Jumuiya ya Wahadhiri wa Kiislamu nchini Tanzania imewataka Waislamu wote nchini pamoja na Watanzania kwa ujumla kujitenga na hamasa na ushiriki wa maandamano yanayohamasishwa kupitia mitandao ya kijamii nchini ya Disemba 09, 2025 yakidaiwa kuratibiwa na Watanzania wasioishi nchini.
Rai hiyo imetolewa na Kiongozi Mkuu wa Wahadhiri wa Kiislamu nchini Tanzania Sheikh Rajab Salum wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam leo Novemba 19, 2025, akiyataja maandamano hayo kuwa batili na jambo lisilokubalika nchini.
Sheikh Salum pia akitaja ajabu ya maandamano hayo kuwa yanaratibiwa na watu wasioshiriki na wanaoishi nje ya Tanzania, amewataka wale wote wanaohamasisha maandamano hayo kurejea nchini ikiwa wana nia njema ili kuja kujumuika na Watanzania.
"Kuna maandamano yanadaiwa kuratibiwa Tarehe 09 Disemba. Ajabu ya maandamano haya ni kuwa wanayoyaratibu wako nje ya nchi, kuna dada mmoja yupo Marekani na mwingine akiwa nchini Kenya, niombe na nitoe angalizo kwa Waislamu kwamba msijihusishe kabisa na haya mambo na niwaombe hawa wanaohamasisha warejee nchini tuje tushiriki wote." Amesema Sheikh Salum.
Jumuiya hiyo ya wahadhiri inaungana na Jumuiya nyingine za Kiislamu ikiwemo Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) pamoja na madhehebu mengi ya Kikristo nchini kulaani uvunjifu wa amani, uharibifu na wizi wa siku na baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025, wakiwataka waumini wao kujitenga na vurugu na hamasa hizo na kuunga mkono hatua za maridhiano zilizoanza kuchukuliwa na serikali ya awamu ya sita ya Rais Samia Suluhu Hassan.
View attachment 3504435