Tundu Lissu Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA, anakabiliwa na
kesi ya uhaini ambayo iliendelea katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Julai 30, 2025 ambapo ilihairishwa hadi Agosti 13, 2025.
Wakili wa Serikali, Nassoro Katuga, kwa niaba ya upande wa Jamhuri katika kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, aliomba mahakama kuahirisha kwa mara nyingine usikilizwaji wa kesi hiyo.
Ikumbukwe Tundu Lissu
alikamatwa April 9, 2025 akiwa kwenye mkutano wa CHADEMA, huko Mbinga, na kufikishwa Mahakamani Aprili 10, 2025, na kusomewa mashitaka 3 ikiwemo uhaini na kuchapisha taarifa za uongo kwenye mtandao wa kijamii wa X. Tangu alipofikishwa mahakamani, hadi leo Julai 31, 2025, zimepita siku takribani 113.
Madai
Kupitia mtandao wa Facebook ipo picha inayosambazwa ikiwa na ujumbe unaodaiwa kuchapishwa na wakili wa serikali Nassoro Katuga, anayeongoza jopo la mawakili wa serikali katika kesi inayomkabili Lissu.
"Ndugu zangu watanzania Samia ndio anayetoa maelekezo kwetu ili Tundu Lissu asiachiwe mpaka uchaguzi uishe kimsingi sisi wenyewe Mawakili wa Serikali tumeishiwa Pawa hakuna kesi pale ndugu zangu Lissu anaonewa tu"
Je, ni upi uhalisia wa ujumbe huo?
Ufuatiliaji wa kimtandao uliofanywa na JamiiCheck kwa kutumia utafutaji wa maneno muhimu (Key word search) umejiridhisha kuwa ujumbe huo si wa kweli ni wa kutengenezwa na wapotoshaji kwani haujachapishwa na Wakili Nassoro Katuga kwenye mtandao wa X kama inavyoonekana.
Vilevile Ujumbe una mapungufu kadhaa, ambapo picha haiakisi uhalisia kama ilivyo katika mtandao wa X. Mathalani kukosekana kwa alama ya Grok, nukta tatu zilizopo upande wa juu kulia zina maumbo ya mraba badala ya duara. Pia jina la mtumiaji linaloonekana katika ujumbe huo (Username) halipatikani katika mtandao wa X.