maiko luoga
New Member
- Mar 2, 2017
- 1
- 0
Wananchi wa Kata sita zinazopitiwa na Mradi wa Umeme wa Madope Hydro uliojengwa kwenye Kata ya Lugarawa Wilayani Ludewa Mkoa wa Njombe wameulalamikia mradi huo kwa kushindwa kuwasaidia tangu uanzishwe mwaka 2016.
Baadhi yao akiwemo Bw, Bosco Mgina na Sabinus Haule wakazi wa Kijiji na Kta ya Lugalawa wamesema mradi huo haujawa msaada kwao kwani tangu uanze kutumika huduma yake imekuwa kikwazo kwa Jamii kauli iliyoungwa mkono na Diwani wa Kata hiyo Erasto Mhagama akisema anaamini wahusika wameshindwa kuuendesha.
“Mradi huu ulichakachuliwa tangu mwanzo Wananchi tunateseka yaani Umeme unakatika kila wakati hatuoni faida ya kuutumia, mitambo yake inaonekana iko vizuri lakini ufanisi hakuna kabisa, mbaya zaidi sisi tunalipa umeme huu shilingi 200 badala ya Shilingi 100 wanayolipa wenzetu wanaotumia REA kote nchini ” Alisema Sabinus Haule.
“Wataalamu wanasema umeme huu haujakamilika hasa zile nyaya haziwezi kufikisha Vijiji vyote, hali hiyo inaathiri sana shughuli za kiuchumi kwa Wananchi, kama inawezekana Serikali kupitia TANESCO ichukue huu mradi ili na sisi tupate huduma ya Umeme ulio kamilika” Erasto Mhagama Diwani wa Kata ya Lugarawa.
Mhandisi Kulwa Masanja Mtaalamu wa Kampuni ya Madope Hydro inayosimamia mradi huo alisema waliojenga mradi huo waliujenga chini ya kiwango kwani nyaya zilizofungwa ni ndogo ukilinganisha na Umeme unaotoka kwenye mitambo hiyo na Padre Eventius Mdendeni Mjumbe wa bodi toka Kanisa Katoliki lililobuni mradi huo amekiri mapungufu yaliyopo huku akiomba Serikali isaidie kuimarisha mradi huo ili uendelee kutoa huduma kwa Wananchi.
“Waya uliopo ni mdogo Vijiji vya Lusala na Utilili Umeme unashindwa kuwafikia tukiruhusu Umeme wa kutosha mtambo una trip, pia tukiruhusu laini zote mbili za mabondeni na milimani laini inakuwa ndefu sana, ukiangalia miundombinu iliyojengwa na wenzetu ilikuwa changamoto waya una milimita 25 badala ya milimita 100” alisema Masanja Mtaalamu wa mradi wa Umeme Madope Hydro.
“Michoro yote na mfumo mzima wa mitambo niliifanya mimi, huu Mradi ni wetu sote hata matatizo yanapotokea naomba tushirikiane pamoja sisi Kanisa Katoliki ambao tuliutafuta mradi na Serikali” Padre Eventius Mdendeni Mjumbe wa bodi ya Mradi wa Umeme Madope Hydro.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa Wise Mgina na Joseph Kamonga Mbunge wa Jimbo la Ludewa Walisema licha ya changamoto zilizoelezwa na watekelezaji wa mradi huo lakini Wananchi wanahitaji kuona wanapata huduma ya Umeme kwenye maeneo yao kwakuwa tangu mwanzo walihakikishiwa kupata huduma hiyo.
“Sisi shauku yetu kuona Wananchi wananufaika na mradi huu maana umekuwa na mda mrefu tangu Gridi ya Taifa haijaanza sisi tulishaanza Madope Hydro, lakini matumaini ya Wananchi wa hivi Vijiji ishirini ya kupata Umeme wa uhakika hayapo tena” Wise Mgina Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa.
“Mpaka pale kwenye Mitambo mambo yako safi kabisa tumefika hata kutoka tumechelewa, mimi kama Mbunge na Viongozi wa Serikali tuko pamoja nanyi mliobuni mradi huu, Kanisa Katoliki ndio lilianza mradi huu basi lawama zinaenda huko hali hii isije ikaathiri hata imani za baadhi ya Watu tukae pamoja tutafute suluhisho” Joseph Kamonga Mbunge wa Jimbo la Ludewa.
Jumla ya Fedha za Kitanzania kiasi cha Shilingi Bilioni mbili.4 zinahitajika kukarabati upya mradi huo ili uweze kusaidia upatikanaji wa huduma ya Umeme wa uhakika katika Vijiji ishirini vilivyopo kwenye kata sita zinazonufaika na Mradi huo ambazo ni Lugarawa, Lubonde, Mlangali, Lupanga, Madope, na Madilu, huku Wananchi wakiomba msaada Serikali iingilie kati kutatua changamoto hiyo.