Wabunge wa Tanzania wajue sio kila jambo linalohusu usalama wa nchi ni la kutolewa ufafanuzi kwa wanasiasa

Kuwashughulikia watu kwa sababu za usalama wa taifa ni jambo zuri, lakini kuwashughulikia kwa maslahi ya kisiasa si jambo zuri kabisa.
 
Wale jamaa wanafanya kazi nzito sana sema ndiyo hivyo watafute mbinu ya kupunguza tension mtaani huku habari za kuokota maiti kila muda nayo sio nzuri hata kama wanafanya kwa maslahi ya taifa
 
Nakuunga mkono mkuu.
Ambaye hajielewi na hajakuelewa, ana matatizo.
Watu wanauchukulia usalama wa nchi for granted.
 
Marekani na washariki wake kushambulia Libya na kuumua Gadafi, unahisi walikuwa wanalinda MASLAHI ya Wamarekani au walibya? Ukinijibu tutaendelea zaidi
 
Mota mada ni mtetea tumbo tu...subiri CCM in;gatuke muone kama atarudi kutetea hivi.
 
Kwa sheria za Tanzania ni mahakama peke yake ndiyo inayoweza kuamua ikiwa mtuhumiwa ana hatia au vinginevyo!!

Sasa hao Wanausalama unaowasema wewe wamepata wapi mamlaka ya kuamua ikiwa watuhumiwa walikuwa na hatia au hapana?!!

Na hata kama walijiridhisha kwamba walikuwa na hatia, tangu lini nchi hii polisi wamekuwa ndio watoa hukumu?!

Hivi unaweza kunitajia sababu za msingi za kwanini watuhumiwa hawakutiwa nguvuni na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria?!

Unataka kuniambia hilo kundi lilikuwa hatari sana kiasi kwamba isingewezekana kuwatia nguvuni hata kama tungepeleka askari wangapi na hivyo possible and safest order ilikuwa ni shoot at first sight?

Kama order haikuwa shoot at first sight, watuhumiwa wamepelekwa kwenye mahabusu zipi?!

Btw, ikiwa ni zaidi ya miezi 6 sasa imepita na bado hao hao wanausalama unaosema hawajaweza kubaini ni nani hasa walihusika kumshambulia Tundu Lissu! Kuna matukio mangapi ya uhalifu yamefanyika nchi hii na hadi leo wahusika hawafahamika?!

Sasa leo wameupata wapi uwezo wa ghafla namna hiyo wa kuweza kuwabaini waliokuwa wanafanya uhalifu huko MKIRU na hivyo kuamua kutoa hukumu isiyofahamika na yeyote?!

Kamanda Sirro ametoa wapi uwezo wa ghafla namna hii wa kuweza kubaini waliofanya mauaji MKIRU TU na sio wahalifu wengine?!

Kuhusu hili hakuna justification yoyote ya kuhalalisha!

Mtu hana haja ya kuwa na weledi wa masuala ya kiusalama kufahamu kwamba Polisi walikuwa wanatoa hukumu just kwa mtu kutajwa! Kwamba, X anakamatwa, anakuwa torchured na kulazimishwa ataje "wenzake" na akitaja, polisi wanafuata watuhumiwa and the game goes on!!

Na kwa jinsi ilivyo, inawezekana kabisa wapo ambao ili kuepuka mateso ya polisi, basi wakataja tu majina au kukubali kuhusika huku wakidhani kwamba huenda wangefikishwa mahakamani bila kufahamu hukumu ingetoka hapo hapo!!

Ni mara ngapi hata kwa kwa makosa ya kawaida watuhumiwa wamekuwa wakikubali "kosa" mbele ya polisi lakini kwenda kukata mahakamani kwa sababu tu walikubali ili kukwepa mateso!

There's no naweza ku-justify haya! Kwa mfano, Zitto Kabwe kataja wanawake waliokuwa wamekamatwa na hadi sasa hawafahamiki waliko!! Hivi kabisa unaweza kuamini kwamba hao akina mama walikuwa ni hatari kweli kweli?! Lakini hata kama walikuwa hatari kweli kweli; si tayari walishawakamata?! According to Zitto, miezi 10 imepita sasa... wako wapi hao akina mama?!

Katika mazingira kama hayo ni kwanini basi watu wasiamini kwamba zile maiti zilizokuwa zinaokotwa zikiwa kwenye viroba ni za hao watuhumiwa?!

Mungu nisaidie nisije kujaribu hata kuwaza kutetea uovu kama huo kwa sababu zozote zile!!!
 
Marekani na washariki wake kushambulia Libya na kuumua Gadafi, unahisi walikuwa wanalinda MASLAHI ya Wamarekani au walibya? Ukinijibu tutaendelea zaidi
Kwanini nijibu hoja isiyohusiana na nilichoandika?!
 
Huwa najiulizaga nini kilitaka kutokea MKIRU? Sijapataga majibu! Ni kikundi cha kigaidi kilitaka kuchomozea Kibiti? Au kikundi cha uamsho kilikuwa na base yake huko? Ilikuwakuwaje hili jambo likamea namna ile hadi ikawa mauaji ya kutisha? Tena askari wetu wakawa wanauawa? Kukua kwake ilikuwa ni weakness ya vyombo vyetu vya usalama au ni politically motivated? Wanasiasa wakubwa kufaidika na mauaji yale kama ilivokuwa kwa Joseph Konyi, kila wakati Mseveni akawa anasingizia bado anahitajika madarakani ili kutokomeza akina Konyi! Miaka na miaka vita ikadumu kaskazini mwa Uganda huku Mseveni akiwa relaxed! Napenda kujua nini kilitaka kutokea MKIRU na tulifikaje stage ile kama nchi? Nchi yenye vyombo vya usalama kuanzia TISS, Polisi hadi JW?
 
Kisa siasa za ukada!!
Siasa za ukada na ukanda! Hatari sana.....tuendako maridhiano ya kitaifa yatahijika sana ili kurudisha mshikamano na udugu kama Taifa. Kwa sasa taifa limeparaganyika na bahati mbaya anayetakiwa kuunganisha taifa kisaikolojia yeye ni shabiki namba moja wa ukada na ukanda badala yake anaamini mshikamano utakaosimamiwa kwa mkono wa chuma na jeshi pamoja na vyombo vingine vya usalama. So sad.
 
