Ndugu mteja,
Una tatizo lolote unapotumia mtandao wetu? Una ushauri wowote ili tuiboreshe huduma yetu?
Tafadhali itumie mada (thread) hii ili tukusaidie kwa urahisi.
Unapokuwa na tatizo, ili tukusaidie kirahisi zingatia haya:
- Ni tatizo gani? (M-PESA, SMS, Calls, Internet, usajili, kukatika kwa mawasiliano n.k)
- Maeneo gani? (Tukifahamu location, inakuwa rahisi kukuelekeza wapi uende ili upate physical assitance toka kwa vendor wetu aliye karibu nawe)
- Tatizo limeanza lini na limejirudia au kuendelea kuwa kero kwako kwa muda gani?
- Kama ni ushauri, zingatia ya juu lakini tutafurahi tukijua kwanini unapendekeza unachopendekeza
- Kama ni pongezi, zingatia ya juu na tungependa pia upendekeze lipi tufanye kuzidi kuiboresha huduma kwako.
Karibu
Vodacom Tanzania
MATUMIZI MABAYA YA MUDA... SIKU MBILI KUSUBIRI HUDUMA KUSHUGHULIKIWA..
5A1812TDNXC Imethibitishwa
tarehe 1/1/18 saa 8:53 PM Pokea kiasi cha Tsh50,000.00 kutoka kwa 190242 - EMMANUEL MAGUFU BWIRE Salio lako jipya la M-Pesa ni Tsh ×××××××
Huo ni ujumbe ambao niliuopokea siku ya tarehe 1.1.2018 saa 8:53 kutoka Vodacom M-PESA baada ya kutoa kiasi cha Tsh50,000.00 kwa wakala.. Kwa bahati mbaya sana, nilikuwa nimekosea kujaza namba za WAKALA ambae nilikuwa nipo ofisini kwake..
Saa 8:58PM nikagundua kwamba nimetoa pesa kimakosa (kukosea namba ya wakala) baada ya kuona mrejesho wa ujumbe huo (hapo juu). Yule mtoa huduma akawapigia simu HUDUMA KWA WATEJA. akaelezwa kwamba nipige mimi mwenyewe. Nikapiga mwenyewe. Wakapokea. Nikaeleza shida yangu.
Yule Dada aliyepokea simu yangu akaniuliza maswali kadhaa; unaitwa nani? Umesajili kutumia kitambulisho gani? Tarehe, mwezi, mwaka wako wa kuzaliwa? Kiasi ulichotoa? Kilichobaki? Jina la wakala uliyetuma.. Nikampa vyote. Nikasubiri maelezo kutoka kwake. Yule mtoa huduma.
Akanipa jibu kwamba; "subiri ndani ya saa 2, tutakureshea fedha zako, baada ya kukamilisha uchunguzi wetu, Je una tatizo lingine tafadhali, tukupe msaada wetu?" nikamjibu "Hapana, ni hilo tu dada yangu" akaniaga na kukata simu yake..., nilisubiri huo muda, hadi nikaona balaa tupu..
LEO NIKAAMKA NAO TENA
Leo tarehe 2.2.2018 saa 8:46PM baada ya kuona pesa yangu haijarejeshwa nikawapigia HUDUMA KWA WATEJA. akapokea mwanamke, nikampa shida yangu, akanieleza kwamba kwa tatizo hilo, pesa zinarejeshwa BAADA YA SAA 48 kupita.., hivyo nisubiri siku mbili ili kurejeshwa kwa hizo pesa.
Nisubiri saa 48 pesa kurejeshwa? Pesa ambazo nimetoa mimi mwenyewe? Nimekosea, dakika chache nimetoa taarifa, zimezuiwa, naambiwa nisubiri siku mbili kupata pesa hizo? Siku mbili? Kwamba shughuli husika za pesa hiyo zisimame kwa siku mbili? Kwamba VODACOM mmekosa kabisa verification and authentication kwenye hilo?
Usafiri wa anga (bird fly) umbali mfupi kati ya Kenya na USA ni 13,733KM = 8,533 miles. Kama ukisafiri kwa ndege (yenye wastani wa spidi ya 560 miles) kutoka Kenya kwenda USA, itakuchukua saa 15.24 kufika USA.. Bado VODACOM wanasubiri saa 48 kushughulika na suala lako.
