Wakili Aloyce Komba: Lissu ana kesi nzuri, mashahidi wa IGP, CDF na DCI walikuwa wa kuongeza tu

Wakili Aloyce Komba: Lissu ana kesi nzuri, mashahidi wa IGP, CDF na DCI walikuwa wa kuongeza tu

Elias Msuya

Platinum Member
Joined
Dec 23, 2011
Posts
267
Reaction score
1,014
f53020d9-1533-4996-8b8c-0a922ec37074.jpg.webp

Wakili Aloyce Komba, Wakili Kiongozi wa Haki Kwanza Advocates, ni mtaalamu wa mwenendo wa kesi za jinai, haki jinai na haki za binadamu. Katika mahojiano haya, anaeleza maana ya Mahakama Kuu kutowalazimisha mashahidi watatu waliokuwa wameombwa na upande wa utetezi katika kesi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu.

Komba anazungumzia nafasi ya mashahidi wa utetezi katika mfumo wa Common Law na adversarial system, mzigo na kiwango cha uthibitishaji katika kesi za jinai, pamoja na hoja kwamba ushahidi uliotolewa na upande wa utetezi unaweza kuwa tayari umetosha kujenga mashaka kuhusu mashtaka yanayomkabili Lissu.

Soma pia: Wakili Maduhu: CDF Jacob Mkunda,IGP Camillius Wambura Na DCI Ramadhani Kingai Na Utetezi Dhidi Ya Kesi Ya Uhaini Inayomkabili Mhe Lissu

Swali: Hatua ya Mahakama Kuu kutowachukulia hatua yoyote mashahidi watatu wa Lissu ambao ni Mkuu wa Majeshi, CDF Jacob Mkunda, Mkuu wa Jeshi la Polisi IGP Camillus Wambura na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Ramadhani Kingai, inaashiria nini kisheria?

Jibu:
Kwanza, mashahidi wa utetezi hawalazimishwi kuwa mashahidi wa upande huo. Wanaweza kuja mahakamani kutokana na wito wa mahakama, lakini wanapofika wanaweza kusema hawawezi kumtetea mshitakiwa au wanaweza kugeuka kuwa hostile witnesses. Katika mazingira hayo, upande uliowaita unaweza kuomba ruhusa ya kuwahoji kwa njia ya cross-examination.

Kwa hiyo, hao mashahidi pengine waliamua kusema, “Tumepata wito wa kuja mahakamani, lakini hujazungumza na sisi wala hujatuomba kuwa mashahidi wako.” Kuna watu wanafikiri kwamba mashahidi wa upande wa utetezi mahakama inaweza kuwalazimisha kuja, lakini kwanza unatakiwa kuwa na uhusiano huo wa ushahidi na mtu mwenyewe.

Inaonekana Lissu alitaka walazimishwe, na mahakama ikasema kama unataka hivyo, basi unaomba wito wa mahakama.

Lakini kama mtu amekuambia, “Hatuko tayari, hatuna haja ya kuja kwenye kesi yako,” kuna shida gani? Je, hiyo inamaanisha kwamba mshitakiwa ameathirika kwa kiasi gani? Anaweza kuendelea na mashahidi wengine ambao wamekubali kutoa ushahidi.

Hawa wanaweza kuwa mashahidi wazuri katika kesi, lakini huwezi kuwalazimisha. Sheria ya Ushahidi inaeleza pia kuhusu mashahidi ambao wanaweza kuwa muhimu kwa kesi, lakini hilo halimaanishi kwamba lazima walazimishwe kutoa ushahidi.

Kwa kawaida, mashahidi wa upande wa utetezi unawatafuta wewe mwenyewe. Kama mtu amekuja na kusema, “Unataka niwe shahidi wako?” anaweza pia kusema, “Mimi sitaki kuwa shahidi wako.” Anaweza kujiuliza, “Ninajua nini kuhusu kesi yako?”

Kwa mfano, DCI Ramadhani Kingai amesema hahusiani na Lissu na wala si rafiki yake. Sasa utamlazimishaje mtu kama huyo awe shahidi wako?

Swali: Lakini kwa mtazamo wako, Mahakama Kuu imekosea katika hatua hiyo?

Jibu:
Sisi wanasheria tunachosema ni kwamba Mahakama imeharibu mfumo wetu wa mahakama za Commonwealth na Common Law. Katika mfumo huo, upande ndio unaamua mashahidi wake ni akina nani.