Wewe umejuaje hayo wakati kiwango cha uelewa wako kama mtanzania ni mdogo? Au wewe siyo mtanzania? Ujinga mwingine ni mzigo!
 
..kama kuna suala NYETI/SIRI/CLASSIFIED basi suala hilo halitajadiliwa in public bali ktk vikao vya faragha baina ya wabunge na wakuu wa vyombo vya usalama.
 
Unajua sababu kwa nini gereza la guantanamo bay lilianzishwa nje ya nchi ya marekani?
 
Infantry soldier ,Una utashi kama wangu,you surpassed tactical points.
Anaelewa atakuwa ameelewa ,naomba uwe unanitagi pia kwenye hizi maada.
Mengine tubishane tu ila kwenye usalama wa Tz Yangu nipo rigid ,
Naipenda Nchi Yangu.
Sheria ya ugaidi,sheria ya uhaini zilitungwa za nini? Katiba kusema kila mtu hana hatia mpaka itakapothibitishwa na mahakama ilikosewa?
Watawala walio ua watu bila kufuata matakwa ya sheria mwisho wa siku waliitwaje? Na walifanywaje kwenye nchi zao.
Katika hili mmefuata njia ya kuzimu, hakuna mwanasiasa alieua watu kwa mikono yake mwenyewe lakini jiulizeni kwa nini walihukumiwa wao?
 
Mkuu, hawa waliosumbuwa watu kule Kibiti wapo mpaka kule Msumbiji, ni network ya watu wenye msimamo mkali.

Jinsi gani wanavyokamatwa na kushughulikiwa, sio jambo ambalo waziri au IGP anaweza kujitokeza hadharani na kuelezea, ndio maana mojawapo ya classified information.

CIA au FBI hawawezi hata siku moja kuwaonyesha wamarekani namna wanavyopambana na uharamia wa chini kwa chini, utakuja kugundua miaka kadhaa baadae kupitia video clips za Youtube.

Kwa hiyo usidhani kwamba uwazi na demokrasia ni mambo ambayo yapo kwenye kila nyanja ya maisha, wakati mwingine usiri kwenye mapambano mazito ya kiharamia ni muhimu sana ukawepo kwa faida yako na ya kwangu.
 

Kabla ya kuingia kwa kina kwenye uchambuzi huu, ni muhimu kueleza bayana kwamba japo maana, mbinu na ufanisi wa uchambuzi wa kiintelijensia ('intelligence analysis' kwa kimombo) kati ya mie niliyepo hapa Glasgow na afisa mchambuzi wa intelijensia aliyepo Dar zaweza kuwa karibu na sawa, mazingira kati yangu na ya afisa huyo ni tofauti. Tofauti sio kwa vile mie nipo Uingereza na afisa husika yupo Tanzania bali vitu kama shinikizo la kupata majibu upesi na nyenzo mbalimbali kama vile watoa habari, mafaili, nk.

Pili, nitajitahidi kadri nitakavyoweza kuepuka 'mtazamo wangu' na badala yake niongozwe na kanuni za uchambuzi wa kiintelijensia. Hata hivyo, ni muhimu kufahamu kuwa moja ya nyenzo muhimu kwenye intelijensia ni mwanadamu, iwe kwenye kukusanya taarifa za kiintelijensia, kuchambua au kushauri. Kwahiyo, japo nitajitahidi kuepuka 'mtazamo wangu,' siwezi kuepuka ubinadamu wangu kama mchambuzi wa kiintelijensia wa somo husika.


Kwa kifupi, tuanze na tunachofahamu hadi muda huu. Kwa mujibu wa taarifa zilizopo mauaji yanayojumuisha eneo la Mkuranga, Kibiti na Rufiji (MKIRU) yalianza Januari 2015 na hadi sasa yamegharimu uhai wa watu 40 wakiwemo askari polisi 13.


Tukisema tuorodheshe mlolongo wa kauli za viongozi mbalimbali, wa serikali na wa jeshi la polisi, basi huenda itabidi kukesha hapa, au kuandika kitabu kizima. Hata hivyo, kwa kifupi, miongoni mwa kauli hizo ni kama ifuatavyo

Rais John Magufuli:

Kwa ujumla, Rais Magufuli ametoa matamko makubwa matatu kuhusu mauaji yanayoendelea katika eneo la MKIRU. Tamko la kwanza ni salamu za rambirambi alizotoa kufuatia mauaji ya askari polisi wanane, ambapo alilaani mauaji hayo. Hiyo ilikuwa April 14 mwaka huu.


Tamko la pili la Rais lilikuwa majuzi alipofanya ziara mkoani Pwani ambapo Juni 20 aliwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa serikali na vyombo vya dola ili kukomesha mauaji hayo. Rais alieleza kuwa watu wanaofanya vitendo hivyo vya mauaji "tunakaa nao, tunawaficha, ni watoto wetu." Kadhalika, Rais Magufuli alieleza kuwa "serikali ya Awamu ya Tano sio ya kuchezewa" na kudai kuwa "(wauaji hao) wameshaanza kunyooka."


Hata hivyo, siku moja baada ya Rais kutoa kauli hiyo ya kutia matumaini, askari polisi wawili waliuawa na gari lao kuchomwa moto, pengine ikiwa ni jibu la wauaji hao kwa Rais aliyedai kuwa "wameshaanza kunyooka."


Tamko la tatu la Rais, na pengine kali kuliko hayo mawili, lilitolewa jana jijini Dar wakati wa uzinduzi wa upanuzi wa Bandari ya Dar, ambapo katika kilichoonekana bayana kuwa majibu kwa rai ya Waziri Mkuu Mstaafu Edward Lowassa kwa Rais Magufuli kumtaka atafakari kuhusu 'mashehe wa Uamsho' wanaosota gerezani kwa miaka minne sasa bila kesi yao kuamuliwa.


