Akizungumza kwa kujiamini, Jussa, mmoja wa viongozi wenye ushawishi ndani ya CUF, aliwataja Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi na mke wa Rais wa Zanzibar, Shadya Karume, kuwa wana CCM wawili wenye uhusiano ama wa kikazi au kinasaba na chama hicho cha kisultani cha Hizbu.
Jussa ambaye alikuwa akikanusha madai ya kada mkongwe wa CCM aliyepata kuwa msoshalisti kiitikadi, Kingunge Ngombale-Mwiru, aliyeihusisha CUF na U-Hizbu, alisema chama hicho tawala ndicho ambacho kina historia ya kuwa na uhusiano na chama hicho cha kisultani.
Alisema inapofika mahali mtu mzima kama Kingunge akasema uzushi, ni dhahiri chama hicho (CCM) kimefikia mahala pagumu na kimepoteza dira na mwelekeo.
"CCM ndiyo ina sifa zote za mahusiano na Hizbu, na si CUF. Na kwa msingi huo, kama kuna hoja pia ya kurudisha Waarabu, hilo linapaswa kuhofiwa kutoka CCM na si kutoka CUF.
"CUF kiliasisiwa mwaka 1992, na viongozi wake wanne wakuu kutoka Zanzibar ni Seif Sharif Hamad, Ali Haji Pandu, Shaaban Khamis Mloo na Machano Khamis Ali. Wote ni wana-ASP wasio na chembe ya shaka.
"Lakini mawaziri wa Zanzibar wa hivi sasa, yupo ambaye anajulikana kuwa alikuwa mwanachama wa Hizbu. Waziri wa Maji, Ujenzi, Nishati na Ardhi, Mansour Yusuf Himid, ambaye ni ndugu wa mama mmoja na Shadya Karume, mke wa Amani Karume, wote wawili ni wajukuu wa Sheikh Mohammed Salim Jinja, ambaye alikuwa mwasisi wa Hizbu na ambaye wenyewe Hizbu wakimwita '‘Founding Father of Zanzibar Nationalism,"alisema Jussa.
Pia alisema yupo waziri mmoja katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoka Zanzibar ambaye amekuwa akiandika makala katika magazeti kuipinda CUF, alipata kuwa mwanachama wa Umoja wa Vijana wa Hizbu uliokuwa ukijulikana kama Youth Own Union (YOU).
Ingawa hakumtaja kwa jina, waziri anayetoka Zanzibar ambaye amekuwa akiandika makala kuiponda CUF kupitia magazetini ni Muhammad Seif Khatib, ambaye sasa ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Muungano.
Khatibu kabla ya kuingia serikalini alipata kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM (zamani UVT) kwa muda mrefu, miaka ya 1980.
Mbali na hao, alisema viongozi wastaafu, kama Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi na Spika mstaafu wa Baraza la Wawakilishi, Mzee Ali Khamis Abdallah, baada ya Uhuru wa Desemba 1963 (miezi kadhaa kabla ya mapinduzi ya Januari 12, 1964) waliteuliwa na serikali ya Hizbu kuwa makatibu wa kwanza (First Secretaries) wa Ofisi za Kibalozi za Zanzibar huko Indonesia na Misri.
"Ni bahati mbaya sana kwamba lugha zinazochochea ubaguzi na kujidai kuwakataa ma-Hizbu zilizotolewa katika Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM hazikukemewa hata na Mwenyekiti wa CCM mwenyewe.
"Ulitumiwa Uhizbu kukataa ufumbuzi wa kudumu wa mpasuko wa kisiasa Zanzibar wakati hao waliokuwa wakiwakataa ma-Hizbu ndio ma-Hizbu wenyewe," alisema Jussa katika kauli inayoweza kuamsha mtazamo mpya wa siasa za Zanzibar siku zijazo.
Mwisho wa kuchamba kwingi ssa CCM wamezidi kutapakaa mivi.