Wakirusha mateke juu, wasichana wa Kitanzania wapata nguvu katika kung fu ya Kichina

Wakirusha mateke juu, wasichana wa Kitanzania wapata nguvu katika kung fu ya Kichina

ldleo

JF-Expert Member
Joined
Jan 9, 2010
Posts
1,310
Reaction score
1,265
11bca9fe91554ead92f050bcb6f45e1b.png


Mariam Saidi Mfaume amekaza ngumi kwenye mkono wake mdogo, akashusha pumzi ndefu na kufyatua teke juu lililopita kwenye hewa yenye ukungu. Matone ya mvua yalidondoka kwa upole kwenye majani yaliyo juu, lakini hakuna kilichoweza kumzuia mtoto huyo mwenye miaka sita kufuata ndoto zake za kung fu.

Jioni yenye unyevunyevu nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam, nchini Tanzania, wakati watoto wengi wakiwa ndani ya nyumba wakikwepa mambo wasiyopenda, Mariam alikuwa akifanya mazoezi ya kung fu na kundi la wasichana, baadhi yao ni wakubwa na wengine ni wadogo zaidi yake, chini ya miti.

Walikuwa wakifundishwa na Mwalimu Saidi Mfaume, baba mzazi wa Mariam, mwalimu wa kung fu ambaye aliwahi kupata mafunzo katika Hekalu maarufu la Shaolin nchini China. Katika kumbukumbu za Mariam, Kung fu imekuwa sehemu ya ulimwengu wake katika muda wote.

"Nilianza kufanya mazoezi nikiwa na umri wa miaka mitatu," Mariam aliiambia Xinhua huku akiwa na tabasamu la ufahari usoni mwake, miguu yake ikiwa imetengana kidogo, na mikono ikiwa tayari kufuata amri ya kuzuia au kupiga. "Kung fu iko kwenye damu yangu."

Ukiangalia anavyorusha ngumi na mateke kwa usahihi kabisa, huku akiwa mzingativu na mwenye kujiamini, ni rahisi kusahau umri wake.

"Kitendo ninachopenda zaidi katika kupigana kung fu ni teke la kuruka juu," Mariam alisema. "Ninaporuka na kupiga teke kwa wakati mmoja, ninahisi kama ninaruka. Inanifanya nijisikie nina kasi na mwenye nguvu, kama vile walimu wa kung fu ninaowaona kwenye filamu."

Mariam anataka kuwa mwalimu wa kung fu kama baba yake.

"Nataka kufundisha watoto wengine, labda siku moja hata mimi pia niwe na shule yangu," alisema, akasita kwa muda mfupi ili kumwita mdogo wake Zarha mwenye umri wa miaka mitatu, ambaye amejiunga na mafunzo hivi karibuni. Wakiwa na nguvu kubwa na waliodhamiria -- wasichana hawa wawili ni wadogo lakini wakali, wakipiga teke kwenye mvua kana kwamba wanadansi na upepo.

Mita chache tu kutoka walipo watoto, Makrina Projest alijifuta jasho kwenye paji la uso baada ya mafunzo magumu ya saa mbili. Akiwa na umri wa miaka 21, Projest ni mwanafunzi mkubwa zaidi katika Klabu ya Kung Fu ya Hekalu la Shaolin yaTanzania na mmoja wa wanafunzi wanaojitolea zaidi.

Akiwa amevalia suruali nyeusi ya mazoezi na kitambaa chekundu kichwani, alisawazisha pumzi zake na kutabasamu. "Siku zote nilitamani sana kujifunza kung fu, tangu nilipokuwa msichana mdogo wakati nilipokuwa nikitazama filamu za Kichina za kung fu kwenye TV."

"Lakini hakuna aliyeniunga mkono," Projest alisema. "Wazazi wangu walisema huo ni mchezo wa wanaume. Ndugu zangu waliniahidi kuniandikisha, lakini hawakufanya hivyo."

"Kwa hiyo mwaka jana nilipopata mshahara wangu wa kwanza tu, niliutumia kujiunga na klabu hii. Ulikuwa ni uamuzi bora kabisa kuwahi kuifanya," alisema.