Katika tamko hilo Rais aliwaomba wanasiasa wanaosema kuwa hawa (mashehe wa Uamsho) wameshikiliwa kwa muda mrefu "wajizuwie midomo yao," na kudai kuwa "hata kuna watu kule Marekani walikaa Guantanamo muda mrefu," na kudai kuwa (wanaoongea kama Lowassa kuwa kesi yao ishughulikiwe) inaweza kuwafanya watu kuhisi (anayesema hivyo) ni "mmoja wao."


Rais Magufuli alihoji "kwanini hata siku moja mtu asijitokeze kualaani wanaouawa bila hatia kule (MKIRU), lakini kwa kutafuta sifa za kisiasa, mtu anatoka anasema watu wako ndani muda mrefu." Rais aliwataka polisi kufanya kazi yao, na kuwaagiza kuwakamata "hao wanaoropoka waisaidie polisi," na "msiogopee sura, awe na mwendo wa haraka, polepole au kukimbia, mkamateni kusudi akaisaidie polisi kule ndani."


Rais alidai pia mtu aliyekamatwa na sare 500 za jeshi zilizokamatwa hivi karibuni "inaonekana anahusiana na walioko ndani (mashehe wa Uamsho)."


Waziri wa Mambo ya Ndani Mwigulu Nchemba na Naibu Waziri wake Yusuph Masauni


Kwa nyakati mbalimbali, viongozi hawa wawili wametoa kauli kadhaa kuhusiana na mauaji yanayoendelea huko MKURU. Kuorodhesha kauli zote kwahitaji makala nyingine pekee, lakini kwa kifupi, Waziri Mwigulu ameshanukuliwa akidai kuwa "mauaji hayo yana harufu ya kisiasa," na kuhoji "Ujambazi gani huo wa Wana CCM tu? Hako kamchezo tumeshakagundua. Dhahiri, huo ni ushamba wa vyama vingi.”


Waziri Mwigulu alikwenda mbali zaidi na kudai kuwa chanzo cha mauaji hayo ni chuki za vyama vya upinzani dhidi ya CCM.


Awali Waziri Mwigulu alieleza Bungeni kuwa serikali imeshabaini kuwa wanaohusika na mauaji hayo wanatoka maeneo ya Mkuranga, Kibiti na Rufiji, na kwamba changamoto ya mauaji hayo ipo mbioni kutatuliwa.


Kwa upande wake, Naibu Waziri Masauni amenukuliwa akieleza kuwa serikali inalipa kipaumbele suala hilo na lazima mauaji hayo yadhibitiwe. "Tuweze kuharakisha zoezi hili ambalo kwa hakika kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu kwa sisi tunaosimamia haki na uhai wa raia wasio kuwa na hatia hii vita lazima tushinde inshaallah,” alinukuliwa Masauni hivi karibuni.


IGP Sirro na mtangulizi wake IGP Mangu:


Wakati IGP Simon Sirro ameanza jukumu hilo la ukuu wa jeshi la polisi wakati jeshi hilo likikabiliwa na changamoto za mauaji ya MKURU, mtangulizi wake IGP Mangu huenda akakumbukwa zaidi kwa onyo lake la kuwasaka "watu waliofurahia mauaji ya askari wanane," kauli ambayo ilionekana kama 'kusaka adui wa kufikirika.' Hata hivyo, suala hilo aliloongelea IGP Mangu lilipaswa kuibua tafakuri pana na endelevu kuhusu uhusiano mbovu kati ya jeshi la polisi na wananchi.


Kadhalika IGP Mangu alieleza kuwa jeshi lake lingeanza kutumia nguvu ilizonazo kulazimisha upatikanaji wa taarifa kuhusu mauaji hayo.


Kwa upande wa IGP Sirro, masaa machache tu baada ya kukutana na wazee wa Kibiti na Rufiji kujadiliana nao kuhusu mauaji hayo, mkazi mwingine aliuawa na watu wasiojulikana. Awali, IGP Sirro aliwaeleza waandishi wa habari kuwa "wauaji hao hawatachukuwa muda mrefu kukamatwa" na kwamba "siku zao zinahesabika." Kadhalika, mkuu huyo mpya wa jeshi la polisi alidai kuwa maongezi yake na wazee wa Kibiti na Rufiji yatafanikisha kukamatwa kwa wauaji hao.


Baada ya kuteuliwa wadhifa huo, IGP Sirro alitangaza dau la shilingi milioni 10 kwa yeyote atakayetoa taarifa zitakazowezesha kukamatwa kwa wahusika wa mauaji hayo.


Juni 25 mwaka huu, IGP Sirro alinukuliwa na vyombo vya habari akieleza kuwa jeshi lake halifahamu wahusika wa mauaji hayo, kauli iliyokinzana na ya bosi wake, Waziri Mwigulu kwamba chanzo cha mauaji hayo ni chuki ya vyama vya upinzani kwa CCM.

Julai 5 mwaka huu, IGP Sirro alieleza kuwa mauaji hayo ya MKIRO 'yana mkono kutoka nje ya nchi' bila kufafanua nchi gani inayohusika. Kadhalika, taarifa hiyo iliyaeleza mauaji hayo kama yaliyokuwa yakiendelea kwa takriban miaka mwili sasa.


Edward Lowassa:


Rai ya Lowassa kwa Rais Magufuli kuhusu hatma ya 'mashehe wa Uamsho' nimeitaja hapo juu, lakini kwa urefu, habari hiyo ipo HAPA.


Zitto Kabwe


Kufuatia kilichotafsiriwa kama majibu ya Rais Magufuli kwa Lowassa, kiongozi mkuu wa chama cha upinzani cha ACT- Wazalendo Zitto Kabwe alitoa maoni yake katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Facebook.


Uchambuzi wa kiintelijensia

Hadi muda huu, hakuna kikundi kilichojitokeza hadharani kudai kuhusika na mauji hayo. Hata hivyo, bila hata kuhitaji uzoefu wa kishushushu, sio vigumu kuhisi kuwa


1. Mauaji hayo yanafanywa na kikundi maalum
2. Wahusika ni watu wenye uelewa/uzoefu wa mbinu za mauaji


Hata hivyo, licha ya kutojitokeza kikundi chochote kudai kuhusika na mauaji hayo, taarifa zilizopatikana siku chache zilizopita zilieleza kwamba kuna ujumbe uliotumwa na 'wahusika wa mauaji hayo,' unaosomeka kama ifuatavyo

Tunawatangazia wananchi tumewaua hawa kwa sababu wanadhulumu watu kwa kutumia kazi zao na yeyote atakayefanya kazi hapa au nje ya hapa tutamtafuta hadi nyumbani kwake.

