Vumbi linalotokana na Ujenzi wa Barabara ya Nsalaga - Ifisi, Mbeya limekuwa na athari kubwa kwa Watu

Vumbi linalotokana na Ujenzi wa Barabara ya Nsalaga - Ifisi, Mbeya limekuwa na athari kubwa kwa Watu

UTPC

Journalists' Union
Joined
Apr 17, 2026
Posts
51
Reaction score
38
Wakati ujenzi wa barabara ya njia nne kutoka Nsalaga hadi Ifisi jijini Mbeya ukiendelea, wananchi wanaoishi na kufanya shughuli zao kando kando ya barabara hiyo wanaendelea kukabiliwa na vumbi, foleni na changamoto nyingine za usafiri.

Sehemu ya kwanza ~ Miradi ya Barabara kutokamilika kumesababisha Athari nyingi Mbeya, kiuchumi, afya na Kijamii

Sehemu ya pili ~ Nini kinachokamisha Mradi wa Njia 4 Mbeya kukamilika? Sababu zimekuwa nyingi na zinazokinzana

Uchunguzi wa Bomba FM umebaini kuwa wakati wananchi wakisubiri kukamilika kwa mradi huo, baadhi ya hatua zimeanza kuchukuliwa na serikali ili kupunguza adha, lakini bado kuna uhitaji wa kuimarisha usimamizi wa usafiri, mazingira na usalama katika maeneo ya ujenzi.
PICHA BARABARA NJIA NNE.jpg

PICHA NJIA NNE.jpg
Wafanyabiashara wanasema vumbi linaathiri afya, bidhaa na mazingira yao ya biashara, huku baadhi yao wakisema kumwagilia maji hakufanyiki kwa kiwango kinachotosheleza.

“Hata umwagiliaji wenyewe wanamwagiwa kwa ujanja ujanja tu. Wakimwagia asubuhi, basi hawaonekani tena mpaka jioni. Tena kama hivyo unavyoona jioni wanamwagia, mchana ndo kuna vumbi. Na hii njia unajua ni njia kubwa, yanapita malori mengi sana, magari mengi, mabasi yanapita yanatimka sana.

Kiukweli adha tunazozipata sisi kama wafanyabiashara na hata majirani wa nyumba hizi ukiingia ndani unaweza ukafikiri nyumba zote ni nyekundu, lakini sio nyekundu ni rangi ya vumbi. Kwa hiyo tulikuwa tunamlilia sana serikali watusaidie, hata meya wetu naye ajaribu kupita atuangalie maisha yetu vipi, maana sisi ndo walipa kodi, sisi ndo tunalipa leseni, sasa inakuwa mtihani, eh. Tungeomba watufanyie haraka hii barabara, au hata wate— sehemu ya mjini tu.”
“Adha za vumbi ni kubwa sana; watoto mafua, hata sio watu wazima mafua, kikohozi muda wote. Huu mtaa ni wa kibiashara, kwa hiyo wafanyabiashara wako wengi sana. Kwa hiyo watu wanauza chakula, mamantilie wako hapa wanauza chakula.

Kwa hiyo unakuta mavumbi hayo, magari asubuhi foleni inakuwa kubwa, watu wanahama barabara kuu wanakuja mpaka huku, wanatibua vumbi, ndo hivyo tena yaani, adha ipo nyingi sana.”
Kutokana na malalamiko hayo, Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini, Patrick Mwalunenge, anasema wamezungumza na Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mbeya ili kuhakikisha mkandarasi anaongeza juhudi za kumwagilia maji barabarani.

“Tumekubaliana pia na na na Meneja wa TANROADS wa Mkoa wa Mbeya, kwamba kwenye kipengele cha mkataba eh cha ujenzi, mkandarasi anatakiwa awe anamwagia maji zile barabara, hasa kwenye maeneo yale ambayo watu wetu wanafanya biashara.

Maeneo ya Kabwe, maeneo ya Mwanjelwa, Soweto, maeneo ya Sae kule, eh Mbeya Pazuri, maeneo yale yote ambayo watu wetu wanafanya biashara pembezoni. Kata ya Nzovwe, Iyunga, Iwambi, eh Simike, yale maeneo yote, eh na maeneo yale ya ya Forest, basi yamwagiwe maji ili watu wetu waweze kufanya biashara zao kwa utulivu.

