MAMLAKA ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), imeiomba Serikali katika hatua za mwisho zilizobaki za kumpata mzabuni wa kutengeneza vitambulisho hivyo, kutumia vyombo vya usalama wa Taifa kumpata mzabuni wa kuendesha mradi huo.
Mamlaka hiyo imetaka kutotumiwa kwa utaratibu wa zabuni za uwazi ili kuepuka kufikishwa mahakamani, pindi baadhi ya wazabuni wanaposhindwa.
Badala yake imetaka wabunge na wananchi waiamini Serikali na kukabidhi kazi hiyo kwa vyombo vya usalama vya Taifa kwa ajili ya kusimamia kumpata mzabuni ili kuepukana na hatari ya kufikishwa mahakamani na wazabuni, kama ilivyotokea Kenya pindi wazabuni wengine wanaposhindwa.
Tangu kutangazwa kwa zabuni hiyo ya kutengeneza vitambulisho, wazabuni 104 walijitokeza, lakini 54 walitoweka, baada ya kuona ugumu wa kazi hiyo na sasa wamebaki watano ambapo Julai mwaka huu taratibu za zabuni zimepangwa kuendelea.
Akitoa mada juu ya maendeleo ya mradi huo kwa wabunge, Mkurugenzi Mkuu wa NIDA, Dickson Maimu, alisema "nawaomba tuiamini Serikali tusifanye zabuni ya wazi, wenzetu wa Uganda hawajafanya na Kenya walifanya kwa uwazi, matokeo yake wamefikishwa mahakamani, mimi nawaomba tuviachie vyombo vyetu vya usalama visimamie vitambulisho hivi".
Wabunge wengi walikubaliana na ombi hilo na kutaka kazi ya mwisho ya kumpata mzabuni ifanywe na Baraza la Usalama la Taifa ambalo limeonekana kuangalia zaidi maslahi ya Taifa.
Mbunge wa Maswa, John Shibuda (CCM) alisema "naomba suala la vitambulisho lipelekwe kwenye Baraza la Usalama la Taifa, likiendelea kuwa katika zabuni ya wazi hatutafika popote, kutokana na umimi na maslahi binafsi. Watu wengine wakikosa zabuni wanakwenda kushitaki wakidai zabuni haikuwa ya wazi."
Alisema katika Baraza la Usalama la Taifa hakuna umimi bali maslahi ya Taifa pekee na kuongeza: "mbona vifaa vya Jeshi havitangazwi? Nawaomba suala la vitambulisho liondoke kwenye zabuni ya wazi. Sisi tuna maneno matamu mengi, utekelezaji shida.Tukiendelea na masuala ya siasa tutakuwa tukijihujumu wenyewe."
Mbunge wa Mtera, John Malecela (CCM), aliitaka Nida kulimaliza suala hilo la vitambulisho ndani ya Serikali na kuhadharisha kuwa baadhi ya wazabuni ndio wamiliki wa vyombo vya habari na hivyo wakishindwa, watavitumia vyombo vyao kuichafua Serikali.
Alitaka vitambulisho hivyo kutotengenezwa Korea Kusini na kusisitiza: "Nahadharisha vitambulisho kupelekwa Korea Kusini, kwa sababu ni matapeli wakubwa. Singapore ndio namba moja, wao wamekuwa na vitambulisho hivyo miaka mingi na wamefika mbali".
Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed (CUF) aliitaka Mamlaka hiyo, kukusanya takwimu za kutosha kwa kutumia watu wenye taaluma hiyo, ili kuepuka dosari katika mpango wa utoaji wa vitambulisho vya Taifa.
Mbunge wa Karatu, Dk Wilbroad Slaa (Chadema) mbali na kukubali suala hilo kumalizwa serikalini kwa kusimamiwa na vyombo vya usalama, alitaka hatua zote za kuaminiana ziwepo na kusema Bunge kupitia kamati zake, lina haki ya kuingilia kama kutakuwa na matumizi mabaya.
Mbunge wa Rombo, Basil Mramba (CCM) alisema "Maimu nakushauri tumia sheria kwa kasi, kwani ipo siku utakuja kunyongwa".
Katika maelezo yake kuhusu mradi huo, Maimu alisema katika kampuni tano zilizobaki, hakuna ya Korea Kusini na kusema mradi huo utagharimu Sh bilioni 200 na utakuwa wa miaka mitatu kwa mujibu wa ratiba ya utekelezaji iliyopitishwa na Serikali.
Alisema Serikali imepata mkopo kutoka Korea Kusini wa Sh bilioni 41 kwa ajili ya kujenga kituo cha kuhifadhi takwimu. Mkopo huo utalipwa kwa miaka 40 kwa riba ya asilimia 0.2.
Alisema vitambulisho hivyo vingekuwa vimeshaanza vingeokoa gharama za uandikishaji wapiga kura ambapo Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) imetumia Sh bilioni 42.9 kusafisha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, na kuongeza "hata Msajili alipotaka kuhakiki wanachama ingemsaidia, ingeongeza ukusanyaji mapato".
Alisema mradi huo utakapokamilika, utakuwa na kadi za aina tatu kwa mfumo wa smart card na zitatolewa kwa Watanzania, wageni na wakimbizi.
Katika taarifa zitakazojumuishwa za mtu ni pamoja na makazi yake, ndoa, umri na zitatumika pia katika upatikanaji wa leseni za kuendesha gari, mifuko ya hifadhi ya jamii na kuisaidia Serikali kufahamu mapato ya kampuni kama za simu za mkononi.
Source: Habari Leo