Kwa Makrina, kung fu ni zaidi ya harakati za kimwili; ni uwezeshaji binafsi.

"Mwanzoni nilikuwa naona haya, na hata niliogopa. Sasa ninajihisi mwenye nguvu. Ninatembea tofauti. Ninajichukulia tofauti," alisema. "Kung fu haihusiani na uchokozi. Bali inahusu kujidhibiti."

Alipoulizwa ana ndoto ya kuwa nani, Makrina hakusita. "Mkunfunzi. Mwalimu. Na labda siku moja, nitakwenda kutembelea China mwenyewe."

Mwalimu Mfaume, 38, sasa anatoa mafunzo kwa wanafunzi 10 wa kike wenye umri wa kuanzia miaka mitatu hadi 21.

"Wasichana wanapokuja kwenye mafunzo, huwa nawachukulia kwa uzito mkubwa," alisema. "Familia nyingi bado zinaona kung fu si mchezo wa wanawake. Lakini nimeona namna inavyobadilisha maisha, hasa ya wasichana."

Wanafunzi hawa kila mmoja ana hadithi yake, na kila hadithi huanza kwa ujasiri. Alisema. "Wengine huja bila sare au chakula. Kwa hiyo mimi huwapa kile ninachoweza, wakati mwingine viatu, wakati mwingine chakula. Ninazungumza na wazazi wao na kuwashawishi kwamba kung fu haitawafanya binti zao kuwa watu wa vurugu. Bali itawafanya wawe na nguvu zaidi."

Mfaume ambaye ni mzaliwa wa Dar es Salaam, alianza safari yake ya kung fu mwaka 2009, na mwaka 2013, alipata udhamini wa mafunzo ya miezi mitatu katika Hekalu la Shaolin, ambayo yalibadilisha uelewa wake juu ya sanaa hii ya mapigano. Mwaka 2014, alirejea tena China ili kupata mafunzo zaidi ya utamaduni wa China. Uzoefu huu ulimwezesha kuunganisha kung fu katika elimu ya nchini kwake na matukio ya kijamii.

Mbali na mvuto wake wa kitamaduni, kung fu ina uwezo wa kiuchumi ambao bado haujatumiwa. Mfaume alisema.

"Watu wengi wanafikiri ni burudani tu, lakini kung fu inaweza kufungua milango, kwa ajili maonesho, kwa ajili ya utalii, kwa ajili ya elimu," alisema.

Klabu yake hualikwa mara kwa mara kuonesha mchezo wa kung fu kwenye sherehe, makongamano, na hafla za kampuni za China. Ubalozi wa China nchini Tanzania pia umewaalika kushiriki katika sherehe za kitamaduni.

"Kuna mahitaji," alisema. "Tunachohitaji ni msaada."

Mfaume anatumai kuwa kung fu itatambuliwa sio tu kama burudani, bali kama uwekezaji katika kuwawezesha vijana, usawa wa kijinsia, na mawasiliano ya kitamaduni.

Wakati mvua ilipoanza kupungua, wasichana walijipanga kwa ajili ya shughuli yao ya mwisho. Wakiwa peku bila viatu na wakiwa wamedhamiria, walisogea mbele kwa pamoja, wakipiga ngumi, wakizuia shambulizi, na kupiga mateke kwa sauti kama za mdundo wa ngoma.

Mariam akaruka juu na kupiga teke, huku uso wake ukikunjuka kwa furaha. Baba yake alipiga makofi taratibu, sauti yake ikiwa tulivu na ya wazi.

Kuna ishara ya ndani kabisa wakati mtoto anaporuka hewani kwa ujasiri kama huo. Katika ulimwengu ambao fursa za wasichana mara nyingi huja zikiwa zinaambatana na rushwa ya aina fulani au kufungiwa milango kabisa, hapa katika kitongoji cha kawaida jijini Dar es Salaam, kung fu ya Kichina sio tu imetoa nguvu, bali imewapatia mbawa wasichana hawa.

Na maadamu kuna wasichana kama Mariam, na washauri kama Mwalimu Mfaume, mbawa hizo zitazidi kuwa imara.
 
Back
Top Bottom