Sisi tumejitolea kufa kuliko kuishi, kwa hiyo dereva au raia popote uwaonapo toa taarifa iwe nyumbani au kazini.

Hakuna njia ya kumaliza dhuluma isipokuwa chuma tu, hapa chuma tuuu!
Kwa mujibu wa taarifa, ujumbe huo uliandikwa kwa kalamu na kisha kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii.


Turudi nyuma kidogo hadi mwaka 2013 ambapo kulitokea uhasama mkubwa kati ya Polisi na baadhi ya wakazi wa Kibiti kufuatia kifo cha mkazi mmoja wa eneo hilo, Athuman Hamis aliyefariki kutokana na majeraha aliyoyapata kutokana na kipigo cha polisi (kwa mujibu wa maelezo ya wakazi hao).

Habari kamili ipo HAPA


Katika kufanya uchambuzi wa kiintelijensia wa suala kama hilo la mauaji hayo ya MKIRU, yahitajika vitu viwili. Kwanza, kuwa na maelezo sahihi kuhusu tatizo husika, na pili, matokeo tarajiwa zaidi ni yapi.

Katika uchambuzi wa mauaji hayo ya MKIRU, ninatumia moja ya njia za uchambuzi wa kiintelijensia, inayojulikana kama ACH - Analysis of Competing Hypotheses - yaani Uchambuzi wa Dhana Zinazoshindana.

Hatua ya kwanza ni kutambua dhana husika. Ili kupata dhana hizo, niliendesha kura ya maoni isiyo ya kisayansi kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter. Vipengele vinne vilivuounda swali husika vilitokana na maelezo mbalimbali yaliyokwishatolewa kuhusu zinazoweza kuwa sababu za mauaji huko MKIRU

Kama inavyoonekana katika 'tweet' hiyo yenye matokeo ya kura ya maoni, dhana kuu nne ni
  1. Ugaidi
  2. Chuki za kisiasa
  3. Chuki za wananchi dhidi ya Jeshi la Polisi
  4. Uhalifu kama mwingine
Kuorodhesha dhana hizo (kama ilivyo hapo juu) na kuzipitia kwa kina zaidi na kujumuisha 'ushahidi uliopo' kwa kila moja (kama inavyofuata hapa chini) ni hatua ya pili ya ACH.

Tuanze na dhana kuwa mauaji hayo yanatokana na chuki za wananchi. 'Ushahidi' kuhusu dhana hii ni wa aina mbili. Kwanza, Januari 23, 2013, kulijitokeza vurugu kubwa huko Kibiti zilizolazimu jeshi la polisi kutumia helikopta kuzidhibiti. Vurugu hizo zilitokana na kifo cha mkazi mmoja wa Kibiti aliyefariki Hospitali ya Taifa Muhimbili alikopelekwa kutibiwa majeraha ambayo ilidaiwa aliyapata kutokana na kupigwa na polisi.

Vurugu hizo zilipelekea Barabara ya Kilwa kufungwa kwa zaidi ya amsaa matatu, na hivyo kuathiri usafiri kwenda mikoa ya Mtwara na Lindi; sambamba na wananchi kuvamia kituo kimoja cha polisi na kuchoma moto nyumba moja ya polisi.



'Ushahidi' wa pili wa dhana kuwa chanzo cha mauaji ya MKIRU ni chuki za wananchi dhidi ya jeshi la Polisi ni ripoti maalum ya kiuchunguzi ya Gazeti la Mwananchi iliyochapishwa Mei 26 mwaka huu.

Kwa kifupi, ripoti hiyo inaeleza kwamba wengi wa wakazi wa MKIRU ni masikini wenye elimu duni, na tegemeo lao kubwa la kipato ni kuvuna raslimali nyingi zilizopo eneo hilo na kuzuza. Biashara kubwa ambayo vijana wanajihusisha nayo ni uchomaji na uuzaji wa mkaa, uvunaji magogo kwa ajili ya mbao, uuzaji wa kuni na mazao mengine ya mashambani kama vile mpunga na mihogo, imeajiri vijana wengi katika maeneo hayo.

Hata hivyo, kwa mujibu wa ripoti hiyo, kumekuwa na unyanyasaji mkubwa unaofnywa na mamlaka za mitaa, maofisa wa Idara ya Maliasili, jeshi la mgambo na polisi.

Licha ya mamlaka husika kuweka lundo la vizuizi, pia wananchi hao walilalamikia 'kodi za kukomoana.' Kwa miaka mingi sasa, wananchi wamekuwa wakilalamikia vizuizi hiyo kuwa kitovu cha dhuluma na uonevu mkubwa wanaofanyiwa wananchi na wasimamizi wa vizuizi ambao wamekuwa wakikadiria kodi za kukomoa, kutaifisha magunia ya mkaa na mbao na mali nyingine za wananchi.


Wananchi hao wanadai kuwa uonevu na dhuluma vimechokoza hasira za vijana wengi, ambao "kazi zao ndio mkaa, kuni na mbao au mihogo." Kuhusu matumizi ya silaha, ilielezwa kuwa vijana wengi katika maeoeneo hayo wana mafunzo ya mgambo na JKT huku wakiwa hawana ajira nyingine zaidi ya kutegemea biashara hizo.




