Wamiliki Shule Binafsi wapinga Serikali kuifungia Chalinze Modern Islamic

Wamiliki Shule Binafsi wapinga Serikali kuifungia Chalinze Modern Islamic

BARD AI

JF-Expert Member
Joined
Jul 24, 2018
Posts
3,591
Reaction score
8,826
Umoja wa Wamiliki na Maneneja wa shule binafsi Tanzania (Tamongosco), wameingilia kati suala la kufungiwa kwa Shule ya Chalinze Modern Islamic kuwa kituo cha mitihani wakitaka uamuzi huo utenguliwe.

Tamongosco wamejitosa katika sakata hilo ikiwa ni siku chache tangu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda kutangaza uamuzi huo baada ya kubainika watahiniwa saba walibadilishiwa namba za mtihani katika kituo cha mtihani chenye usajili na namba PS1408009.

Oktoba 25 mwaka huu, waziri huyo alichukua uamuzi huo kufutia malalamiko ya mtahiniwa Iptisam Suleiman Slim wa kituo cha mtihani cha shule hiyo kueleza alibadilishiwa namba yake ya mtihani wakati akifanya mtihani wa taifa wa darasa la saba uliofanyika Oktoba 5 na 6 mwaka huu.

Uchunguzi wa timu iliyoundwa ilibaini wanafunzi saba akiwemo Iptasam walibadilishiwa namba katika baadhi ya masomo yao hivyo Waziri Mkenda aliagiza kuchukuliwa hatua kwa watumishi wa shule waliohusika na kadhia hiyo pamoja na kukifungia kuwa kituo cha mitihani kwa muda usiojulikana.

Juzi, Mwenyekiti wa Tamongosco, Leonard Mao, alisema licha ya kupongeza hatua ya haraka iliyochukuliwa na Serikali kufanya uchunguzi ili kuthibitisha au kukanusha taarifa ambayo mtahiniwa husika aliitoa kupitia mitandao ya kijamii, umoja huo haujaridhishwa na hatua ya kufungiwa kwa kituo hicho.

Mao aliomba Serikali kuangalia namna sekta zingine zinavyosimamiwa na njia hizo zitumike hata kwenye elimu. Alisema kosa linapofanyika, adhabu iende kwa mtu husika aliyetenda kosa na sio kuwaadhibu wasio na hatia.

Katika kuwasilisha malalamiko yao, tayari umoja huo umeshaandika barua kwa Waziri Mkenda kueleza kutoridhishwa kwao na uamuzi huo wa kukifungia kituo hicho kwani athari yake ni kubwa si tu wa wanafunzi walio madarasa ya chini, bali hata kwa wazazi wanaolazimika kuhangaika kutafuta shule nyingine kwa ajili ya watoto wao na mmiliki wa shule ambaye hakuhusika kwa namna yoyote katika kosa lililofanyika.

“Tumebaini utata katika maeneo kadhaaa ikiwemo mazingira ya wanafunzi kupewa namba tofauti na zile zilizo kwenye mfumo wa Necta, matokeo ya uchunguzi na hatua ambazo Serikali imezichukua,” alisema Mao na kuongeza:

“Kwa lengo la kuona kwamba haki inatendeka na bila kuathiri dhana nzima ya kuhakikisha elimu bora inaendelea kutolewa kwa wote, tumeona ni vema kuiarifu wizara kuhusu maoni yake ili utata huo uondolewe kwa manufaa ya umma.”

Majibu ya Waziri

Waziri Mkenda baada ya kilichoelezwa na umoja huo; naye alisema amepokea barua ya Tamongosco na anayafanyia kazi mapendekezo waliyotoa.

Kuhusu kufungwa kwa shule hiyo alisema, uamuzi aliotoa ni kuifungia shule kuwa kituo cha kufanyia mitihani na sio kama shule, hivyo wanafunzi wataendelea kusoma, ila mitihani watatakiwa kufanya katika vituo vingine.

“Mapendekezo yao tumeyapokea, tutayafanyia kazi. Kuhusu hiyo kanuni inayozungumziwa (ya kufungiwa kituo) iko kwa ajili ya kudhibiti udanganyifu kwenye mitihani. Halafu niliweke wazi hili shule haijafungwa kwa watoto kusoma; imefungwa kuwa kituo cha mtihani, na lengo ni kuwafanya hata wenye shule wachukizwe na vitendo vya watu wanaojaribu kuchezea mitihani,” alisema Profesa Mkenda.

MWANANCHI
 
Huo umoja wamejitokeza ili kumuonyesha mwenzao kuwa umoja upo na wanashirikiana katika hali zote ila wanajitia upofu kutoelewa kuwa mwenzao alichofanya hakina afya kwenye mfumo wa elimu.

