KERO Vitisho toka kwa M/Kiti wa Kitongoji cha Itumbi (Mbeya) kwa wakazi wa Majengo-Mapya

KERO Vitisho toka kwa M/Kiti wa Kitongoji cha Itumbi (Mbeya) kwa wakazi wa Majengo-Mapya

Hii ni kero ambayo mwananchi ameiwasilisha JF akitaka wahusika kuchukua hatua
A

Anonymous

Guest
UTANGULIZI

Mtaa wa Majengo mapya_Jeshini, unapatikana Mkoani Mbeya, wilaya ya Chunya, kata ya Matundasi, kitongoji cha Itumbi.

HISTORIA YA ENEO

Hili ni eneo ni mojawapo nchini ambalo liliteuliwa kuwa kambi ya kijeshi ya wapigania uhuru kusini mwa Afrika.

Mara baada ya shughuli kumalizika, walikuja watu na kuanza kuishi maeneo hayo huku shughuli zao zikiwa ni kilimo na ufugaji.

Mnamo mwaka 2007 na 2013 serikali ya kijiji iliwapatia wawekezaji baadhi ya maeneo hayo kwa shughuli za uchimbaji madini ya dhahabu.

Shughuli za uchimbaji madini zilipelekea kuongezeka idadi ya watu. Na wakazi walioongezeka walijenga makazi yasiyoyakudumu kwa kutumia mabati namaturubai ndani ya eneo la wakata leseni ya uchimbaji madini.

Idadi ya watu wazima na watoto ilipozidi kuongezeka eneo hilo, ilisababisha kwa baadhi ya wawekezaji wenye leseni ndogo za uchimbaji kuingiwa na hofu ya kuporwa maeneo yao na serikali, kupitia mchakato wa kurasimisha kuwa kijiji. Hivyo hofu yao ilifanya watoe tangazo la kuwafukuza wakazi wanaoishi ndani ya maeneo yao.

Wananchi waliopata taarifa ya kuhamishwa kutoka katika maeneo ya wawekezaji, waliwaomba wenyeji(waliotangulia kuja kabla shughuli za uchimbaji madini) maeneo watakayoweza kujenga nyumba za kudumu.

USALAMA WA ENEO

Eneo bado ni hatarishi kwa shughuli za makazi na kiuchumi (kilimo,ufugaji na uchimbaji madini) kutokana na uwepo wa masalia ya mabomu.

Licha ya kuwepo kwa jitihada za wakazi kushirikiana na vyombo vya usalama kutegua mabomu yanayopatikana, bado elimu ya kutambua masalia hayo haijatolewa ipasavyo.

Hadi sasa kuna historia ya kifo cha mtoto mmoja aliyekufa kwa kuchezea bomu lililosalia pasipo yeye kutambua.

KERO YA WAKAZI WA MAJENGO MAPYA

Wakazi wanaulalamikia uongozi wa serikali ya kitongoji cha Itumbi kutokana na Mwenyekiti wa kitongoji hicho akishirikiana na mjumbe wa uenezi CCM kata, anawatishia wananchi akiongozana na maofisa wa JWTZ kuwa wanapaswa kuondoka eneo hilo kwa sababu zifuatazo;

1. Eneo ni mali ya jeshi la wananchi la Tanzania
2. Eneo ni kituo cha utalii wa makumbusho ya wapigania uhuru
3. Eneo sio salama kwa makazi na shughuli za kiuchumi

Wakazi mara baada ya kupokea hoja hizo waliitisha mkutano wa hadhara pamoja na M/kiti wa kitongoji cha Itumbi. Mkutano huo hakumalizika kutokana na vurugu zilizotokea pindi M/kiti aliposhindwa kujibu maswali aliyoulizwa..

Wananchi wa Majengo mapya, wana hoja zifuatazo kwa mkuu wa wilaya:

1. Mkuu wa wilaya ana taarifa za wakazi wa hapo wanapaswa kuhama?

2. Ikiwa eneo si salama kwa makazi wala shughuli za kiuchumi, kwanini wanaofukuzwa ni wakazi tu, lakini wanaomiliki migodi na wachimbaji madini maeneo hayo hawafukuzwi?

3. Ombi la wakazi kuomba kikosi cha jeshi la wananchi kuja kukagua masalia ya mabomu kwa mitambo yao maalumu litatekelezwa lini?

4. Uwepo wa taarifa kinzani kutoka kwa maofisa wa jeshi la JWTZ kuhusu umiliki wa eneo hilo, wapo waliosema eneo ni mali ya serikali ya kijiji na wapo wnaosema ni la kwao, je ukweli ni upi?

Baadhi ya wakazi wanadai sababu kuu ya wao kufukuzwa, na matajiri wanaochimba dhahabu kuachwa, ni jambo la rushwa linaloendelea baina ya wawekezaji na Mwenyekiti wa kitongoji cha Itumbi.

Zipo taarifa hazijathibitishwa bado kuwa Mwenyekiti wa kitongoji ameuza eneo wanaloishi wakazi kwa mwekezaji, hivyo analazimisha watu kuhama ili mwekezaji aanze uchimbaji madini.

Wananchi wamejitahidi kutafuta mawasiliano ya mkuu wa wilaya wa Chunya, kuomba ahadi ya kukutana naye bila mafanikio.

OMBI LA WAKAZI KWA SERIKALI YA RAIS MAMA SAMIA

Wakazi wanaomba yafuatayo kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan:

1. Waruhusiwe kuishi eneo hilo, kwa kua wanalitegemea katika shughuli za kimalazi na uchumi.

2. Wapewe eneo la kujenga shule na zahanati; Wakazi wamekiri kuwa idadi ya watoto wa hapo ni kubwa wanapata changamoto kutembea umbali mrefu kwenda shuleni, pia huduma za afya ziko mbali.

3. Jeshi la JWTZ kushirikiana na vikosi vya usalama viende kukagua masalia ya mabomu yaliyobakia, pia kutoa elimu zaidi ya utambuzi wa mabomu kwa wananchi.

4. Haki itendeke kwa wakazi na wawekezaji wa uchimbaji madini ikiwa eneo litaonekana si salama kwa makazi au shughuli za kiuchumi mfano uchimbaji madini ya dhahabu.

Msemaji Mkuu wa wakazi wa eneo hilo, amesema yeye pamoja na wakazi wa eneo hilo, wapo tayari kushirikiana na vyombo vya usalama ili kuhakikisha masalia ya mabomu hayaleti madhara kwa wananchi.

KANISA.jpg
Makazi.jpg
Chd2.jpg
Pht33.jpg
Pht5.jpg
 
Serikali bado ipo Yanga Day, itawasikiliza yakianza kuwalipukia kama yale ya Mbagala
 
Back
Top Bottom