Nimeona niweke Extract ya New Labor law:
sehemu ya migomo tu:
Mzee FD, heshima yako mkuu
Kwanza shukurani kwa kutupeperushia extract ya new labor law hapa ukumbini. Pili, ningependa kutoa wazo la kupanua wigo wa mjadala nje ya sheria ulizozileta mbele yetu. Kwasababu binafsi naamini kuwa katika masuala ya nchi na ustawi wa wana jamii, nafikiri ni vema kuichungulia sheria katika ukamilifu wake. Hii ina maana kwamba, kutafakari mazingira yaliyopelekea kutungwa kwa hiyo sheria, nani walihusika kutunga hiyo sheria, kwa msukumo wa nani, na kwa manufaa ya nani.
Kwa mfano; viongozi wetu wamejilundikizia madaraka makubwa yasiyo na mipaka. Linapotokea jambo lolote linalowapa hudhia, wanatunga sheria mpya ili kuondoa hudhia. Hii imeonekana wakati wa migomo ya wanafunzi pale Chuo Kikuu-Mlimani/Muhimbili. Sheria zilizotungwa ziliambatana na masharti ya udhamini na uhuru wa wanafunzi kuonyesha itikadi zao za kisiasa. Sheria hizo zilitungwa kwa msukumo wa ndani ya nchi, na si kwa manufaa ya wanafunzi bali kwa manufaa ya viongozi wasiotaka kuchanga bongo na badala yake wanatafuta njia za mkato.
Tumeshuhudia wanafunzi wanasaini masharti yaliyojumuishwa katika sheria mpya za kujiunga na vyuo vikuu. Lakini wanakumbana na mazingira magumu alafu wanaamua kugoma. Je, katika hali kama hii, tutaangalia sheria walizosaini wanafunzi kabla ya kujiunga na chuo ili tuwahukumu? Au tutaangalia sheria katika ukamilifu wake. Vivyo hivyo, hata mgomo wa waalimu ulioongozwa na Mwalimu Mashanga miaka ya tisini mwishoni ulizaa sheria mpya za migomo.
Madaktari wetu wana kiapo cha maadili-"Nonmalficience"-do no harm to the patient. Pia, naamini kwa nchi yetu, udaktari ingawa ni proffesional, lakini ni swala la wito kutokana na mazingira magumu wanayofanyia kazi, hivyo lazima uwe na moral obligation. Daktari anapokuwa njia panda katika kutoa maamuzi, kwa maana kwamba, anaona wagonjwa mahututi wanaokaribia kufa, maadili yake ya kazi yanasema do no harm, dhamiri yake inamsuta, na mazingira yakazi hayamruhusu, anatakiwa atoe uamuzi gani? agome au aendelee na kufanya kazi katika mazingira hayo huku akipiga baragumu ingawa hakuna wa kumsikiliza? Who cares? wanaotakiwa kuchanga bongo wanatibiwa nje.
Katika mazingira ya njia panda ya namna hiyo, sheria za nchi zinatakiwa zichukuwe mkondo. Lakini zinatungwa na nani? kwa manufaa ya nani? Sheria nyingi za nchi yetu kuanzia mwaka 1992 zimekuwa zikitungwa kwa lengo la kuziba matundu ya mtungi uliojaa gesi. Serikali inajaribu kuziba mianya ya migomo kwa kuweka sheria ambazo zinafanya mazingira ya kuwepo migomo yawe magumu. Je tunaweza kuangalia hizi sheria na kuwahukumu madaktari baada ya migomo?
Lakini kuna sheria zinazotungwa kwa msukumo kutoka nje ya nchi kwa manufaa ya mataifa ya nje na makampuni yao. Mfano ili kuwavutia "wawekezaji" tulitakiwa kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji. Maana yake ni kuwa sheria za zamani zifutwe na zitungwe mpya. Makampuni ya watanzania yanalipa kodi lakini makampuni ya kigeni yanasheria zake za kodi ambazo ni tofauti na za watanzania. Nchi yetu ina sheria za kodi ya mapato kwa kila mtanzania anayefanya kazi au anayefanya biashara nchini. Katika hali ya kawaida, sheria za nchi za kodi zinatakiwa zisiwe za kibaguzi au kiupendeleo. Lakini Mkataba wa Buzwagi-Barrick unaonyesha kwamba sheria ya kodi ya mapato ya nchi yetu imelegezwa ndani ya mkataba kwa manufaa ya wafanyakazi wa Barrick.
Leo hii tunajiuliza kuwa inakuwaje mtu mwenye akili timamu akasaini mkataba na kampuni ya nje unayoitaka hiyo kampuni isilipe kodi. Lakini tunajua kuwa sheria ya madini inampa uwezo waziri kusamehe kodi kwa jinsi anavyoona yeye. Kama hivyo ndivyo, tunaweza kusema mawaziri wetu hawana makosa kwasababu hawakuvunja sheria za nchi. Ukweli utabaki kuwa sheria nyingi zinatungwa ili kufukia mashimo kwa manufaa ya wachache na sio kwa manufaa ya ustawi wa jamii yetu. Kwa mantiki hiyo hatuwezi kuziangalia sheria peke yake alafu tukatoa hukumu. Kama tulivyoona Buzwagi, wakati mwingine sheria za nchi zinafungwa na mikata fyongo. Hivyo, tunahitaji kupanua wigo wa mjadala na ikiwezekana kuiona mikataba ili kufanya uchambuzi ulio saihi.