pamoja na wenzangu wa Misri maelfu ya maili kutoka nyumbani," Jin aliiambia Xinhua.
Baada ya kufanya kazi pamoja kwa muongo mmoja, timu imekuwa na mawasiliano mepesi, Jin alisema. "Wakati mwingine maneno machache ya kawaida, au hata kuangalia mara moja tu, ilitosha kuelewa mtu mwingine anamaanisha nini."
Kampuni ya Jushi ya Misri iko ndani ya Eneo la Ushirikiano wa Kiuchumi na Biashara la TEDA Suez la China na Misri (Eneo la Ushirikiano la TEDA), mradi muhimu chini ya Mpango wa Ukanda Mmoja, Njia Moja uliopendekezwa na China. Kufikia mwishoni mwa 2025, eneo la viwanda lilikuwa limevutia zaidi ya biashara 200, na kuleta moja kwa moja zaidi ya fursa za ajira 10,000 kwa wenyeji.
Wakati yakiendelea kuboresha sekta ya utengenezaji ya Misri, makampuni ya China wakati huo huo yananoa watu wengi wenye ujuzi kwa ajili ya mahitaji ya viwanda ya baadaye ya nchi hiyo.
Katika eneo la viwanda, karakana ya uzalishaji wa mashine za kuosha vyombo ya Midea (Misri) Kitchen & Water Heater Appliances Co., Ltd. ina shughuli nyingi. Maryam Ibrahim, mtaalamu wa udhibiti wa ubora wa Misri, anaongoza timu yake na kupita kwenye safu za uendeshaji wa mashine wakati wa mafunzo ya kila wiki.
"Kampuni maarufu duniani imefunguliwa mlangoni pangu," alisema Maryam, ambaye alijiunga na Midea Group mwaka 2022 baada ya kusoma Kichina katika Chuo Kikuu cha Suez Canal cha Misri.
Maryam amepanda ngazi ya kitaaluma akienda sambamba na upanuzi wa kasi wa kiwanda. Alishuhudia mashine ya kwanza ya kuosha vyombo ikianza kutumika mwezi Machi 2023. Leo, karakana hiyo inajivunia uzalishaji wa kila mwaka wa vitengo 350,000, na Maryam amepanda hadi kuwa mkuu wa idara ya ukaguzi wa ubora.
"Maadili makali ya kazi, msisitizo wa kazi ya pamoja, na kumweka mteja mbele... haya ndio mambo yote niliyojifunza kutoka kwa wenzangu wa China," Maryam alisema.
Kukiwa hakuna viwango vya ukaguzi wa ubora vya ndani kwa mashine za kisasa za kuosha vyombo nchini Misri, Maryam alikwenda Foshan, Mkoa wa Guangdong, China, kwa mafunzo mwaka 2023. Kwa miezi miwili mfululizo, alijifunza upimaji wa mashine, akaandika viwango vya kiufundi, na kuboresha ujuzi mwingine muhimu.
Katika muda wake wa ziada, Maryam huwafunza lugha wenzake wa Kichina, na kukuza kujifunza kwa pamoja. Anabainisha kuwa mazingira ya tamaduni mbalimbali yamepanua mtazamo wake.
"Kwa kujifunza kuhusu tamaduni na historia tofauti, mtu anakuwa na ujasiri zaidi, na imeniwezesha kukua vizuri zaidi mimi mwenyewe binafsi," alisema.
Yang Yang, mkurugenzi wa uendeshaji na rasilimali watu katika kampuni ya Midea Misri, alisema kampuni hiyo kwa sasa imeajiri zaidi ya wafanyakazi 580 wa Misri.
"Zaidi ya asilimia 85 ya watendaji wa wakuu katika kampuni wamekua hatua kwa hatua kutoka nafasi za chini kabisa," Yang alisema.