Naomba nifafanue kwa hao wachina na biashara zao.
Wiki hii nimerejea toka Chunya, eneo la Makongolosi, Mwaoga, Pantamela, Saza na Mkwajuni.
Maeneo hayo ni maarufu kwa uchimbaji mdogomdogo wa dhahabu ambapo wananchi huchimba na kisha kujipatia mawe, mawe ambayo huyapeleka kwenye crusher na kusagwa kuupata unga wa dhahabu ambao huchujwa kwa teknolojia ya kienyeji na kuambulia ama Points au hata Grams kadhaa za dhahabu.
Katika process zao za kuuosha huo mchanga na kuambulia dhahabu, huwa kuna udongo ambao hubakia. Udongo huo hujazana na kufikia mafurushi makubwa ambayo kwa wajasiriamali huyapima na kubaini ni asilimia ngapi ya dhahabu imesalia katika hayo 'marudio' na kisha huyafanyia uzalishaji mpya wa teknolojia ya kisasa kunasa dhahabu ikiwemo kwa kutumia 'cyanide processing'. Uzalishaji huo ambao ni RAHISI sana, hupelekea wajasiriamali hao kujipatia dhahabu kuanzia kilo moja mpaka kilo 5 kutegemea na aina ya tanks ulizojenga.
Aina hizo za uzalishaji wa dhahabu (sio uchimbaji), ni wa kienyeji na unaopaswa kufanywa na wazawa kwani hauhitaji mtaji mkubwa sana na uzoefu wangu si zaidi ya mil 400 unaweza kufungua na kuanza kuzalisha walau hata kilo 2 za dhahabu. Uzoefu huo ninao na nimeshuhudia.
Furushi moja la marudio ya udongo wa dhahabu huuzwa kati ya mil 10-60 kwa furushi, ambapo hawa wawekezaji wa nje ndio wameipandisha bei ya marudio na kuwafanya wazawa kushindwa kumudu ushindani kulingana na mitaji yao.
Pale wilaya ya Chunya pekee yapo makampuni zaidi ya 6 yakifanya shughuli hizo kienyeji. Wapo KASCO amewekeza bil 4 katika biashara hiyo, wapo Caspian eneo la kijiji cha Mwaoga, wapo hao wachina ambao wamekamatwa, wapo wahindi, wapo wazungu, wapo waarabu katika kijiji cha Pantamela.
Wapo wazawa kama vile Nyamaswa, wapo KICOL ambao wapo Mwaoga.
Biashara hiyo ilianzia eneo la Geita, Nyarugusu, Ishokera na kutawanyika maeneo mengine. Teknolojia hiyo ya uzalishaji dhahabu kienyeji imetokea Zimbabwe.
Ukifika Chunya utakutana na Wazimbabwe, Zambians na raia wa mataifa mengineyo wakijichumia dhahabu huku tumelala.
Kwa nini wachina wamekamatwa kirahisi?
Pale wilaya nzima ya Chunya kumeingia ushindani mkubwa wa kupata udongo wa marudio ya dhahabu, tena gharama zake zimekuwa ni kubwa sana. Kutokana na hilo basi, imepelekea Wachina kufata na kununua marudio Nzega na kuyasafirisha kwa malori hadi Makongolosi na kuweka hifadhi ya kutosha kuendesha uzalishaji huo. Serikali pale Chunya yajua fika kabisa.
Kwa sasa, udongo huo unagombaniwa sana katika kijiji cha Kitunda wilayani Sikonge mkoani Tabora, vikumbo vimeshamiri sana pale.
Mimi ni shuhuda wa yote yanayoendelea pale Chunya, wachina wamechomewa pia na wafanyakazi wao kwa kuwalipa malipo duni sana.
Chanzo: Mimi mwenyewe!