Bandari ya Los Angeles iliyopo katika fukwe za San Pedro Magharibi ya Marekani katika jimbo la California ina hekari 7,500 na maili 43. Inahesabika kama bandari namba 19 kwa shughuli nyingi. Inakadiriwa kwamba zaidi ya $1.2bn thamani ya mizigo inasafirishwa kutoka bandari hiyo KILA SIKU.. Vodacom wanataka saa 48 kushughulika tatizo la mteja mmoja.
MATUMIZI YA SAA 48 (SIKU MBILI)
Saa 48 ni safari ya kutoka MWANZA kwenda MBEYA kwa usafiri wa umma (bus). Safari Yenye uchovu mwingi sana. Utafika Mwanza saa 4 asubuhi.
Saa 48 ni safari ya kutoka DSM kwenda KIGOMA kwa njia ya reli kwa usafiri wa Gari Moshi. Unatumia siku mbili njiani ukiwa kwenye gari Moshi. Ukiwa porini.
Saa 48 muda wa kusafiri kwa basi kutoka DSM kwenda Afrika ya kusini. Unatumia siku mbili kuitafuta Afrika kusini ukivuka mipaka ya nchi kadhaa.
Saa 48 kiwanda cha VOLKSWAGEN cha Ujerumani, kinatumia kuzalisha magari zaidi ya 2,400 kwenye kiwanda kimoja kwa uzalishaji wa kawaida.
Saa 48 bandari ya Singapore inapakua na kupakia zaidi ya tani 1,000 za mizigo katika bandari hiyo kutoka na kuingia Singapore. Moja kati ya bandari zenye shughuli nyingi ulimwenguni.
Saa 48 ni muda ambao 2PAC aliutumia kurekodi wimbo wake wa CALIFORNIA LOVE baada ya kutoka Jela, akimshirikisha Dr Dre kwenye albamu ya All eyez on me (1996)kwenye studio za DEATH ROW za SUGE KNIGHT. Wimbo wa Dunia.
Saa 48 ni muda wa shughuli za kiwanda cha BAKHRESA FOOD PRODUCTS kuzalisha bidhaa, kupakia mizigo na kusafirisha kwenda kwa wateja wake wenye kuhitaji bidhaa kutoka viwandani.
Ingawa saa 48 hizo wakuu wa wilaya/mikoa wanatumia kama fimbo, wanatumia saa hizo kwa amri zao kuwaweka raia mahabusu kabla ya kufikishwa mahakama. Sheria za kukoloni.
INGELIKUWA VIPI KAMA......
Ingelikuwa vipi; kama fedha hizo nakwenda kulipa huduma za matibabu hospitali? Mgonjwa wangu angesubiri siku mbili ili fedha zirejee? Siku mbili anasubiri muamala. Loh!
Ingelikuwa vipi; kama fedha hizo ningelikuwa natakiwa kutuma ada ya chuo/shule? Mwanafunzi angelifukuzwa shule hadi pesa hizo zitoke baada ya siku mbili?
Ingelikuwa vipi; kama fedha hizo nadaiwa kodi ya pango? pango la bishara au nyumbani, Ningesubiri siku mbili wakati huo 'mazagazaga' yangu yakiwa nje ya pango hilo?
Ingelikuwa vipi; kama fedha hizo ni kwa ajili ya kupeleka dhamana mahakamani? Mtu wangu angekosa dhamana au faini hiyo ili apelekwe 'giningini' huko ngome?
Ingelikuwa vipi; kama fedha hiyo ni nauli ya kutoka IRINGA kwenda TARIME kwetu kuwahi mazishi ya ndugu, rafiki, jamaa yangu? Ningesubiri siku mbili pesa irejeshwe?
NAFIKIRI; Tunatumia muda mwingi sana kushughulika na huduma za wateja, tena kwa kutumia 'hours' na sio 'hour'. Kama kweli tunataka kuwa taifa lenye kutafuta uchumi wa kati wa viwanda, tuache urasimu wa muda.. Bado naendelea kusubiri pesa kurejeshwa.. Hadi sasa. KULOSTISHANA tu.
Mwisho; mkirejesha, rudisheni na ile 'fee' ya kutuma ambayo mliikata wakati natuma hiyo pesa. Maana sio mnachukua 'ada' kwenye huduma ambayo inatakiwa kufanyiwa marejeo.. Rejesheni mpunga wangu wote.. Na ile Ada ya kutuma.. Naendelea kusubiri saa 48.
____________________________________
[emoji767] Martin Maranja Masese (MMM)