Na Mwandishi wa Habari Hub
Zanzibar, Juni 12, 2025
Katika juhudi za kukuza ushiriki wa wanawake katika siasa na demokrasia, Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA-Zanzibar) kimeandaa kikao kazi cha siku mbili kilichowakutanisha wadau kutoka taasisi 15 zisizo za kiserikali, wakijadili kwa kina suala la udhalilishaji na ukatili wa kijinsia katika nyanja za kisiasa, hasa wakati wa uchaguzi na kampeni.
Kikao hiki ni sehemu ya utekelezaji wa Mradi wa Wanawake na Uongozi, unaolenga kuwajengea uwezo wanawake kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kidemokrasia, sambamba na kubadili mitazamo ya kijamii ambayo huwazuia wanawake kushiriki katika uongozi.
Sabrina Mwintanga, ni Afisa Mradi wa Mradi wa Wanawake na Uongozi, alieleza kuwa kuna haja kubwa ya kufikia jamii moja kwa moja ili kuibadilisha mitazamo potofu dhidi ya wanawake katika uongozi.
“Tunataka jamii ielewe kuwa mwanamke ana uwezo kama mwanaume katika uongozi. Lakini bado kuna changamoto za vitisho, ulaghai wa kingono, na ubaguzi wa wazi”.
Salma Sadat ni muwezeshaji katika kikao kazi hicho aliongeza kuwa suala la ukatili dhidi ya wanawake linatokana na malezi na mitazamo ya kijinsia iliyoenea kutoka ngazi ya familia hadi kwenye vyama vya siasa.
“Tunaona jinsi wanawake wanavyochukuliwa kwa jicho tofauti, kuanzia majumbani hadi kwenye uteuzi ndani ya vyama. Ukatili wa kisiasa ni kikwazo kwenye kufikia adhama ya maamuzi kwenye vyombo husika”.
Kwa upande wake, Asma Ali Mkurugenzi wa Jukwaa la Vijana Zanzibar amesisitiza kuwa baadhi ya wanawake hufanyiwa udhalilishaji wa kingono kama njia ya kuwakatisha tamaa.
“Ukatili wa kisiasa una sura nyingi. Kuna wanawake wanaolazimika ‘kujionesha’ ili kupata nafasi. Hii ni aina ya ukatili na udhalilishaji ambao haupaswi kufumbiwa macho.”
Utafiti wa Inter-Parliamentary Union (IPU) wa mwaka 2021 ulionyesha kuwa 81% ya wanawake waliowahojiwa katika siasa za Afrika walikumbana na vitisho, unyanyasaji wa maneno au kingono.
Katika ripoti ya UN Women ya 2023,
ilibainika kuwa asilimia 43 ya wanawake waliwania nafasi za kisiasa nchini Tanzania waliwahi kudhalilishwa kwa maneno au kwa njia ya mitandao ya kijamii, huku wengine wakikumbana na vitisho vya maisha na ulaghai wa kingono.
Hamad Rashid ambaye ni Mkuu wa Idara ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA Zanzibar, amasema kuwa kua umuhimu wa maandalizi ya wanawake katika siasa mwanzo kabisa na sio kukurupuka.
“Siasa ni kujiandaa, kujipanga na kuwa na rasilimali. Hatuwezi kuzungumzia usawa bila kuwapa wanawake uwezo,” Hamad ameongeza kuwa “Katika chama chetu, tuko kwenye mchakato wa kukamilisha sera ya jinsia. Lengo ni kumlinda mwanamke na kuongeza ushiriki wake katika ngazi za maamuzi.”
Hanima Ali Sultani ni Afisa wa Dawati la Wanawake kutoka Chama cha Wananchi CUF, amegusia suala la ubaguzi wa kijinsia ndani ya vyama.
“Kuna dhana ya kubaguana ambayo ipo ndani ya vyama na inaendelea,” Anaendelea kusema kuwa “Tunahitaji kukabiliana na hali hii kwa uwazi na kuhakikisha wanawake hawabaguliwi kwa misingi ya jinsia yao.”
Nae Mkurugenzi wa Jumuiya ya Wanawake wenye Ulemavu Zanzibar JUWAUZA Sabahi Mzee amesema hofu kuhusu ongezeko la ulemavu wakati wa chaguzi kutokana na vurugu na ukatili wa kisiasa ipo kwenye jamii.
“Kitu ambacho tunatamani kisitokee ni watu wenye ulemavu kuongezeka kutokana na uchaguzi. Kila mara watu wanapigwa, wanaumizwa na haya yote huongeza idadi ya watu wenye ulemavu”.
Harusi Mpatani ni Mkurugenzi wa Kituo cha Msaada wa Kisheria ZAHLO, amewashauri wanawake kutumia taaluma za sheria kuwalinda dhidi ya ukatili.
“Tumezoea kuona wanawake wakidhuriwa wakati wa uchaguzi. Sasa ni muda wa kujilinda na kutumia wanasheria waliopo kuwasaidia wanawake kisiasa”.