Kwa sababu tunajua Jiji la Mbeya ni la wafanyabiashara, na biashara zetu nyingi ziko ziko pembezoni mwa zile barabara. Wananchi wa Mbeya wanaupenda mradi, wanaufurahia, lakini vumbi limekuwa ni kero. Na mimi kama mwakilishi wao na dada yangu Tulia Ackson, daktari, tutapambana kuhakikisha kwamba pamoja na kwamba barabara inajengwa, lakini isiwe kero kwa kwa wananchi wetu.”
NJIA NNEE.jpg
Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mbeya, Mhandisi Suleiman Bishanga, anasema ujenzi wa mradi huo umefikia 44.8% na mkandarasi akiwa anaendelea na kazi kwenye mradi huo.

“Tuna barabara yetu ya TANZAM ambayo inapanuliwa kwa njia nne, na kwa sasa hivi tuko 44.8%, na serikali imetoa msisitizo tuweze kuitengeneza katika hali ambayo ni ya kimataifa, lakini kwa ajili ya ku-connect na nchi za SADC. Hii ni jitihada za kutafuta soko lakini kutengeneza tija kwa maana ya wakulima kusafirisha mizigo yao.

Baada ya miezi michache nafikiri kwa maana sasa hivi tumepokea fedha ambazo tunamrudisha mkandarasi aende sasa, tutaanza na eneo hili kuanza kuweka lami kuelekea upande wa mjini. Na tunaendelea na ujenzi wa madaraja ambayo yako sehemu ya Nzovwe...”
Hatua hii ni muhimu kwa sababu, kwa mujibu wa Dkt. Emmanuel Buberwa, daktari kutoka Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Mbeya, vumbi linaweza kuathiri mfumo wa hewa na kusababisha kikohozi, pumu, nimonia na matatizo mengine ya mfumo wa upumuaji.

Ili kutatua kero ya vumbi kwa ufanisi, TANROADS Mkoa wa Mbeya inaweza kujifunza kutoka kwenye uzoefu wa upanuzi wa barabara ya Morogoro na miundombinu ya mabasi ya haraka (BRT) jijini Dar es Salaam, ambapo wakandarasi walilazimika kisheria kuweka tabaka la lami ya muda kwenye njia zote za mchepuo.

Mbinu hii ya kihandisi iliondoa kabisa adha ya vumbi kwa wafanyabiashara na wapita njia, tofauti na utaratibu wa sasa wa mradi wa Mbeya unaotegemea kumwagilia maji yanayokauka ndani ya saa chache.

Madereva wa daladala wanasema foleni zimeongeza muda wa safari, huku mtaalamu wa uchumi akieleza kuwa hali hiyo inaongeza matumizi ya mafuta na kupoteza muda ambao ungeweza kutumika katika shughuli nyingine za kiuchumi.

Kuhusu swala hilo, serikali tayari imeanza kuchukua hatua mbalimbali, ambapo Kaimu Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mbeya, Mhandisi Justin Mrope, anasema tayari wameanza kuchukua hatua ya kutatua tatizo la foleni katika Jiji la Mbeya.

“Tulipokea maelekezo kutoka kwa waziri wetu wa ujenzi akisema kwamba ofisi za mikoani tuhakikishe tunatatua changamoto ya foleni. Sisi kama ofisi tulikaa na kujitathmini chanzo cha foleni kwenye mji wetu wa Mbeya kama mnavyojua, tukaona kwamba chanzo cha foleni ni zile sehemu ambazo wenzetu wa traffic polisi huwa wanasimamisha magari.

Kuna maeneo ambayo kwenye hii barabara ya TANZAM yalikuwa yana ajali nyingi sana. Sasa ili kuhakikisha usalama kwa watumiaji wa barabara, kuna maeneo wenzetu wa traffic polisi wakaona ni vyema magari yapite kwa zamu. Kwa hiyo wakati ule wakiyasimamisha, ndipo wakija kuyaruhusu, unakuta kama ni malori yanakuja yakiwa yako mengi, kuanzia 30, 50, yanaenda kwa wakati mmoja, yanafikia yote mjini pale.

Kwa hiyo ikitokea dharura kidogo sijui boda imepita kasimama mmoja, basi na mengine yote yanasimama, foleni inakuwa kubwa. Sasa kwa kuanzia, tukasema, okay, twende tukafanye maboresho kwenye hayo maeneo ambayo wenzetu wa traffic wanasimamisha magari kwa ajili ya kutunza usalama. Kwa hiyo tulianza na pale Inyala, tulipanua.

Kwa hiyo pale Mlimanyoka sasa hivi hakuna kusubirisha magari na hakuna foleni pale. Lakini si pale peke yake, sehemu nyingine ni hapa tulipo, Shamwengo. Kwa nini? Kwa sababu huu mlima ulioko hapa nyuma yangu mara kwa mara unakuwa na ajali nyingi sana. Na ajali ya mwisho kama wote tutakumbuka, ilisababisha magari sita yalipata ajali ajali kwa wakati mmoja hapa.