“Si suala la kidini. Ni manyanyaso tu. Leo unadhulumu watano, kesho kumi, hawa wakiji-organise unatarajia nini?” aliuliza mkazi mmoja wa eneo hilo, na kuongeza kuwa ingawa dhehebu moja la kidini lina vijana wengi lakini halina uhusiano na mauaji.
Kuhusu dhana nyingine kwamba mauaji ya MKIRU yantokana na ugaidi, kuna 'ushahidi' wa matukio mbalimbali kwa takriban miaka mitano sasa ambayo japo serikali imekuwa ikiyaita kuwa ni ujambazi, yana viashiria vya ugaidi.
Moja ya vitu vinavyoleta ugumu katika kutanabaisha ugaidi au lani kasumba iliyoshamiri kitambo ambapo baadhi ya wanasiasa wamekuwa wepesi kuwatuhumu wapinzani wao wa kisiasa kuwa wanapanga au wanajihusisha na vitendo vya kigaidi kwa minajili tu ya uhasama wa kisiasa.
Baadhi ya wanasiasa wa chama tawala CCM, kwa nyakati tofauti wamewahi kuvituhumu vyama vya upinzani vya CUF na Chadema, na baadhi ya viongozi na wanachama wake, kuwa wahusika wa ugaidi, tuhuma ambazo mara zote hazikuweza kuthibitishwa.
Japo magaidi hupendelea wafahamike kuwa ndio wahusika wa tukio la kigaidi, kunapojitokeza watu wasio na hatia kutuhumiwa kuwa ndio magaidi, hiyo inaweza kurahisisha kazi ya magaidi halisi.
Katika mlolongo wa matukio mbalimbali yenye viashiria vya ugaidi, Julai 2 mwaka huu, Rais Magufuli aligusia kuhusu 'mashehe wa UAMSHO' ambao wapo gerezani kwa zaidi ya miaka minne sasa wakisubiri hatma ya mashtaka ya ugaidi yanayowakabili. Katika hotuba yake jijini Dar, Rais Magufuli aliashiria kuwa kuna uhusiano katika ya mauaji ya MKIRU na mashehe hao wa UAMSHO, huku akiibua taarifa mpya kuwa hata sare 500 za jeshi zilizokamatwa jijini Dar zilikuwa na uhusiano na mashehe hao/ 'ugaidi' huko MKIRU.


Kadhalika, Julai 5 mwaka huu, IGP Sirro alinukuliwa na vyombo vya habari akieleza kuwa mauaji ya MKIRU yana 'mkono wa nchi za nje.' Kingine cha muhimu katika maelezo ya IGP Sirro ni kubainisha kuwa mauaji ya MKIRU yamekuwa yakiendelea kwa zaidi ya miaka miwili.

Tukio jingine ni pamoja na lile la Mei mwaka jana huko Mwanza ambapo kulitokea mapambano makali kati ya askari wa jeshi la polisi wakisaidiwa na wenzao wa Jeshi la Wananchi dhidi ya kilichoelezwa na serikali kuwa ni genge la majambazi. Mapambano hayo yalielezwa kuwa na uhusiano na uvamizi kwenye msikiti wa Rahman jijini humo, ambapo kulitokea mauaji ya kutisha baada ya watu wasiofahamika kuvamia msikiti huo na kuwauwa kwa kuwachinja Imamu aliyekuwa akiswalisha swala ya Isha, Ferouz Elias (27) na waumini wawili, Mbwana Rajab na Khamis Mponda.

Tukio jingine lilitokea Novemba 22 mwaka jana ambapo Jeshi la Polisi lilikamatwa wanawake wanne na watoto wannewaliodaiwa kuwa katika mafunzo ya kigaidi, huko Vikindu, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam




Tukio jingine ni lile la Machi 2 mwaka juzi ambalo lililozua taharuki miongoni mwa Watanzania wengi kufuatia kuibuka kwa video yenye ujumbe ulioashiria uwepo wa kundi linalopambana na jeshi la polisi kwa sababu za kidini


Kadhalika, Juni mwaka 2015, taasisi ya ACLED ilitoa taarifa iliyoonyesha kulikuwa na ongezeko la matukio yenye viashiria vya ugaidi. Ripoti hiyo iliyoambatana na majedwali yanayoonyeshwa mwenendo wa matukio hayo ilitokana na taarifa mbalimbali katika vyombo vya habari vya Tanzania.


Taarifa hiyo ambayo unaweza kuisoma HAPA ilibainisha kwamba Tanzania ina vikundi vidogo vya kigaidi vyenye uhusiano na kundi la Al-Shabaab la Somalia au Al-Hijra la Kenya. Vikundi hivyo ni pamoja na Ansar Muslim Youth Centre cha mjini Tanga.

Pia, Novemba mwaka 2013, Jeshi la Polisi lilifanikiwa kuwakamata watu 69 waliokuwa kwenye kilichoelezwa kuwa ni mafunzo ya kigaidi kuhusu kundi la Al-Shabaab.

Vilevile, takriban mwezi mmoja kabla ya tukio hilo, watu wengine 11 walikamatwa na Polisi mjini Mtwara wakituhumiwa kujihusisha na kundi la Al-Shabaab.

Kadhalika, mwezi huohuo, mfanyabishara Juma Abdallah Heri alikamatwa na polisi kwa tuhuma za kufadhili vikundi vya kigaidi nchini Tanzania.

Mwendelezo wa matukio hayo ni pamoja na lile la April mwaka jana ambapo zilipatikana taarifa kuwa Mtanzania Issa James Mwesiga aliuawa na kundi la Al-Shabaab nchini Somalia kwa tuhuma za ujasusi. Inaelezwa kuwa Mtanzania huyo alijiunga na kundi hilo la kigaidi mwaka 2013.



Agosti 2015, Watanzania sita walikamatwa huko Garissa, nchini Kenya wakiwa njiani kuelekea Somalia kujiunga na kundi la Al-Shabaab. Walikutwa na mabomu saba na bastola saba.



Awali, Machi mwaka huohuo, mwanamke mmoja, Ummur Kayr Sadir, alikamatwa na wenzie wawili wakiwa safarini kwenda Somalia kujiunga na kundi hilo la kigaidi.


Septemba mwaka jana, taasisi ya Intergovernmental Authority on Development (IGAD) ilitoa ripoti iliyoeleza kuwa kundi la Al-Shabaab lilikuwa ikifanya jitihada kubwa kupata wafuasi wa kiume na kike wa kujiunga na kundi hilo, hata nje ya Somalia (lilipo kundi hilo) na Tanzania, Uganda, Ethiopia na Djibouti zilikuwa zilikilengwa katika jithada hizo.

