SI KWELI Wanafunzi waliochelewa kuripoti shule ya wasichana ya Lucas Malia walala mtaani baada ya kuzuiwa kuingia

SI KWELI Wanafunzi waliochelewa kuripoti shule ya wasichana ya Lucas Malia walala mtaani baada ya kuzuiwa kuingia

Baada ya kuitathmini taarifa hii, tumebaini kuwa si ya kweli.
Wakuu,

Nimekutana na ujumbe unasambaa kwenye mitandao ya kijamii Twitter, Instagram na hata humu JF nimeona mtu kaweka uzi kuwa wanafunzi tena wakike kutoka shule ya wasichana ya Lucas Malia walifungiwa mlango na hivyo kulazimika kulala nje sababu eti walichelewa kufika siku waliyotakiwa kuripoti shuleni. Tukio hilo limetokea Julai 9 na mpaka sasa hawajapolewa wako wanaranda tu mtaani.

download (2).jpg

Wakuu taarifa hii ni ya kweli?
 
Tunachokijua
Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Lucas Malia ipo Mkoa wa Lindi Wilaya ya Ruangwa Kata ya Mnacho. Shule ipo umbali wa kilometa 1 kutoka barabara kuu ya Ruangwa-Nanganga.

Ukifika kijiji cha Chimbila B. Shule ipo upande wa kulia ukitokea Nanganga na ipo kushoto ukitokea Ruangwa.

JUlai 11, 2023, Mtumiaji wa JamiiForums alitoa dokezo lililodai kuwa Shule ya Lucas Malia Lindi imekataa kupokea wanafunzi wa Kike walioripoti kwa kuchelewa. Hii ilikuwa ni Siku ya pili wanalala mitaani bila kujua hatma yao.

Kwenye dokezo hilo, baadhi ya wachangiaji walionesha kuunga mkono uamuzi wa shule hiyo wa kukataa kuwapokea wanafunzi hao walioripoti kwa kuchelewa huku baadhi wakilaani kitendo hicho kisicho cha kiungwana, ambacho ni hatari kufanyika kwa mtoto wa kike.

Undani wa tukio
Alipoulizwa na JamiiForums, Mwalimu Mkuu, Gladness Makongwa, amesema;

“Siwezi kulizungumzia suala hilo kwenye simu, zaidi ya hapo naomba uzungumze na Mkurugenzi wa Halmashauri.”

Aidha, Katibu Tawala Mkoa wa Lindi, Zuwena Omari Jiri, amesema;

“Taarifa iliwafikia wenzangu; Afisa Elimu wa Mkoa, Mkurugenzi na Afisa Elimu wa Wilaya, wameelekea Shuleni, watafanya kikao kujua kitu gani kimetokea na nini kinaendelea.”

JamiiForums ilifanikiwa pia kupata maelezo ya Frank F. Chonya, Mkurugenzi Mtendaji (W), Luangwa aliyethibitisha kuwa taarifa hiyo haikuwa ya kweli.

Akizungumzia suala hilo, Chonya alisema;

“Wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha nne wa shule hiyo, wote wameripoti shuleni kwa wakati. Wanafunzi wa A - Level ( kidato cha tano na cha sita) ambao kwa sasa tuna wanafunzi wa kidato cha sita pekee, waliosajiliwa ni 114 walioripoti hadi sasa ni wanafunzi 111 wanafunzi 6 kati ya hao 111 wamesimamishwa masomo kwa sababu ya utovu wa nidhamu na wasioripoti hadi sasa ni wanafunzi 3.”

Aidha, Wanafunzi 6 waliosimamishwa masomo wameshachukuliwa na wazazi wao moja kwa moja kutoka shuleni hapo.

Aliendelea kufafanua kuwa Kufuatia tarifa iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii, walichukua hatua za Kufika kwenye shule hiyo, kuzungumza na kuhoji watumishi wakiwemo walimu na wanafunzi na wote wamethibitisha kuwa hakuna mwanafunzi aliyekataliwa kupokelewa kwa sababu yoyote ile na hakuna mwanafunzi aliyelala mtaani kama ilivyoenezwa kwenye mitandao ya kijamii.

“Kwa maelezo hayo ni wazi kuwa taarifa iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii, si sahihi.”

Amemaliza kwa kutoa wito kwa waandishi wa habari, kuendeleza weledi wa taaluma ya uandishi wa habari na maadili ya kazi hii muhimu kwa jamii.

Aidha; ni muhimu sana kwa mwandishi wa habari kuandika na kueneza habari sahihi na kuepuka kuzua taharuki kwa jamii.
Hii nchi sijui shida ni elimu yetu? Kwa hiyo shule imekosa adhabu mbadala ya kuwapa wanafunzi ikachagua kuwaacha wawe omba omba mitaani? Wenye akili hawana mamlaka
 
Back
Top Bottom