SoC01 Vijana wauza matunda wamekwamia wapi kuboresha biashara?

SoC01 Vijana wauza matunda wamekwamia wapi kuboresha biashara?

Stories of Change - 2021 Competition

Prof Sankara

Member
Joined
Sep 17, 2021
Posts
6
Reaction score
10
Na Prof Sankara

Kitu gani unazingatia unapo nunua matunda?, ukubwa, rangi, utamu urahisi wa bei au mazingira yanapouzwa?.

Kwa asili kila biandamu hupenda huduma bora, hata hivyo kulingana na mazingira inawezekana mtu akalazimika kutumia huduma fulani iliyopo katika eneo lake kutokana na kutokuwa na huduma mbadala bora zaidi kwenye eneo lake.

Wafanya biashara wengi wa matunda huuza matunda kwenye meza za mbao, pembezoni mwa barabara, au karibu na baa, migahawa ya chakula na maeneo ya sokoni.

Mitaa na vichochoro vingi jijini Dar es salaam vimejaa meza za wauza matunda. Biashara ya matunda ni nzuri kama ilivyo umuhimu wa matunda kwa afya ya binadamu. Wanaofanya biashara za matunda ni vijana, wa kike na kiume ambao kwa jina rasmi tunawaita wajasiriamali wadogo.

Vijana wengi wameanza kuelewa dhana ya kujiajiri, wengi wao ni wasomi wa elimu ya juu, wameona fursa iliopo katika ujasiriamali. Hata hivyo bado kuna vijana wengi wana mtazamo tofauti kuhusu ushiriki wao katika biashara au kujiajiri wenyewe.

Makala haya yanaangazia fursa ya uuzaji wa matunda, inavyoweza kuwatoa vijana wengi kimaisha, na namna ya kuboresha biashara hii kuwa katika mfumo mzuri na rafiki kwa kuwavutia wateja. Namna serikali inavyoweza kuwasaidia vijana kuboresha biashara ya kuuza matunda kwa tija na maendeleo ya uchumi wa taifa.

Ubora wa huduma na mazingira yake

Mazingira ambayo matunda huuzwa, ni sehemu za wazi, ambapo vumbi huingia, wauzaji hawana kawaida ya kuosha matunda, na mazingira ni machafu, meza huwekwa juu ya mitaro ya maji machafu. Harufu mbaya ya maji machafu iliyopo katika eneo la biashara ni chanzo cha kuondoa umaridadi wa biashara. Tunafahamu kuwa wafanya biashara hawa wa matunda hulazimika kuweka biashara zao katika maeneo yenye watu wengi, hivyo kutokana na ufinyu wa maeneo hulazimika kuweka meza juu ya mitaro ya barabara ambayo chini imejaa maji machafu. Vumbi linalotimuka na jua kali vinaweza kuchangia kuondoa ubora wa matunda au hata kuondoa ladha, na kusababisha magonjwa.

Obadia Mrute ambaye ni mteja wa mtunda katika banda la matunda lilopo Kibamba, anasema “napenda kula matunda kama matikiti, nanasi, na ndizi, kila siku jioni nakuja hapa kula matunda. Sina haja ya kubeba matunda kupeleka nyumbani maana mimi ninaishi mwenyewe (sijaoa) hivyo nikimaliza naenda kula chakula cha usiku narudi geto.

Lakini mazingira ya huduma hii ya matunda hayaridhishi, mazingira machafu, wakati mwingine matunda yanakuwa yamechakaa kama ndizi kulegea na kuharibika, vumbi, na kutooshwa kwa matunda” Mrute anasema kuwa kutokana na kutokuwa na sehemu nyingine yenye mazingira mazuri kwa huduma ya matunda, analazimika kununua katika banda hilo lakini ukweli ni kwamba huduma hairidhishi.

Wauzaji wanasemaje?

Frank Charles Mjasiriamali wa matunda Mbezi anasema “kijana mwenye shahada ya kwanza anaona kazi kama hii haimfai, anataka kazi ya ofisini (kuajiriwa) pia kazi hii inahitaji muda mwingi zaidi, kuamka mapema kufuata bidhaa, unalazimka kuchelewa kufunga maana wateja ni wengi usiku, hivyo anaona bora kuajiriwa afanye kazi kwa masaa nane hadi tisa kwa siku”. Anasema kuwa “baadhi yao husingizia mitaji kitu ambacho siyo kweli, biashara ya matunda haihitaji pesa nyingi sana, mfano kama mimi nilianza na mtaji wa shilingi 30000 tu”.

Ni kweli nahitaji kuboresha biashara yangu lakini kutokana na bughudha za mara kwa mara, kutoka kwa mamlaka za serikali, zinasababisha nisiwe na utulivu. Kuhamishwa mara kwa mara, maana biashara yangu nimeiweka katika meza, kutokana na uwezo mdogo wa kugharamikia fremu, au kujenga matenti. Kama unvyojua biashara kama hii lazima iwepo katika eneo ambalo kunakuwa na mkusanyiko wa watu, anasema Frank.