Shule haijafungiwa na masomo yanaendelea kama kawaida ila imezuiliwa kuwa kituo cha kufanyia mitihani.
 
Umoja umeshindwa kuongea chochote dhidi ya madhira makubwa waliyosababisha kwa watoto wadogo na familia zao ambao naamini hawakujiunga na hiyo shule ili waibiwe mitihani walijiunga wakiamini watafundishwa wafaulu kwa akili zao

Hawajaongea lolote kuhusu aibu ya familia za watoto walioitwa "hawana akili na walipaswa kufanyiwa mitihani"ila wametetea mwizi mwenzao ni aibu sana
 
kosa la mwajiriwa usihusishe shule, shule haikuwatuma kufanya hayo ,ingekuwa shule hiyo ni dini nyingine isingefungiwa mitihani
 
Hawa wenye shule wanajua hiyo ndo michezo yao.Wanateteana.Anne Marie,Hazina ,Tusiime nk nani asiyejua michezo yao. Mkuu wa Anne Marie Ametoka lupango kwa dhamana juzi.
 
Mmiliki wa shule anawajibika na kila kitu kinachofanyika ndani ya shule yake, kwa kuwa huo ndio wajibu wake.

Kwa namna tukio lile lilivyotokea, inaonekana kulikuwa na mtandao au mfumo rasmi ndani ya ile shule wenye kuratibu ule ujanja ujanja, na wala halikuwa kosa binafsi la mtu mmoja kwa maslahi yake binafsi.

Adhabu ile ni sahihi na halali.
 
  • Thanks
Reactions: Mu7
Mimi nilitegemea wale wakosoaji wangekuja na hoja hizi;

1. Kuhoji ni sheria zipi zimetumika kutoa adhabu ile (Wampinge waziri kwa kuhoji uhalali wa ile adhabu kisheria). Bahati mbaya sana Waziri alitoa ile adhabu kwa mujibu wa sheria za baraza la mitihani.

2. Wahoji ni kwanini wahusika halisi nao wasichukuliwe hatua za kijinai ili kutoa fundisho kwa wengine, lengo kuwalinda wamiliki wa taasisi kuingia kwenye hasara mara kwa mara.
 
kosa la mwajiriwa usihusishe shule, shule haikuwatuma kufanya hayo ,ingekuwa shule hiyo ni dini nyingine isingefungiwa mitihani
Kuna shule ilikuwa Segerea, dsm. Sisemi iliitwaje. Matokeo yake yaliwahi kufutwa na mmiliki ndie alikuwa mtuhumiwa mkuu wa udanganyifu wa mitihani.

Ni muhimu kwa serikali kuunda sheria itakayozuia mtuhumiwa wa udanganyifu wa mitihani kujishughulisha na masuala ya elimu.
 
Mwenye shule anahusika,kwanini aajiri mtu ambaye ni dishonest? Kwanini aajiri mtu ambaye ni non professional? Mfano Anne Marie DSM mkuu wa shule ni kijana aliyemaliza tu kidato cha sita,unategemea nini? Na mwenye shule hawezi kujitetea kwakuwa huyo kijana kamaliza shule hiyo hiyo na alikuwa anamsomesha yeye mwenyewe.Wafungiwe tu.
 
kosa la mwajiriwa usihusishe shule, shule haikuwatuma kufanya hayo ,ingekuwa shule hiyo ni dini nyingine isingefungiwa mitihani
Mahaba kwa dini yamekupofusha hata huoni ukubwa wa kosa lililofanyika. Hiyo dini inaonewa ili iweje kwanza? Wamefanya kosa, wameadhibiwa. Ulitaka washangiliwe ndio ujue wametendewa haki? Unaboa we kiumbe!
 
Umoja wa Wamiliki na Maneneja wa shule binafsi Tanzania (Tamongosco), wameingilia kati suala la kufungiwa kwa Shule ya Chalinze Modern Islamic kuwa kituo cha mitihani wakitaka uamuzi huo utenguliwe...
Bila kuwaadhibu na wamiliki wa shule itakuwa ni kupoteza muda, hivyo kituo kifungwe kufanya mtihani ili waone uchungu
 
Umoja wa Wamiliki na Maneneja wa shule binafsi Tanzania (Tamongosco), wameingilia kati suala la kufungiwa kwa Shule ya Chalinze Modern Islamic kuwa kituo cha mitihani wakitaka uamuzi huo utenguliwe...
Hapo ndipo utajua kuwa elimu ya Tanzania imeshikwa na wahuni.Hao ndio wanaturudisha nyuma miaka 50.Na pia kabla ya kupewa ajira ya ukuu wa shule unaambiwa fanya lolote watoto wafaulu.Huu ni ujinga mkubwa.
 
Back
Top Bottom