Wafanyakazi wa zamani wa kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) wameiomba Serikali na Rais Samia Suluhu Hassan kuingilia kati mgogoro wao na Harbinder Singh Sethi, anayedaiwa kutaka kuwatoa kinguvu kwenye nyumba za kampuni wanazoishi hivi sasa.
Malalamiko haya yametolewa na Willibrod William Rwamugira, ambaye alikuwa mfanyakazi wa IPTL akihudumu kama dereva wa Bw. Sethi kwa takriban miaka minne kabla ya kampuni hiyo kufungwa.
Historia ya Mgogoro na Kufungwa kwa IPTL
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Rwamugira alisema kuwa chimbuko la tatizo hili lilianza pale mkataba wa IPTL na TANESCO ulipomalizika na kutokuongezwa tena.
Alisema kufuatia matatizo yaliyokuwepo na usitishaji wa uzalishaji umeme, Harbinder Singh Sethi alikamatwa na kuwekwa gerezani na ndipo uongozi uliobakia ulifanya maamuzi ya kupunguza wafanyakazi wote, na kubakiza wafanyakazi tisa (9) pekee kwa ajili ya kulinda mitambo, nyumba, na mali mbalimbali za kampuni.
Hivyo, Wafanyakazi hao wamedai kuwa wamefanya kazi ya kulinda rasilimali hizo kwa karibu miaka minne mfululizo bila kulipwa mshahara wowote.
Serikali ilipoingilia kati
Kwa mujibu wa Rwaugira baadaye, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali iliingilia kati suala hilo, ambapo kamati maalumu kutoka ofisi hiyo ilifika kiwandani na kufanya tathmini (inventory) ya kina ya mali zote za IPTL, ikiwemo mitambo, nyumba, na rasilimali nyingine.
Wafanyakazi walielezwa kuwa, kuanzia wakati huo, kampuni na mali zake zote zilikuwa chini ya usimamizi wa Serikali moja kwa moja.
Wafanyakazi waliwasilisha madai yao ya mishahara ambayo hawajalipwa kwa ofisi hiyo, na walipewa matumaini makubwa kuwa Serikali inaendelea na mchakato wa kuwalipa stahiki zao.
Soma Pia:
Sethi Kuibuka na Kudai Umiliki
Amani ya wafanyakazi hao imevurugika hivi karibuni baada ya Sethi kuibuka na kuwataka wampishe kwenye nyumba hizo kwa madai kuwa anataka kuziuza. Wafanyakazi wamepinga amri hiyo vikali, wakisisitiza kuwa wao walikabidhiwa kulinda maeneo hayo na Serikali ambayo ndiyo wanayoitambua.
Ili kuthibitisha kuwa Sethi hana mamlaka ya kisheria ya kuuza mali hizo na kwamba hakuwa mmiliki halisi, Bw. Rwamugira aliwasilisha nyaraka zifuatazo mbele ya waandishi wa habari:
Nyaraka, ikiwemo barua ya toleo la ajira yenye tarehe 10 Julai 2014, inathibitisha kuwa Bw. Sethi aliajiriwa na Bodi ya Wakurugenzi kuwa Mwenyekiti Mtendaji (Executive Chairman) wa IPTL.
Kwa mujibu wa mkataba huo wa ajira, Bw. Sethi alikubaliwa kulipwa mshahara halisi (Remuneration - NET) wa Dola za Marekani 150,000 (USD 150,000) kwa mwaka. Vilevile, hati za mshahara (Payroll) zinaonyesha kuwa aliwahi kuchukua mshahara wa zaidi ya shilingi milioni 500 kwa mwezi.
Wafanyakazi hao waliwasilisha nyaraka za hukumu inayoonyesha kuwa, kisheria, Bw. Sethi si mmiliki wa kampuni ya IPTL tena.
Wafanyakazi hao wamesema wanasubiri malipo yao kutoka serikalini baada ya kulinda mali hizo za mabilioni kwa miaka kadhaa. Wanaiomba kwa unyenyekevu Serikali, chini ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, itoe msimamo na kuwasaidia wasiondolewe kinguvu na Bw. Sethi, huku wakisubiri ahadi ya Serikali ya kuwalipa stahiki zao kukamilika.