BigTall
JF-Expert Member
- Mar 9, 2022
- 525
- 1,257
Shule ya Msingi ya Green Acres iliyopo maeneo ya Mbezi Beach Africana, Dar es Salaam kuna matukio ya ukatili yameripotiwa kutokea, naomba kutumia jukwaa hili kupaza sauti ili haki ipatikane.Tukio la kwanza ni la ulawiti na udhalilishaji wa kingono ambalo limefanywa na Mkuu wa Shule hiyo anayejulikana kwa jina la Saleh Ayoub.
Mbali na huyo watuhumiwa wengine ni Mwalimu Abraham pamoja na Matron anayetambulika kwa jina la Eliminata.
Mwalimu Mkuu amuharibu Mwanafunzi
Mwanafunzi wa Darasa la 5 (jina nalihifadhi, hapa tumuite YYY) mwenye umri wa Miaka 11 alifanyiwa vitendo vya ukatili wa kulawitiwa na Mwalimu huyo mara kadhaa katika siku tofauti Mwaka huu 2024.
Mwalimu huyo akawa anamtishia mtoto kwa kumwambia ‘Ukisema nitamuua mama yako’, ikabidi awe kimya akiendelea kufanyiwa ukatili.
Mtoto akawa anaendelea kuumia huku mara kadhaa akimwambia mama yake ‘nataka kuhama hiyo shule’, alisema hivyo bila kutaja sababu, mama mtu akaamini labda anataka kuwafuata marafiki zake, hakujali sana kuhusu ombi hilo la mtoto wake.
Alipoona kila siku anasisitiza, ikabidi akubali kumhamisha ili kukwepa kero ya mtoto wake, baada ya kufanya hivyo ndipo Mtoto akafunguka kumwambia mama yake kuwa ‘Mwalimu Mkuu alikuwa ananichukua na kunipeleka chooni au kwenye chumba ananilazimisha kuvua nguo kisha kuniingizia mdudu wake huku nyuma’.
Mama mtu akaenda kuripoti Polisi, akatakiwa aende hospitali ya Serikali, mtoto akafikishwa Hospitali ya Tabata ya Serikali, ikabainika ameharibika sana sehemu zake za nyuma, akaenda Ustawi wa Jamii kufungua shauri pia.
Baada ya hapo Mtoto akapelekwa Mwananyamala Hospitali akapigwa bomba kwa kuwa ilibainika hawezi kuzuia haja kubwa tena.
Kinachoendelea kwa sasa ni kuwa Mtoto bado anaendelea na matibabu, Watuhumiwa walishikiliwa Kituo cha Polisi Oysterbay baada ya muda wakaachiwa kwa dhamana.
Mama mtu hajui mwelekeo wa kesi hiyo, kila akienda Polisi anapigwa kalenda, Watuhumiwa wapo shuleni wanaendelea kama kawaida.
Labda nielezee hao watuhumiwa wengine, ni Matroni na Mwalimu ambao inadaiwa nao wamekuwa na tabia ya kuwapiga na kuwaminya sehemu za siri Watoto shuleni hapo inapotokea wamefanya kosa au wamekiuka jambo lolote kinyume na utaratibu.
Maombi kwa Waziri Gwajima
Nitoe ombi kwa Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dorothy Gwajima ambaye amekuwa akionesha uwajibikaji yanapotokea matukio ya ukatili kufuatilia kwa ukaribu suala hilo ili haki iweze kutendeka kwa uwazi bila kuwepo kwa danadana.
Wamiliki wa Shule ya Green Acres wanatakiwa kuwajibika pia kwa kuwa kama huyu mtoto kaamua kumwambia mama yake, vipi kuhusu wengine ambao hawasemi chochote? Tutaamini vipi kama Watoto wetu wengine wapo salama?
MAMA MTOTO AZUNGUMZA
JamiiForums imefanya jitihada za kumtafuta mama mtoto ambaye anaeleza:
Hiyo taarifa ni ya ukweli, nipo namuuguza mwanangu, napambana mwenyewe hakuna wa kunisaidia, mwanangu ameharibika sana nyuma.
Kuna kesi mbili nimefungua, ya kwanza ni ya Ulawiti inayomhusu Mwalumu Mkuu Saleh Ayub, nyingine ni ya Shambulio la Aibu inayomhusu Mwalimu wa Darasa, Mr Abraham ambapo mtoto akikosea amshika kwenye makalio, anabinya kwa nguvu na kuyavuta, amewafanyia watoto wengi tu.
Matroli kule mtoto akikojoa kitandani anamshika sehemu zake kwa mbele na kuziminya kwa nguvu na kuzivuta, mtoto akilia anaendelea kuzivuta, akinyamaza anamuachia.
Kila nikienda Polisi Oysterbay ambapo ndipo kesi ilipo naambiwa faili lipo kwa Mwanasheria niwe mpole kwa kuwa kule kuna mafaili mengi.
Tangu nimeripoti kesi hii ni zaidi ya mwezi lakini hakuna kinachoendelea.
Baba mtoto hasapoti chochote, alimkatabaa, nimebaki napambana mwenyewe (analia), ninachotaka ni haki itendeke na mtoto wangu anakuwa Mwanaume kamili.
Ninachoomba ni Serikali inisaidie, isikie kilio changu na mwanangu, tunateseka kwa kuwa hatujuani na watu wenye nguvu Serikalini.
USTAWI WA JAMII
Afisa wa Ustawi wa Jamii anayeshughulikia suala hilo, Joyce Mtesigwa amezungumza na JamiiForums na kusema ‘Sisi tumeshafanya upande wetu, tumeshachukua maelezo ya mzazi na mtoto, amehojiwa, ametoa maelezo yake, tunasubiri haki itendeke shauri litakapofika Mahakamani.’
MPELELEZI WA KESI
JamiiForums ilipowasiliana na Christowelu Mkumbo, amesema ‘Ahh kuhusu kesi ya YYY (anamtaja jina la mtoto) wa Green Acres, mimi sina mamlaka ya kujibu chochote unatakiwa kufika ofisini kwa bosi wangu, mimi ni mpelelezi tu nipo chini ya Mtu, katika hilo no comment.’
MWALIMU MKUU WA GREEN ACRES AZUNGUMZA
Alipotafutwa Mwalimu Mkuu wa Green Acres, Saleh Yusuf kuulizwa kuhusu suala hilo, amesema ‘Mimi hilo jambo... labda umtafute Mkurugenzi wa Taasisi sio mimi, taarifa zote muulize mwenye shule. Asante sana kwa kunipigia.’
Aione Waziri Dkt. Gwajima D kwa hatua zaidi
Mwendelezo wa taarifa bofya...
~ Dar: Mwalimu wa Shule ya Green Acres anayedaiwa kumlawiti Mwanafunzi wake afikishwa Mahakamani
~ Watu 6 kutoa ushahidi Kesi ya Mwalimu wa Shule ya Green Acres anayetuhumiwa kumlawiti Mwanafunzi wake
~ Dar: Kesi ya Mwalimu Saleh Ayoub anayedaiwa kumlawiti Mwanafunzi yaahirishwa hadi Februari 17, 2025
~ Shahidi: Mwalimu Mkuu anayedaiwa kumlawiti Mwanangu alimwambia 'ukisema nitakupiga nikuvunjevunje'
~ Kesi inayomkabili Mwalimu wa Shule ya Green Acres anayedaiwa kumlawiti mtoto yaahirishwa hadi Machi 24, 2025