Mwekezaji aling'akia Bunge
*Ni Mmarekani anayemiliki hoteli mbugani Serengeti
*Mbunge asema anapewa kiburi na vigogo serikalini
Na John Daniel, Dodoma
WABUNGE wameonesha wazi kukasirishwa na kiburi cha baadhi ya wawekezaji wasiojali utu wa Watanzania na kuitaka Serikali kumchukulia hatua kali na mara moja mmiliki wa hoteli ya Guruneti VIP iliyopo katika mbuga ya wanyama ya Serengeti mkoani mara.
Mwekezaji huyo anadaiwa kuizuia Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali kufanya kazi yake kwa madai kuwa wageni wake hawataki usumbufu.
Licha ya kutaka kuchukuliwa hatua kali mwekezaji huyo, pia wameitaka Serikali kulieleza Bunge siri ya kiburi cha raia huyo wa Marekani, hadi kufikia hatua ya kuzuia chombo kikubwa kama Bunge kuingia katika hoteli hiyo jambo ambalo ni dharau kwa Serikali na wananchi.
Wakichangia Muswada wa Sheria ya Ukaguzi wa Hesabu za Umma wa mwaka 2008, iliyowasilishwa bungeni jana na Waziri wa Fedha na Uchumi, Bw. Mustapha Mkulo, wabunge hao walisema kutokana na kitendo hicho, mwekezaji huyo amepoteza sifa za kuwekeza nchini na anastahili kusitishiwa mkataba kwa utovu mkubwa wa nidhamu kwa Bunge, Serikali na Watanzania wote.
Sasa nchi hii imevamiwa katika sekta ya wanyamapori, CAG angepewa meno ya kuingia katika sekta hii na kuona mapato ya hawa watu, tulikwenda kule Mugumu (5/6/2008) katika hoteli ya Guruneti VIP pale Serengeti, tukazuiwa kuingia.
"Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali, sasa katika Tanzania hii wawekezaji wamejikatia ki-Tanzania chao, Serikali itusaidie kueleza huyu mwekezaji ametoa wapi kiburi hiki!, alisema Bw. John Cheyo ambaye ni Mbunge wa Bariadi Mashariki (UDP).
Kwa upande wake, Mbunge wa Karatu, Dkt. Wilbroad Slaa (CHADEMA), ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa, alisema ni lazima Serikali iliambie Bunge ni wapi mwekezaji huyo ametoa kiburi cha kudhalilisha Watanzania na kuona Bunge kama chombo ambacho hakiwezi kuingia katika hoteli yake.
Mimi kwa bahati nzuri nimetembea katika nchi nyingi mpaka huko kwao Marekani, kitu cha kwanza kwa mwekezaji ni kuheshimu Taifa lao, Waziri atusaidie huyu mwekezaji anazungumza na nani, kuna nani nyuma yake, na huko kuna nini?, alihoji Dkt. Slaa.
Naye Mbunge wa Kwamtipura, Bw. Zuberi Ali Maulid (CCM), alisema: Tulipotaka kwenda katika hoteli hiyo, tuliambiwa kwamba mwenyewe amekataa kwamba wageni wake hawataki usumbufu, hao watu walitoka katika sayari gani, Jupiter au Saturn?.
Nashauri sana tuwe makini katika mikataba, haya ni matusi kwetu na tena kwa chombo kikubwa kama Bunge, swali la msingi ni huko kuna kitu gani mpaka hataki tuingie, mkataba alioingia na Serikali ni wa aina gani, hapa lazima Serikali itupatie majibu, alisisitiza.
Mbunge wa Iramba Mashariki, Bw. Mgana Msindai (CCM), licha ya kulaani kitendo cha mwekezaji huyo, alisema eneo hilo lina utajiri mkubwa wa wanyama aina mbalimbali na kwamba alipokuwa Mkuu wa Chuo cha Wanyamapori cha Pasiansi, Mwanza, lilikuwa ni eneo maalumu kwa ajili ya mazoezi kwa wanafunzi, hivyo kitendo alichofanya Mmarekani huyo, kinaashiria kuna kitu ndani ya eneo hilo.
