Ingawa mjadala huu ni wa muda mrefu kidogo, ila mwanzoni mwa mwezi huu, Mahakama ya Rufaa ya Tanzania ilitoa hukumu ambayo inawapa haki wanafunzi kama hawa kuweza kusoma bila haki zao za kuabudu kuingiliwa na serikali au mamlaka zingine. Haki za Binadamu wananchi wa Tanzania wanazohakikishiwa kwenye katiba ya sasa ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Haki zingine za kimataifa ambazo Tanzania imeridhia kuzikubali, inakataza kuwepo kwa sheria nyingine zozote ambazo zinakinzana na kuzuia raia wa Tanzania kutokuwa huru na kufurahia haki zao za msingi za binadamu ikiwemo ya kutokuzuiwa kupata elimu kwa sababu ya misingi ya dini zao.
Katika mjadala huu ambao umeendelea kwa muda mrefu hapa jukwaani, wengi wametoa maoni tofauti tofauti wakishuku au kupinga haki ya wanafunzi hawa kuendelea na dini na imani zao hasa katika vyuo hivi binafsi ambavyo vina sheria zao ambazo walikubaliana nazo wakati wanaomba kujiunga. Tafadhali soma nakala ya
HUKUMU ya Mahakama ya Rufaa maana inaweza kusaidia kupanua upeo wetu wa kuelewa haki wanazopewa wananchi, hasa inapokuja kwa maswala ya uhuru wa dini.
Wengine wametoa changamoto ya maisha binafsi ya wanafunzi hao ambayo huenda yanakinzana na madai yao ya kidini. Ingawa mimi binafsi nakubaliana asilimia 100 na changamoto hii maana kama unadai kuonewa kidini, angalau elekeza maisha yako kikamilifu kwa kufuata maadili ya dini hiyo. Lakini inaposoma hukumu hii, unagundua kwamba "Dini" au "Imani za Kidini" kisheria inapewa tafsiri pana kabisa na tafsiri binafsi za kidini nazo zina nguvu ya kisheria. Kwa hiyo mbele ya sheria, kinachotakiwa tu ni kwamba ile haki inayodaiwa inadaiwa kwa dhati, katika kipengele tu cha haki hiyo na kwamba dhamiri ya mhanga wa kunyimwa haki hiyo anaamini kwa dhati kabisa kwamba (kwa tafsiri hii), kufanya mtihani siku ya Jumamosi hakuridhiwi na maadili ya imani yake. Kwa hiyo utaona swala la dhamira binafsi ni muhimu katika sheria, na ingawa ni kinyume kabisa kimaadili, lakini mbele ya sheria, wanafunzi hawa bado wana haki ya kikatiba na kisheria kutokufanya mitihani siku ya Jumamosi na kuruhusiwa kuendelea kusoma (labda kwa kufanya mitihani siku nyingine ya wiki) kama dhamiri yao inawahimiza kufanya hivyo hata kama kwenye maeneo mengine ya kidini (mfano kingono kama ilivyoelezwa awali), wanaweza wasiwe makini sana, lakini kinachohesabiwa ni Dhamiri binafsi ya mhusika.
Niwatakie siku njema na wiki njema.