Hapo ndipo tunapojiuliza itakuwaje. Sisi tuko kwenye adversarial system, ambayo kila upande unaamua namna ya kuwasilisha kesi yake na mashahidi wake.

Lakini katika baadhi ya nchi za Ulaya, kama Ujerumani na kwingineko, kuna mfumo wa inquisitorial ambapo mahakama yenyewe inaweza kufanya uchunguzi na hata kuamua mashahidi wanaoweza kuitwa.

Sisi tuko kwenye mfumo wa adversarial. Hata hivyo, mifumo yetu imeanza kuchukua baadhi ya mitindo ya Marekani, kama masuala ya Alternative Dispute Resolution (ADR) na plea bargain, ambayo hayakutokana na mfumo wetu wa asili kwa namna hiyo.

Kwa mfumo wa Common Law, kwa mtazamo wangu, ilipaswa mahakama iruhusu mashahidi wote ambao mshitakiwa aliomba waitwe, kwa sababu huo ndio mfumo wa kesi ya ushindani.

Swali: Hoja hii ilianza vipi katika kesi ya Lissu?

Jibu:
Ilianza Mahakama ya Kisutu. Hakimu aliposikia orodha ya mashahidi wa Lissu alishangaa, na hapo ndipo ilipotokea hoja kwa mawakili wa Jamhuri kwamba Lissu hakuwataja mashahidi hao wakati wa committal proceedings.

Lakini kwa maoni yangu, hilo halikuzuia Mahakama Kuu kuwaita mashahidi hao.

Kwa hiyo hilo lilikuwa tatizo kubwa kwa mahakama zetu kwa sababu linagusa namna mfumo wa adversarial unavyofanya kazi na haki ya upande wa utetezi kuwasilisha kesi yake.

Swali: Kwa hiyo, kwa kuwakosa hao mashahidi watatu, Lissu ana wakati mgumu katika kesi yake?

Jibu:
Hapana. Tundu Lissu tayari ameshatengeneza kesi yake vizuri sana.

Ninavyoona, alitaka kuwaongezea tu hao mashahidi wengine—IGP, DCI na CDF—ili kuona kama vyombo vya dola vinajua kwamba alifanya kosa hilo linalodaiwa. Alitaka tu kujazia ushahidi wake.

Lakini mpaka hapo, Lissu ana kesi nzuri kwa sababu bado kosa la uhaini halijathibitishwa.

Tumeona mawakili wa Jamhuri wakiuliza masuala mbalimbali kwa mashahidi wa upande wa utetezi. Lakini Lissu ametumia mashahidi wake kama John Mnyika, Amani Golugwa na ushahidi wake mwenyewe. Kwa mtazamo wangu, huo ushahidi unatosha kabisa kubomoa kesi hiyo. Sasa tunaiachia mahakama ifanye uamuzi wake.

Swali: Unaposema ushahidi huo unatosha, ni kwa misingi gani ya sheria ya jinai?

Jibu:
Kwenye kesi za jinai kuna vitu muhimu sana vya kujenga kesi. Kwanza ni burden of proof na pili ni standard of proof.

Burden of proof ni nani anatakiwa kuthibitisha kosa? Ni yule anayemtuhumu au anayemshtaki. Katika kesi ya jinai, ni Jamhuri au upande wa mashtaka ambao unatakiwa kuthibitisha kosa.

Halafu kuna standard of proof. Ni kwa kiwango gani wanapaswa kuthibitisha?

Kwenye kesi ya jinai, kiwango hicho ni beyond reasonable doubt—yaani kuthibitisha kosa bila kuacha mashaka yanayoweza kuwa na msingi.

Katika kesi za madai, tunazungumzia balance of probabilities. Lakini katika jinai kiwango cha uthibitishaji ni cha juu sana.

Ndiyo maana mara nyingi mtu wa utetezi hahitaji kuthibitisha kwamba yeye hana kosa kwa kiwango sawa na upande wa mashtaka. Anaweza kutengeneza mashaka katika ushahidi wa mashtaka.

Na kwenye kesi hii, kwa mtazamo wangu, mashaka mengi yametengenezwa mpaka watu wa kawaida wanaweza kuyaona.

Swali: Unasema mashaka hayo yanahusiana pia na kifungu cha uhaini?

Jibu:
Ndiyo. Kifungu kinachohusu uhaini hakijarekebishwa kwa namna ambayo ingeondoa maswali haya. Uhaini unahusishwa na vitendo kama kutaka kumuua Rais au kumpindua.

Sasa tunajiuliza, hayo maneno yanaelewekaje katika mazingira ya kesi hii?