Februari 28 mwaka jana, watu watatu waliuawa na polisi jijini Arusha, huku taarifa zikieleza kuwa watu hao walikuwa wanakikundi wa Al-Shabaab.

Juni mwaka jana, watu wanane waliuawa kinyama huko Tanga, ikiwa ni wiki mbili tu baada ya tukio jingine la kinyama jijini Mwanza ambapo Imamu wa msikiti wa Rahman na waumini wawili walichinjwa.

Oktoba mwaka jana, polisi walimkamata mwalimu mmoja wa madrasa huko Bagamoyo kufuatia taarifa za wananchi kwa polisi. Mwalimu huyo alikamatwa akiwa na watoto 22 ambapo polisi pia walikuta maandiko mbalimbali ya kuhusu ugaidi na walikuta bomu la gesi nyumbani kwa mwalimu huyo.

Mei mwaka jana, kikundi kilichojitambulisha kama Ahl Kalf Mujahidina kilitoa wito kwa Waislam kuwa wajiunge nacho, ambapo kilieleza kuwa kimeweka makazi yake kwenye mapango ya Amboni huko Tanga.
FireShot Capture 17 - Uwito Kutoka Kwa Ahl Kahf Mujahidina W_ - Https___alharakatul.wordpress.com by Evarist Chahali on Scribd


April mwaka jana zilipatikana taarifa za kuundwa kwa kundi jipya la kigaidi linalofahamika kama Jahba East Africa ambalo lilijitangaza kuwa wafuasi wa kundi hatari la kigaidi la ISIS. Kadhalika kundi hilo lilidai kuwa miongoni mwa wafuasi wa filisofia yake wapo nchini Tanzania.



Kwahiyo hadi hapa, tumeshaona dhana mbili na 'ushahidi' wake, na sasa tumalizie na dhana mbili zilizosalia. Dhana nyingine ni kwamba mauaji hayo ya MKIRU yanayokana na chuki za kisiasa. 'Ushahidi' pakee katika dhana hii ni kauli ya Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba, kwamba mauaji hayo 'yananuka siasa.'


Na dhana ya nne na ya mwisho ni kwamba mauaji hayo ni matukio ya uhalifu kama matukio mengine. 'Ushahidi' kuhusu dhana hiyo ni ukweli kwamba takwimu za uhalifu nchini Tanzania kwa mwaka 2013 na 2014 na 2015 zinaonyesha mauaji kama kosa kubwa la pili kwa ukubwa (wingi) nyuma ya ubakaji katika kundi la makosa dhidi ya binadamu.

Hatua ya tatu ya ACH inahusisha kuandaa 'matrix' yenye dhana husika, kwa minajili ya kupima 'consistency' au inconsistency.' Pia kuna fursa ya kupima kuaminika na kulandana kwa kila dhana.

Mkiru Killings Analysis of Competing Hypotheses by Evarist Chahali on Scribd


Hatua ya nne ya ACH inahusisha kuangalia 'diagnosticity' - uwezekano wa dhana kuwa sahihi. Kadhalika katika hatua hii, dhana yenye/zenye mapungufu - kwa maana ya kwamba hazijitshelezi kueleza somo linalochunguzwa - yaweza/zaweza kuondolewa. Na katika somo hili la mauaji ya MKIRU, nimefikia hitimisho la kuondoa dhana mbili za 'mwisho' (nitaeleza maana ya 'mwisho' mbeleni) yaani "chuki za kisiasa" na "mauaji hayo ni uhalifu kama mwingine." Kwahiyo ninabakiwa na dhana mbili, yaani "ugaidi" na "hasira za wananchi."

Hatua ya tano ya ACH inatokana na hatua ya nne na imenipelekea kuwa na matrix yenye dhana mbili, ya ugaidi na hasira za wananchi.

Mkiru Matrix Drawn Down by Evarist Chahali on Scribd


Hatu ya saba ya ACH ni kuripoti matokeo ya uchambuzi. Najua hayo majedwali ya matrix yanaweza kumchanganya msomaji lakini nyenzo muhimu kufikia hitimisho la karibu zaidi na ukweli. Ikumbukwe kuwa intelijensia sio sayansi timilifu kwa asilimia 100 - kwa kimombo wanasema "intelligence is not exact science." Kwahiyo, dhana, ushahidi wake, na msaada mkubwa wa ACH unanipeleka kufikia hitimisho lifuatalo.

1. Kumekuwa na harakati za muda mrefu za kusambaza na hatimaye kuimarisha ugaidi nchini Tanzania. Katika uchambuzi huu, ushahidi uliotumika umeanzia mwaka 2013, miaka minne iliyopita. Hata hivyo, jitihada hizo za kusambaza/kuimarisha ugaidi zimekuwa kama za kulipuka na kufifia (sporadic), japo kama tukiamini kuwa mauaji ya MKURU ni sehemu ya harakati hizo, basi hitimisho linakuwa kwamba harakati hizo zimefanikiwa kujikita.

2. Chuki ya wakazi wa maeneo husika zinasaidia kufanikisha harakati hizo za magaidi hao. Katika matrix ya pili iliyobakiwa na dhana mbili badala ya nne za awali, kuna 'consistency' katika 'uhusiano' wa dhana ya ugaidi na chuki ya wananchi. Pengine hili limechangiwa na mamlaka husika kutofanyia kazi vilio vya wakazi wa eneo hilo (rejea taarifa ya kiuchunguzi ya Gazeti la Mwananchi kuhusu maujai ya MKIRU).

3. Kauli ya IGP kuwa mauaji hayo yana mkono wa kutoka nje inapewa uzito na matukio mbalimbali yaliyotumika katika uchambuzi huu. Na katika hitimisho langu, natafsiri kuwa mauaji yanayoendelea katika maeneo ya Mkuranga, Kibiti na Rufiji ni ugaidi unaofanywa na kundi lenye asili ya nje ya Tanzania lakini lenye ufuasi wa kutosha nchini humo, na linapatiwa msaada na wakazi wa eneo hilo.

