SoC01 Vituo vya kilimo atamizi (incubation centres): Njia ya kuongeza uzalishaji pamoja na kuinua kipato kwa vijana Tanzania

SoC01 Vituo vya kilimo atamizi (incubation centres): Njia ya kuongeza uzalishaji pamoja na kuinua kipato kwa vijana Tanzania

Stories of Change - 2021 Competition

Akwinox_Nico

New Member
Joined
Jul 15, 2021
Posts
3
Reaction score
0
Andiko langu linaanza kwa kusema Tanzania inaweza kuwa nchi nambari moja duniani katika ujenzi wa ajira nyingi kwa vijana na kila mtu akabaki akijiuliza imekuweje kwa muda mfupi namna hii?. Nchi ya Tanzania sio nchi ya kulia njaa kila siku, sio nchi ya kutembeza bakuli na kuomba misaada isiyokwisha huku ikiwa na kila kitu. Tuna ardhi iliyo bora kabisa (Ardhi hii ukikata kidole na kukipanda walahi kinaota na sijajua litatoa zao gani lakini nina uhakika kitaota tu kutokana na rutuba iliyo nzuri), misitu, mito, wanyama pori, milima ya kuvutia, lakini kikubwa sana ni rasilimali watu. Tunao watu zaidi ya milioni 45 kwa makadirio lakini nina uhakika kama hatutafanya kukadiria na kuhesabu vizuri kabisa kila mmoja basi tunaweza kuwa na idadi kubwa zaidi ya hii inayotajwa kwenye maandishi.

Nianze kwa kutoa pongezi kwa yote yaliyofanyika na viongozi wetu hasa kuanzia awamu ya kwanza hadi aawamu ya sasa. Kiukweli kabisa wamefanya mengi mazuri kwa utashi wao na nguvu zao walizopewa na mwenyezi Mungu. Na sipo hapa kukosoa chochote kilichofanyika bali kuongezea mchango wangu mdogo katika kupunguza msongamano wa vijana wasiokuwa na ajira lakini pia kuboresha thamani ya kilimo.

Mawazo ya andiko langu yamesukumwa kwa kiasi kikubwa na uzoefu wangu wa kuandika miradi midogo midogo (hususani mijini na vijijini) ambayo imekuwa ikiwanufaisha wachache na hivyo kufanya kusiwepo na matokeo makubwa na chanya kwa ajili ya kubadirisha hali za vipato hasa kwa jamii masikini ambazo maisha yao yamekuwa ya dhiki kwa muda mrefu sana.

Kumekuwepo ongezeko kubwa sana la vijana wanaomaliza elimu mbalimbali na kuishia kuwepo mitaani bila kufanya kazi na matokeo yake ni kuongezeka kwa matukio ya kiharifu na kuvunjika kwa amani. Ifahamike tu kuwa Serikali imekuwa ikifanya mambo mengi kujaribu kuongeza ajira na kuboresha kilimo lakini bado matokeo yake hayajaweza kuinua vijana.

Andiko hili limejikita katika kupendekeza mambo yafuatayo;-
(a) Serikali ikae chini na wataalamu wa ardhi ili waweze kwanza kutambua ardhi ambayo iko wazi kwa ajili ya kuanzisha vituo atamizi vya kilimo na baada ya hapo watengeneza ramani ya matumizi ya ardhi kutokana na ukanda (agricultural zones) mfano inaweza kuwa ukanda wa kati, ukanda wa nyanda za juu kusini, ukanda wa magharibi na kadharika.

(b) Serikali ikubali kuingiza pesa katika kuanzisha miundombinu ya kimkakakati kama vile kutengeneza makazi ambayo sio ya kudumu (farm houses) kwa ajili ya vijana watakaokuwa wanaishi hapo kwenye vituo atamizi, yachimbwe mabwawa ya umwagiliaji, iwekwe miundombinu mizuri ya barabara, mifumo mizuri ya masoko iandaliwe, kiwanda kidogo cha kusindika, kuwepo na majokofu ya kuhifadhia vyakula (chillers/coldrooms), maghala ya kuhifadhia vyakula. Kuwepo pia na huduma chache za kukuza vipaji kama vile viwanja vya michezo, kituo cha afya, huduma za ibada, kituo cha polisi, kuwepo na kituo kidogo cha vijana kujifundisha maswala ya utawala na uzalendo (leadership & citizenship centre).