Ndiyo maana hata Lissu aliwahi kusema kwamba hii ni kesi ya kwanza ya kiraia, kwamba hajajumuishwa na vyombo vyenye mamlaka ya kutumia silaha. Yuko peke yake bila kuwa mwanajeshi au mtu mwenye kiapo cha kutokuasi.

Kwa hiyo ukiangalia suala la kusema “tutaasi”, unajiuliza, je, Lissu ana hadhi hiyo ya kutokuasi? Aliapishwa wapi? Wenye viapo vya aina hiyo ni wanajeshi na baadhi ya vyombo vya usalama.

Hapo ndipo kuna maswali ya kisheria ambayo mahakama itabidi iyatafakari kwa kina.

Swali: Je, upande wa mashtaka ukitumia ushahidi wa matukio ya Oktoba 29, 2025, unaweza kuathiri kesi hii?

Jibu:
Ni kweli walitegemea kuleta ushahidi huo. Walikuwa na shahidi ambaye walitaka kumleta na ushahidi wake ukapingwa kisheria mpaka kufika Mahakama ya Rufani.

Kwa hiyo, hilo linaonyesha umuhimu walioupa ushahidi huo.

Lakini swali ni hili: Vitendo vya Oktoba 29, ushahidi wake uko wapi katika kuthibitisha kosa linalomkabili Lissu?

Kwa mtazamo wangu, kuna hatari ya kuingiza masuala ya kisiasa katika kesi ya jinai. Kesi ya jinai inapaswa kujengwa kwenye vipengele vya kosa na ushahidi unaothibitisha kila kipengele hicho.

Kwa hiyo, tusubiri Mahakama.

Swali: Unaona Mahakama inaweza kufikia uamuzi tofauti na unavyotarajia?

Jibu:
Inawezekana Mahakama ikamkuta na hatia. Hilo linawezekana, na kama itakuwa hivyo, litatushangaza.

Lakini mshitakiwa ana haki ya kukata rufaa. Huo ndio mfumo wa haki.

Kwa sasa, mimi naona ni muhimu tuache Mahakama itathmini ushahidi uliowasilishwa mbele yake, izingatie sheria, mzigo wa uthibitishaji na kiwango cha uthibitishaji kinachotakiwa katika kesi ya jinai.

Kimsingi, upande wa mashtaka ndio unaobeba mzigo wa kuthibitisha kosa. Utetezi unaweza kuibua mashaka katika ushahidi wa mashtaka, na kama mashaka hayo ni ya msingi, ndipo mahakama inapaswa kuyazingatia katika kufikia uamuzi wake.

Kwa hiyo, kwa upande wangu, suala kubwa si idadi ya mashahidi pekee, bali ni kama ushahidi wote uliowasilishwa umeweza kuthibitisha vipengele vya kosa la uhaini kwa kiwango kinachotakiwa na sheria.
 
Wakili Aloyce Komba, Wakili Kiongozi wa Haki Kwanza Advocates, ni mtaalamu wa mwenendo wa kesi za jinai, haki jinai na haki za binadamu. Katika mahojiano haya, anaeleza maana ya Mahakama Kuu kutowalazimisha mashahidi watatu waliokuwa wameombwa na upande wa utetezi katika kesi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu.
Naunga mkono hoja
Mimi kwa upande wangu, nilianza kuzungumzia uhaini hata kabla ya hii kesi
1789986352536.png

Ijue Katiba ya JMT kwa Jicho la Mtunga Katiba: Watanzania Tusishabikie Uhaini. Hukuna Uhaini wa Kauli na Maneno, Uhaini ni Mipango na Matendo
1789986405693.png

Uhaini My God!. Kuna Uwezekano Anadanganywa na Kadanganyika? I Don't Believe This!. Sitatizwi na Uongo Wao, Natatizwa na The Motives Behind Such Lies!

Wazalendo Wapenda Haki, Msiwe na Wasiwasi, Uhaini ni ...​

Pascal Mayalla: Kusema Tutakinukisha au kuandamana ..​

https://www.jamiiforums.com/threads...a-sio-uhaini-nasema-kama-mwanasheria.2419101/

P
 

Attachments

  • 1789986650609.webp
    1789986650609.webp
    266 bytes · Views: 13
  • 1789986690091.webp
    1789986690091.webp
    266 bytes · Views: 10
Hii kesi ni uoga wa samuya kuiogopa akili mingi za lissu, wivu tu kwa kuwa yeye kanyimwa hizo akili!
 
Back
Top Bottom