4. Kuhusu 'mashehe wa UAMHO,' hakuna ushahidi wa moja kwa moja kuthibitisha kauli ya Rais Magufuli hivi karibuni iliyoashiria kuwa kuna uhusiano kati sare za jeshi zilizokamatwa hivi karibuni, mashehe wa UAMSHO na mauaji ya MKIRU. Kinachowezekana ni wahusika (magaidi) wanaweza kutumia suala la mashehe hao kama sababu ya kufanya ugaidi wao.

5. Tukiafikiana kuwa mauaji ya MKIRU yanafanywa na magaidi, na tukiafikiana pia kuwa magaidi hao wanaweza kutumia suala la 'mashehe wa UAMSHO' kama moja ya sababu zao, bado ni muhimu kuepuka kulifanya suala hilo kuwa linatokana na masuala ya kidini. Kama ambavyo kuna wanasiasa wanaotumia mauaji hayo kuendeleza chuki za kisiasa na hatusemi siasa ndio chanzo cha mauaji hayo, ndivyo ilivyo kwa wanaoweza kutumia dini kama kisingizio cha kufanya ugaidi. Hili ni muhimu sana kuzingatiwa kwa sababu asilimia kubwa ya wakazi wa MKIRU ni Waislamu, na kuhusisha ugaidi huo na Uislamu/Waislamu sio tu itaathiri uwezekano wowote wa ushirikiano baina ya wakazi wa eneo hilo na vyombo vya dola/serikali bali pia inaweza kuzua balaa la machafuko ya kidini.

6. Tukiafikiana kuwa kinachoendelea huko MKIRU ni ugaidi basi itabidi pia tuafikiane kuwa mapambano dhidi ya ugaidi yanahitaji uwekezaji mkubwa kweli intelijensia kuliko matumizi ya nguvu. Taarifa kwamba baadhi ya wakazi wa maeneo ya MKIRU wamelazimika kuhama makazi yao kwa "kuhofia vipigo kutoka kwa Polisi" zinafanya uwezekano wa kupata ufumbuzi kuwa mgumu.

7. Kwa wanaofahamu vema pwani ya mkoa wa Pwani sambamba na jiografia yake na mikoa ya jirani watatambua kuwa wingi wa "vipenyo" (ambavyo hadi hivi karibuni vilikuwa vikitumika kama 'njia za panya' kuingiza na kutoa bidhaa mbalimbali) na mtawanyiko wa makazi yaliyochanganyika na mashamba, mapori na misitu, vinaweza kuwa mazingira mwafaka kwa watu hao wenye nia mbaya.

Nihitimishe uchambuzi huu kwa kusisitiza kuwa intelijensia sio exact science. Nimejitahidi kadri nilivyoweza kuongozwa na ACH kufikia hitimisho husika. Lengo la kufanya uchambuzi huu sio kuonyesha mapungufu ya mtu au taasisi fulani. Nimekuwa nikitumia ACH kwa majukumu yangu binafsi, na nimeona sio vibaya kuitumia kwenye suala hili la MKIRU. Hakuna anayelazimishwa kuafikiana na uchambuzi huu.
CHANZO :-
Uchambuzi Wa Kiintelijensia Kuhusu Mauaji Ya [HASHTAG]#MKIRU[/HASHTAG] Kwa Kutumia "Dhana Zinazoshindana" (ACH)
Uchambuzi Wa Kiintelijensia Kuhusu Mauaji Ya [HASHTAG]#MKIRU[/HASHTAG] Kwa Kutumia "Dhana Zinazoshindana" (ACH) ~ Kulikoni Ughaibuni
 
Kujadili suala la usalama wa taifa ni kujipotezea muda, kwa always and will always be classified.

Usalama wa Taifa wanaweza kuua, kulemaza, ama kufanya lolote linalowezekana ili Nchi iwe salama.

Kama ikitokea ndugu yako anajihusisha na masuala yanayohtarisha usalama wa Nchi bola tu mmwonye mapema. Akigundulika na akashindwa kutoa ushirikiano always atadiappear tu au kuna namna mbaya itafanywa ili kumnyamazisha.

Issue ya usalama wa Taifa ni very sensitive. Kosa moja nchi inaangamia. Mbona hata ushahidi upo tena humu humu Nchini.

Mtoa maada yupo sawa japo watu wengine hutumia mwanya wa usalama wa Taifa kuwapoteza watu wasio na hatia.

Usalama wa Taifa is a very serious thing than any of us who are not them can imagine. And those guys take the real risk to make it happen. Ndio maana ukiwafanyia ujinga wanakupoteza tu na Nchi inaendelea kuwa na amani. Narudia tena kusema siasa ikiingiamo ni rahisi kuabuse majukum ya usalama wa Taifa.
 
Hapa hatuzungumzii jinsi walivyopambana nao bali tunazungumzia jinsi walivyo-handle Watuhumiwa!

Btw, ni FBI na CIA gani unaowazungumzia wewe?!

Inapotokea issue kama ya MKIRU, Marekani watatuma military task force kwa lengo la kuwakamata Watuhumiwa!!

Task force itaua Watuhumiwa only if necessary.

Watuhumiwa wakikamatwa watapelekwa kwenye detention facilities for interrogation!

Kama assault imefanyika ndani ya US na Watuhumiwa hawakutoa ushirikiano, watawahamishia kwenye Black Site nje ya US.

Kila mmoja anafahamu kwamba the "most dangerous" terrorist suspects walikuwa wanapelekwa Gitmo Military Detention Facility!

Hao ndio Wamarekani unaowatolea mfano... sisi hao wa kwetu wanapelekwa wapi?!

Suala la Gitmo halikuwa siri though walikuwa na uwezo wa kuwa-detain kwenye unlocated military facility let alone shooting them at first sight!

And look! Takribani 200 Detainees, including Tipton Three (Ruhal Ahmed, Asif Iqbal & Shafiq Rasul) baadae waliachiwa huru baada ya kuonekana hawahusiki!

What if kingefanyika kile kinachohisiwa kufanywa huko MKIRU dhidi ya Watuhumiwa?!

Si hivyo tu! Hata wale wengine walioonekana kuhusika bado waliendelea kuwa detained na hakikufanyika kile kinachohisiwa kufanyika MKIRU!