Lameck Mzava ni muuzaji wa matunda eneo la Ubungo anasema kuwa “nimeanza biashara hii kwa mtaji wa shilingi 50000, na sasa ni miaka miwili. Kimsingi biashara hii imenisaidia kuendesha maisha, kama Napata mtaji mkubwa ninaweza kuiboresha biashara yangu zaidi.

Wataalam na wajiriamali

Daktari Kessy Mrema ambaye ni mjasiriamali anasema kuwa “Vijana wengi wana elimu ya kutosha lakini wanaendelea kubaki na mtazamo wa kuajiriwa. Wengi wanasingizia hawana mitaji, lakini ukweli ni kwamba mitaji siyo tatizo. Tatizo ni kwamba wanataka mitaji mikubwa wakati hawana uwezo wa kufanya biashara kubwa. Mfanya biashara yeyote aliyefanikiwa kibiashara lazima aanzie katika hatua ya chini na mtaji mdogo. Akiwa anaendelea kukua ndivyo anavyozidi kuimarika, kuitawala, kuijua biashara na kuipanua zaidi. Hakuna mfanya biashara aliyeanza na mtaji mkubwa hapa duniani”.

Lakini pia tatizo lingine linachangia vijana wengi kutojihusha na ujasiriamali ni mfumo wa malezi uliopo kwa sasa. Wazazi kupenda kuwasomesha watoto wao shule za bweni, ambapo mpaka anafika chuo kikuu anakuwa hana maarifa au uwezo aliojengewa na wazazi wa namna ya kujiajiri. Mfano sisi kipindi chetu tulienda shuleni tukiwa wakubwa, muda likizo unaweza ukalima bustani, kuuza vitumbua au karanga mitaani. Kazi hizo zilisaidia kutujengea uwezo wa kufanya biashara ndogondogo.

Na shuleni tulijifunza stadi za kazi kwa vitendo, kulima, kuchonga, kujenga nk. Leo masomo haya hayapewi kipaumbele shuleni. Ndiyo maana hatushangai kuona mhitimu wa chuo kikuu anashindwa hata kuanzisha genge, anasema Daktari Kesy.

Nini kifanyike.

Ili kufanikiwa kwa mjasiriamali lazima azidi kutafuta maarifa katika eneo analofanyia kazi, kuongeza ubinifu zaidi, na kuboresha huduma kwa wateja.

Wauzaji wa matunda kuongeza ubunifu wa kuongeza thamani katika biashara ya matunda. Kuweka mipango biashara ya muda mrefu, na kujua kubadilisha biashara kulingana na majira. Uuzaji wa matunda ni fursa pana kwa vijana, ni wakati wa kuacha aibu na kutegemea kuajiriwa, badala yake wajikite katika kutengeneza ajira na kuthubutu kuongeza thamni ya biashara zao.

Wito kwa serikali na wadau wa maendeleo

Kutokana na changamoto za wauza matunda kuwa ni kukosekana kwa mazingira rafiki na usumbufu wanaoupata kutoka kwa mamlaka za serikali katika biashara zao. Ni wakati sasa serikali kuwa na mpango madhubuti wa kuweka maeneo rasmi ya biashara za matunda.

Pawepo na utaratibu wa kutengenezewa mabanda au matenti rasmi ambayo watapangishwa kwa gharama nafuu. MfanoVETA au SIDO wanaweza kupewa kazi ya kuunda mabanda au matenti hayo. Faida ya uwepo wa mabanda hayo au matenti ni kupendezesha mji au mahali ambapo yatawekwa. Kwa maana kwamba sasa hivi hakuna muonekano rasmi kwa baadhi ya wafanya biashara. Faida nyingine ni urahisi wa ukusanyaji wa mapato ya serikali. Faida ya mwisho na muhimu ni usafi katika eneo la biashara.

Wawekezaji kujitokeza kwa kusaidia wauzaji wa matunda kufanya kazi zao katika mazingira mazuri. Mfano kuwepo na aina moja ya mabanda rasmi ya kuuzia matunda ambayo yataidhinishwa na serikali. Kama ilivyo kwa bucha za nyama kuna vigezo ambavyo serikali inavitaka kutimizwa ndipo uruhusiwe kufungua bucha. Kama vile vioo, jokofu, maji ya kuoshea matunda, na chumba kilichosakafiwa vizuri.

Kwa kufanya hivyo kutapandisha hadhi biashara ya matunda, kuepusha usumbufu wa mara kwa mara au kuhamishwa na kufukuzwa katika maeneo mfano pembezoni mwa barabara. Serikali itakuwa na mfumo mzuri wa ukusanyaji wa mapato na ukaguzi wa ubora wa huduma ya matunda.
 
Upvote 4
Back
Top Bottom