Mimi ni mkazi wa Ulongoni A karibu na Bar ya Magogoni, Mtaa unaitwa kwa Makamba Jijini Dar es Salam hapa Ilala upande Kinyerezi, kero yangu ni umeme kukatika katika kila mara ifikapo saa moja jioni, yaani umeme unaweza kukatika hata mara 50 kwenye saa moja.
Tumeshawasilisha kero hii Tanesco kwa kuwapigia mara nyingi sana ila hawajawahi kutatua tatizo hili.
Wanasema watakuja kufunga Transfoma kila siku na tangu nimehamia mtaa huu ni mwaka wa nne sasa.
Tunaiomba mamlaka husika ifuatilie na kutatua tatizo hili haraka iwezekanavyo kwani wananchi tunaathirika kwa kiwango kikubwa. Tunaamini huduma bora na ya uhakika ya umeme ni haki ya kila mwananchi.
Habari, ndugu mteja.
Kwanza, tunaomba radhi kwa kuchelewa kutoa majibu kwa wakati, akaunti yetu ilikua na changamoto, ila kwa sasa ipo sawa.
Licha ya muda kupita, tuliona ni vyema kufuatilia hii changamoto, japo kufahamu kama ilitatuliwa au la. Kwahiyo, asante sana kwa kutufikishia taarifa hii. Mara baada ya kuipokea, timu yetu ilifanya uchunguzi wa haraka katika eneo husika ili kubaini hali ya changamoto hii.
Uchunguzi umebaini kuwa changamoto ya umeme mdogo haipo katika maeneo ya Ulongoni A na Kinyerezi kama ilivyoripotiwa, bali ipo katika eneo la Mongo la Ndege, jirani na Baa ya Magogoni, Mtaa wa Makamba. Aidha, imebainika kuwa maeneo ya Ulongoni hayana changamoto ya umeme mdogo kutokana na maboresho ya mtandao yaliyokwishafanyika katika maeneo ya Ulongoni, Berege na Kilimahewa. Vilevile, kwa kushirikiana na uongozi wa mtaa na baadhi ya wakazi wa eneo hilo, ilithibitishwa kuwa hawakuwa na changamoto hiyo. Hata hivyo, tunaendelea kufuatilia kwa karibu ili kubaini endapo kuna mteja yeyote anayekabiliwa na hali kama hiyo.
Chanzo cha tatizo katika eneo la Mongo la Ndege ni ongezeko la mahitaji ya umeme lililosababisha mtandao wa usambazaji kuzidiwa, pamoja na umbali wa mtandao wa msongo wa kati kutoka eneo lenye matumizi makubwa ya umeme.
Ili kupunguza athari za changamoto hiyo, tayari tumejenga njia mpya ya msongo mdogo wa umeme, kugawa mzigo wa matumizi na kuwahamishia baadhi ya wateja kwenye transfoma iliyo karibu. Kutokana na hatua hizo, kiwango cha umeme kimeimarika kutoka takribani volti 154 hadi volti 220.
Aidha, katika mwaka wa fedha 2026/2027, tumepanga kutekeleza maboresho makubwa zaidi katika eneo hilo, yakiwemo ujenzi wa laini mpya za umeme, ufungaji wa transfoma mpya na upanuzi wa mtandao wa msongo mdogo, ili kuboresha upatikanaji wa huduma kwa muda mrefu.
Tunawashukuru kwa kuendelea kutupa taarifa na ushirikiano wenu, kwani unatupa fursa ya kufuatilia changamoto kwa haraka na kuendelea kuboresha huduma zetu.
Asante sana! ^FL.