Kwa hiyo kuja kuondoa yale magari barabarani na nini kusafisha barabara ilichukua muda mrefu na foleni ilikuwa kubwa sana. Kwa hiyo tunatengeneza barabara nyingine ya mchepuko ili hiyo barabara ya lami itumike kwa ajili ya magari yanayoshuka kuelekea uelekeo wa Dar es Salaam. Kwa hiyo tunaishukuru sana serikali kwa kutuletea mradi huu, kwa sababu huu mradi una gharama kama bilioni moja na nusu. Serikali imetupatia hizo pesa kwa ajili ya kufanya mradi huu.”
Ujenzi wa barabara za mchepuo unaweza kusaidia kutenganisha sehemu za ujenzi na mtiririko wa magari, na hivyo kupunguza msongamano wakati kazi kuu ya barabara ikiendelea.

Uchunguzi pia umebaini malori ni sehemu ya changamoto ya msongamano katika baadhi ya maeneo. Ili kupunguza tatizo hilo, serikali imeanza ujenzi wa maegesho maalum ya malori katika eneo la Iyela jijini Mbeya, karibu na uwanja wa ndege wa zamani. Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Justine Kijazi, anasema maegesho hayo yanalenga kuondoa malori yanayoegeshwa kiholela kando kando ya barabara kuu.

“Hapa sasa malori yaweze kupaki kwa ajili ya kazi kubwa ambayo tunaitegemea. Ndani ya wiki moja hii tutakuwa tumemaliza ku-clear na sasa tutakuwa tunapanga malori vizuri ili yaweze kuja kupaki huku.”
Hatua nyingine inayoweza kuongeza matumaini ya kukamilika kwa mradi huo ni upatikanaji wa fedha. Katika ziara yake jijini Mbeya Agosti 8, 2026, Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, alisema serikali imeanza kutoa fedha kupitia Mfuko wa Barabara kwa ajili ya kukamilisha miradi ya barabara iliyopewa kipaumbele zaidi, ikiwemo ujenzi wa barabara ya njia nne jijini Mbeya.

“Kwenye barabara yetu hii naambiwa tayari imeshapata fedha, kile kiwango chote ambacho mkandarasi alikuwa anadai hiki cha nyuma. Shilingi bilioni tisa alizokuwa anadai zote zimeshatolewa, sasa mkandarasi akaanze akaendelee kufanya kazi.

Tutaendelea kufuatilia takriban kila atakapokuwa anatoa zile ankara zake za madai ziweze kulipwa kwa wakati, barabara hii sasa hivi isisite, iendelee kujengwa, ikamilike. Kwa upande wetu Wizara ya Fedha, tumekutana na Wizara ya Ujenzi, tumewaambia wazipange barabara zote kwa vipau mbele kwenye kupata fedha hizi kutoka na mfuko.

Tumekubaliana namna ya kupata fedha nyingine kama kitangulizi wakati hizi nyingine zinaendelea kukusanywa kidogo kidogo, ili miundombinu ya barabara zote tulizonazo, zile ambazo zipo katika mpango wa maendeleo kama hii barabara ya Mbeya ya njia nne, ziweze kutekelezwa kwa haraka na tuondokane na kadhia hii ya usumbufu wa barabara yenyewe kwa mashimo, lakini na vumbi.”
Kwa wananchi wa Jiji la Mbeya, kukamilika kwa barabara hii ndiko ambako kunasubiriwa zaidi.



ANDIKO LA: Heneliko Malo
Makala imeandaliwa na Mwandishi anayeshiriki katika programu maalum ya kukuza uandishi wa maslahi kwa umma (Public Interest Journalism Fellowship) inayoratibiwa na UTPC kwa kushirikiana na IMS
 

Attachments

Jiji la Vumbi ~ Mbeya 🙌


Watu wanalalamika kukawia kukamilika kwahiyo barabara, tangu mwaka 2022 ni mashimo tu pamoja na Vumbi kutimka
 
Duh!
Mradi umechukua muda!
Sasa kutokana na ajali za mara kwa mara, nawashauri Tanroads, pale Iwambi mpaka Mbalizi, bara bara ya kati kati wanyanyue tuta urefu wa mita moja ili magari madogo ya kwenda na kurudi yapite juu ya tuta na malori ya kwenda na kurudi bara bara yake itakuwa ya chini.
Hii itaepusha maroli kuyagonga magari madogo pindi yanapofeli breki au yanapofeli kupanda mlima.
20261026_104448.jpg
 
Back
Top Bottom