Kuna mtu anasoma hapa na anaweza kusema mbona kama hivi vitu vitakuwa haviwezekani na kwamba vitaipa serikali mzigo mkubwa na kwanini vianzishwe wakati tayari kuna vituo vya mafunzo ya kilimo? Jibu ni kwamba vituo hivi bado vinafundisha na kuwaacha vijana warudi makwao na kuanza kutafuta ajira mtaani.

Tofauti ya Vituo Atamishi ni kwamba kijana tayari anakuwa amekwishaingia kwenye mfumo rasmi wa ajira kuanzia siku ya kwanza anafika kwenye kituo husika. Swali jingine linaweza kuwa, je huu mpango utaanzaje? Serikali kwanza lazima ichague ukanda mmoja ambao utakuwa ndio sehemu ya kufanyia majaribio (pilots study). Baada ya hapo ikishirikiana na wataalamu wake, itabidi kutengeneza orodha ya angalau vijana elfu 5-10 nchi nzima ambao watatoka katika kila Mkoa wa Tanzania na kuwekwa kwenye kituo husika na watapewa jina la Cohort 1.

Uchaguliwaji wa vijana husika utatokana na nini walichosomea vyuoni mwao. Tunategemea kuwepo na wahandisi wa aina mbalimbali, waliosomea kilimo kwa ujumla, masoko na uchumi, waliosomea usafirishaji, ughavi na ununuzi, wataalamu wa chakula na usindikaji, wataalamu wa wadudu na udongo, wataalamu wa fedha.

Hawa wote watakuwa chini ya usimamizi wa mkuu wa Kituo Atamizi ambaye atawajibika kwenye wizara husika itakayokuwa imepewa majukumu ya kusimamia.

Swali kuu litakuwa ni kwa namna gani Serikali pamoja na vijana husika watanufaika na uwepo wao ndani ya vituo atamishi? Ili uweze kuwa mnufaikaji wa mpango huu ni lazima kukubali ukweli kuwa hakuna kitu cha bure na hata maandiko matakatifu yanasema asiyefanya kazi na asile.

Hapa Serikali itachukua 40% ya faida ya mauzo yatakayopatikana huku 60% ikibakia katika kuendesha kituo hadi hapo serikali itakapokuwa imerudisha fedha zake za uwekezaji na baada ya hapo kituo kitaanza kujiendesha chenyewe na kupata 100% ya faida yote huku usimamizi bado ukiwa mikononi mwa serikali. Ikumbukwe tu kuwa hapa kinachotaka kufanyika ni kwanza kuwahakikishia vijana ajira na huku wakiendelea kukuza ujuzi wao kwa vitendo na wakati huo huo wakiwa na uhakika wa malazi, chakula na mshahara. Kuhakikisha vijana wanafanya kazi kweli na kuzalisha, kutakuwa na mpango maalamu ulioanzishwa na wataalamu waandamizi ambao watafanya kazi kwa ukaribu sana na wanufaika husika ili pia kuhakikisha hakutokei uzembe.

Ndani ya Kituo Hatamishi kutakuwa na uzalishaji wa mazao kuanzia ya muda mfupi na muda mrefu na hii itatokana na namna mpango utakavyokuwa umewekwa. Lengo hapa ni kuhakikisha kituo kinaanza kujilisha chenyewe ndani ya muda mfupi bila kuitegemea Serikali. Moja kati ya uwekezaji wa kifedha ambao Serikali itaweka ni kuhudumia kituo ndani ya mwaka mmoja na baada ya hapo kila kitu kitakuwa chini ya kituo chenyewe.

Swali gumu ambalo hata mwandishi wa andiko hili nilikuwa najiuliza ni je kwanini Serikali isiwape tu mitaji vijana na kujikita kwenye uzalishaji kama ilivyoelezwa ndani hapa? jibu lake ni kwamba ukishawapa mitaji vijana watajikuta wameingia kwenye mzunguko ule ule wa kimasikini maana hawatapewa mitaji ya kutosha ili kufanya kilimo biashara na wengi wao wataishia tu kupata hasara kwa maana hawatakuwa na nyenzo bora za uzalishaji na pia hawatakuwa na uhakika wa masoko yao.

Uzuri wa mpango huu ni kwamba Serikali ndo mlezi mkuu na itawekeza fedha nyingi ili kuhakikisha kituo kinasonga mbele. Maana yake ni kwamba uhakika wa masoko pamoja na kujitangaza hata nje ya nchi utakuwa mkubwa sana. Hii pia itasaidia katika kuwawajibisha wale ambao watakuwa wazembe na kufuja miundo mbinu iliyowekwa kwa manufaa mapana ya kituo kizima.