But look again!! In 2011 Wiki leaks walivujusha classified files kuhusu Gitmo Detainees zilizoonesha kuna Detainees wengine zaidi ya 150 iliosemekana walikuwa innocent!!

For more info, Google "2011 Gitmo Files". Hata The New York Times waliandika hii habari!

Unadhani wote hao walikamatwa kwa bahati mbaya?! It's obvious wengine walitajwa!

But look again! What if kama ingekuwa kimefanyika kile kinachohisiwa kufanyika MKIRU?

Sasa hao FBI & CIA unaowalinganisha na MKIRU ni FBI & CIA wa wapi hao?! Au kupitia operesheni yao ipi?
 
Nyie watu tangu torrents zianze kuachia pirated movies na series na za bure na mkaja kulifahamu neno "Classified" basi ni taabu tupu!!

Hivi kuna kosa kubwa nchi hii kwa jamhuri kama Uhaini?!

Ambacho kilitokea kwa Watuhumiwa wa uhaini back in the days ndo hiki kinachohisiwa kutokea MKIRU?!

What do you know about classified info?! Hivi watu wanahoji declassification of files au wanahoji ni wapi waliko Watuhumiwa wa ugaidi MKIRU na ikiwa kuna uhusiano wowote wa kutoonekana kwao na kuokotwa maiti kwenye viroba?!

Zitto anadai takribani watu 300 hawajulikani walipo! Ni mpumbavu tu ndie anaweza kutetea kutoweka kwa idadi yote hiyo ya watu pasipo na uchunguzi wa kuthibitisha tuhuma zao!

After 9/11, US walifanya kamata kamata sehemu mbalimbali duniani na Watuhumiwa kwenda kuwa detained at Gitmo only later to discover mamia miongoni mwao hawakuwa na hatia!

What if US wangefanya kile kinachohisiwa kufanyika MKIRU? Ni mamia mangapi wangekuwa wametangulizwa jehanamu pasipo na hatia?
 
Salute kwako!
Kuna watu wanatumia nafasi zao kisiasa kuvimbisha matumbo yao kwa lolote lile liwe la heri ama shari kwa taifa hili mradi tu liwafanye wawepo kisiasa (kiki)

Nimesoma taarifa ya ZZK. na nilimsikiliza kwa makini LEMA..
Nikajiuliza wanayasema haya kwa sabbu hawajui hasa maana ya uhalifu au chanzo cha machafuko katika Nchi na maana ya Usalama ?
Au wanafanya vile wakiwa wanajua isipokuwa wanataka kuwaghiribu watu wakati huo wakiwa wanapata mkate wao wa kila siku..

Nimeona majina aliyoyatoa Zito kabwe akielezea kadhia ya MKIRU.. hivi zito huyu hakuwepo hapa Nchini wakati mauji ya kibiti yakiwa yanaendelea?
Alikuwa Nje ya Nchi akaja kusimuliwa?
Kama alikuwepo alitegemea wimbi lile la mauaji lizimwe kwa kwenda kuwapigia magoti wauaji? Na kuwabembeleza waache kuuwa watu wasio na hatia?
Je wauaji walikuwa hawajui kuwa kuna sheria na mahakama zinazohusiana na haki endapo waliona kuna haki zao zinapuuzwa?

Leo zitto anaweka majina ya watu walio potea ama kutekwa au kuchukuliwa.. wakiwa ama wana taarifa za uovu au walihusika na uovu.!
Ina maana zito hafahamu kuwa polisi au wahusika wa usalama wanafanya hivyo wakiwa na taarifa muhimu wanazozitaka kutoka kwa mhusika? Na endapo mhusika hataki kutoa hizo taarifa kwa njia ya amani unataraji wanao hitaji hizo taarifa waanze kulia ama kufunga na kuomba ili wazipate toka kwake?

Huyu Zitto hakuwepo hapa Nchini wakati wa Mauaji ya kule Tanga ama lile Tukio la Amboni? Wahanga wa yale mauji je anawaambia nini?
Yale mauaji ya mskitini kule Mwanza..!
Au yale ya ukonga Staki shari polisi
Ama yale ya mbagala walipouwawa wale Askari?
Achilia mbali wana CCM walio uwawa kibiti. Kwake hawa wote sio kitu isipokuwa wale ambao kwa namna moja ama nyingine wanaotuhumiwa kusuka mipango ya mauji haya wanapohitajika na vyombo vya usalama kwake.ndio hoja!

Its none sense !

Amezungumzia kuhusianishwa na Dini nimkumbushe tu,

Nigeria Boko haramu wanaua wakiwa na Msimamo wa kidini (Uislam)

Somalia Alshabaa b wanaua watu wakihusianishwa na msimamo wa kidini (Uislam.)

Marekani walipigwa na Osam bin laden
Pia kulikuwa na chachu ya kidini (Uislam)

Waliofanya Mauaji Tanzania Tanga na Mwanza.
Walihusianishwa na dini (Uislam)

Nilikuwepo Znzibar wakati wa Vuguvugu la Jumuia ya uamsho wa Waislam Zanzibar.

Walioathiriwa wengi na vuguvugu lile ni Wakristo.! Makanisa yalichomwa moto watu waliuwawa.!

Yote hayo yakihusianishwa na (Uislam )

Je watu hawa wao hawakuona umuhimu wa kufuata sheria za Nchi kudai haki zao endapo waliona hawatendewi sawa wakaamua kuwa wauaji?

Inakuwaje wanapodhibitiwa ndugu zao wanapiga kelele bungeni kuwa haki zao zinazuiwa wale walio uwawa hawakuwa na haki ya kuishi?

Najua watadai kuna sheria za Nchi Je hizo zinafanya kazi kwao tu?

Kibiti lilikuwa ni tone tu la wimbi kubwa lililokuwa linakuja.

Hongera vyombo vyetu vya Ulinzi na Usalama.!

Hongera IGP na wakuu wenzio wote.!

Hongera Amiri Jeshi Mkuu umeonesha kuwa Tanzania ni Nchi na haiwezi kutekenywa ikacheka.

Nukuu kutoka kwa

IGP simon Sirro..

"Wamekuja kwa ubaya tutawajibu kwa ubaya"!..
Mwisho wa kunukuu.
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…