Source:
Habari Leo
Shadrack Sagati
Daily News; Thursday,May 15, 2008 @00:01
Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba
amesema kitendo cha Chama cha Wananchi (CUF) kutaka kuingizwa katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni sawa na uhaini. Akizungumza na gazeti hili jana, Makamba alisema suala la kuundwa kwa serikali ya kitaifa kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2010 lilitolewa kama pendekezo na CUF, lakini yeye alilikataa.
Alisema suala la kuundwa kwa serikali ya kitaifa kamwe halikuwahi kujadiliwa kwenye vikao vyao. "Sisi tuliona hilo suala halituhusu bali linahusu dola, ndiyo maana tukalikataa kulijadili kwa kina," alisema.
Hata hivyo, wakati wa vikao hivyo kutojadili suala hilo kumbukumbu za kikao cha kamati hizo cha Januari 21, 2008 kilichofanyika saa 2.30 usiku, Kingunge Ngombale-Mwiru aliyekuwa mwenyekiti mwenza wa CCM alitoa taarifa ya mjadala wa suala hilo.
Kwa mujibu wa kabrasha la muhtasari wa vikao hivyo, Kingunge alianza kwa kusema "
wameelewana kuwa pande zote mbili zinataka ufumbuzi wa kudumu wa mpasuko wa siasa Zanzibar na kwamba unahitajika mustakabali mpya wa siasa ambao utatokana na uchaguzi ulio huru na wa haki mwaka 2010.
"Hata hivyo katika kipindi hiki cha kuelekea 2010 kuwe na njia ya kujengeana imani ambazo katika hatua za siasa zitajumuisha na Rais wa Zanzibar aliyepo madarakani kuteua mawaziri kadhaa kutoka CUF waingie serikalini.
"
Lakini kwa kuwa hili la Rais kuteua mawaziri kutoka CUF ni la dola na si la vyama, basi CUF watatayarisha mapendekezo yao na kisha watayawasilisha kwa CCM yaweze kufikishwa kwa viongozi wa juu."
Jana Makamba akizungumza na gazeti hili alisisitiza kuwa suala hilo halikujadiliwa na hawakufanya hivyo kwa vile Zanzibar kuna Rais halali ambaye alishinda uchaguzi uliopita, hivyo asingeweza kujadili kuundwa kwa serikali ya kitaifa kabla ya 2010.
Lakini kwenye muhtasari wa vikao hivyo, wakati wa mjadala wa suala hilo baadhi ya wajumbe walitaka ufafanuzi kuhusu suala hilo la baadhi ya mawaziri kutoka CUF kama ni ombi, makubaliano, au ni mapendekezo ya CUF.
Ndipo Makamba aliyekuwa mwenyekiti wa kikao alitoa ufafanuzi kwa kusema, "CUF itawasilisha mapendekezo yake rasmi kwa maandishi kwa Katibu Mkuu wa CCM ili naye ayawasilishe kunakohusika."
Jana katibu mkuu huyo wa CCM alisema alilikataa suala hilo la CUF kwa vile chama hicho kilitaka kuingia serikalini kwa kupitia mlango wa nyuma, jambo ambalo alidai haliwezi kamwe kutokea.
"Mimi nilikataa kwa sababu kuundwa serikali ya kitaifa ni pale tu ambako kuna mgogoro wa siasa, lakini Zanzibar hakuna kitu kama hicho, kujadili suala kama hili wakati kuna serikali ambayo iko madarakani kwa halali ni sawa na uhaini," alisema Makamba.
Pia katika kumbukumbu za vikao vya mazungumzo vinaonyesha kuwa suala la kuundwa kwa serikali ya kitaifa kabla ya uchaguzi wa 2010 lilianza kujadiliwa katika kikao Mei 3 hadi 9, mwaka huu.
Suala hilo lilikuwa katika ajenda ya pili ambayo ilikuwa inasema njia ya kuimarisha mazingira ya uelewano wa siasa na uendeshaji wa uchaguzi huru na haki Zanzibar.
Katika nyaraka za vikao hivyo inaonyesha kuwa CUF ilitoa masharti ya kumtambua Rais Amani Karume; lakini liambatane na dhamira ya dhati ya CCM kuihakikishia CUF kwamba kiongozi huyo naye atawatangaza wawakilishi wa CUF kuingia kwenye serikali ya kitaifa.
Pia chama hicho kilisema kitamtambua tu Rais Karume kama kitahakikishiwa kuwa lengo la mazungumzo hayo ni kuunda serikali ya pamoja mara tu baada ya mazungumzo kukamilika na makubaliano kutiwa saini.
CCM ilipokea pendekezo hilo la CUF na kuomba muda wa kulitafakari. Kesho yake ujumbe wa CCM kupitia kwa katibu wake Vuai Ali Vuai ulisema suala la uteuzi wa wawakilishi waliopendekezwa na CUF linazungumzika na ujumbe wa CCM utalifanyia kazi.
Hata hivyo, wajumbe wa CCM walisema tangazo la kumtambua Rais Karume aliyechaguliwa katika uchaguzi wa 2005 haliwezi kutumika kumlazimisha Rais aunde serikali ya pamoja kabla ya mwaka 2010.
Juzi CUF iliweka hadharani nyaraka mbalimbali kuonyesha makubaliano yaliyofikiwa katika mazungumzo hayo na namna walivyoandaa rasimu ya majadiliano hayo ambayo yalikuwa yatiwe saini na makatibu wakuu.