Naye Mbunge wa Kibakwe, Bw. George Simbachawene (CCM), alisema licha ya hatua kali ambazo atachukuliwa na Serikali, ni muhimu mkataba wake ukawasilishwa bungeni ili Bunge lijiridhishe kama hauna dosari na kuongeza kuwa kitendo alichofanya ni matusi kwa Watanzania.
Hoja ya mkataba huo kuwasilishwa mbele ya Bunge, iliungwa mkono na wabunge wengine wanne huku wakisisitiza kwamba si rahisi kwa mwekezaji mwenye mkataba wa kawaida kudhalilisha nchi kwa kiasi hicho na kwa kujiamini.
Katika hali isiyokuwa ya kawaida, Mbunge wa Vunjo, Bw. Aloyce Kimaro (CCM), alitoa siri na kueleza, kwamba kiburi cha mwekezaji huyo kinatokana na urafiki wake na Serikali.
Alieleza, kwamba alipohudhuria katika moja ya chakula cha usiku Marekani ambacho kiingilio kilikuwa dola 1,000 alishuhudia jinsi mgeni huyo alivyokuwa karibu na vigogo kadhaa wa Serikali ya Tanzania.
Nimesikitishwa sana na mwekezaji kuzuia Kamati ya Bunge kufanya kazi yake, kama amezuia Bunge je wananchi anawafanyeje? Ni lazima anawatesa, taarifa nilizonazo ni kwamba mwekezaji huyu ana jeshi lake kubwa pale na anawasumbua wananchi.
Huyu Bwana nilikutana naye kule New York, Marekani, na ni rafiki wa Serikali, kiburi alicho nacho ni cha Serikali; ameitukana Serikali sasa hana haki ya kukaa pale, aitwe ajieleze kwa Kamati hii kwa nini alifanya hivyo, Bunge hili ni la kisasa, tunataka kutenda haki, alisema Bw. Kimaro.
Hata hivyo, kutokana na kauli hiyo ya mwekezaji huyo kuwa na urafiki na vigogo wa Serikali, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Bunge, Bw. Philip Marmo, aliomba mwongozo wa Spika akitumia kanuni ya 68 kifungu kidogo cha kwanza akimtaka Bw. Kimaro atoe maelezo ya kina kuhusu urafiki huo.
Akijibu hoja hiyo, Bw. Kimaro alisema kutokana na maofisa wa Serikali walivyokuwa naye karibu wakati wa chakula hicho cha usiku Marekani na kwa mazingira yalivyokuwa, aliamini kwamba ni rafiki wa Serikali na kuongeza kwamba anazo picha zinazoweza kuthibitisha kauli yake kama zitatakiwa.
Akizungumza na Majira nje ya ukumbi wa Bunge, Mbunge wa Serengeti, Dkt. James Wanyancha, alikiri kwamba mwekezaji huyo anawatesa wananchi na kuongeza kuwa amepokea malalamiko mengi juu ya suala hilo.
Unajua tatizo ni kwamba yule mwekezaji amejenga ukuta pale na ukitaka kuingia lazima uombe kibali, ana askari wake ambao huwa wanaingia mpaka kwa wananchi kufanya ukaguzi na kuwapiga, swali ni kwamba wanafanya ukaguzi kwa ruhusa ya nani na je nani kampa uwezo wa kisheria kuunda Jeshi?, alihoji Dkt. Wanyancha.
Awali wakichangia Muswada huo wa Sheria ya Hesabu za Umma wa mwaka 2008, wabunge waliitaka Serikali kumpa meno kisheria na uwezo zaidi CAG, ili aweze kushughulikia tatizo la mapato katika sekta ya utalii, matumizi yasiyo ya lazima kwa Serikali hususan ununuzi wa magari ya kifahari bila sababu na kukamilisha miradi kwa wakati.
Walisema ofisi ya CAG inapaswa kujibu Bunge moja kwa moja na si kupitia Waziri wa Fedha kwa kuwa si rahisi mtu kukaguliwa kisha huyohuyo aliyekaguliwa akabidhiwe taarifa ya ukaguzi kwa ajili ya kuiwasilisha bungeni.
http://majira.co.tz/kurasa.php?soma=tanzania&habariNamba=6901