Huu mpango utakuwa wa miaka minne hadi mitano itategemea na namna gani Serikali itaamua kuuendesha. Kila mwaka kituo kitapokea vijana wapya ambao wataingia kwenye mfumo na kumaliza kipindi chao katika muda uliopangwa. Kwa wale ambao watakuwa wanafanya vizuri basi watapewa ajira za kudumu kwenye vituo husika kwa maana tayari Serikali itakuwa imeshaanzisha Vituo Atamishi kwenye zones nyingine na vituo vyote vitatumia masomo waliopata kutoka kituo namba moja.

Wale wanaofanya vizuri ndio watakwenda kuwa walimu kwenye vituo vipya na mzunguko unakuwa kwa namna hiyo. Imani ya andiko hili ni kwamba baada ya miaka 20, kutakuwa na vituo vingi sana karibia kila kanda muhimu ili kuwapika vijana waweze kuwa na uhakika wa ajira pamoja na kujiongezea ujuzi mbalimbali baada ya kumaliza masomo yao.

Uzuri mwingine wa vituo hivi ni kuwa vitatumika kama sehemu za kukuzia vipaji kwa vijana hasa wale wa miaka kuanzia 12-17 kwa kuwawekea miundombinu rafiki kwa wao kukuza vipaji vyao na kuitwa akademia ya michezo (sports academy). Hawa vijana watachukuliwa kutoka maeneo jirani na vituo na hawatakuwa wakiishi kwenye vituo bali watatokea majumbani mwao kwa utaratibu maalumu utakaokuwa umewekwa.

Kutakuwa na program maalumu ya kuwafundisha vijana lugha nyingine za kigeni pamoja na kuwafundisha namna ya kuongea hasa pale wanapokuwa wamepewa nafasi za kuongea mbele za watu. Elimu hii ya ziada haijawekewa sana msisitizo kwenye mitaala ya shule na vyuo na inafanya vijana wahitimu masomo yao lakini wasiwe na ujuzi wa kujieleza pale wapewapo nafasi.

Uzuri mwingine wa kuwepo vituo vya namna hii nchini ni kupunguza nadharia na kuongeza vitendo lakini pia kuongeza tija ya uzalishaji kwa kuhakikishiwa masoko ya bidhaa zitakazozalishwa hapa mfano;- mbogamboga, nafaka za aina mbalimbali, maziwa, nyama, matunda ya aina mbalimbali, miti ya kitafiti ya kisayansi na mazao mengine mengi yatakayozalishwa kutokana na ukanda husika. Mashamba yote yatafungwa mifumo ya umwagiliaji pamoja na mfumo wa jua (solar power) ili kusaidia katika umwagiliaji na kuhakikisha kilimo kinakuwa endelevu muda wote bila kutegemea mvua ambazo kwa kiasi kikubwa zimekuwa sio za uhakika kumsaidia mkulima katika uzalishaji wake.

Mwisho, nihitimishe kwa kusema kuwa, kila kitu kinaweza kufanyika kukiwa na uongozi imara na wenye maono ya kuangalia mbali. Kikubwa ni kujaribu kwanza kuona nini kinaweza kuzuia jambo lisifanyike na kutafuta namna bora ya kuweza kuboresha. Bado naamini kuwa kilimo ndo sekta muhimu kwa sasa ambayo inaweza kutengeneza ajira nyingi sana hasa kwa vijana na kuwawezesha kujikwamua katika utegemezi.

Ni imani yangu kuwa Serikali itatengeneza miundombinu mizuri ya kiuzalishaji na kiusafirishaji pamoja na kupanua masoko nje ya nchi na kwa kuanza inaweza anza na nchi zinazoizunguka Tanzania, baadaye Afrika na hatimaye kuishangaza dunia nzima kwa kuilisha chakula kutoka kwenye hivi Vituo Atamishi ambavyo kwa miaka 20 ijayo vitakuwa na uwezo mkubwa sana wa uzalishaji kwa kusimamiwa na uongozi ulio imara na usiopenda kuendelea kuwa omba omba wakati kila kitu tunacho na nchi yetu bado ina ardhi nzuri sana ya uzalishaji. Kama ziada, vituo hivi vitachagiza ukuaji wa miji midogo iliyoko jirani kabisa na maeneo ambayo vituo hivi vitaanzishwa. Ramani nzima ya kituo itachorwa chini utekelezaji unafuata.
 
Upvote 3
Back
Top Bottom