Ukiwachunguza kwa kina utawaona ni watu ambao hawajasoma, kichwani wamekariri Qur'an tu, hawajuwi chochote kuhusu historia ya kisiwa chao. Watu dizaini hii ni wabaya kuishi nao, ni wanafiki mno.
Mbongo...
Hebu soma hayo hapo chini huenda ukapata kitu:
PITIO LA KITABU CHA KHAMIS ABDULLA AMEIR: ‘’MAISHA YANGU MIAKA MINANE NDANI YA BARAZA LA MAPINDUZI KHAINI AU MHANGA WA MAPINDUZI?’’
SEHEMU YA PILI
Huko nyuma nimeeleza kuwa nitaeleza ni waandishi gani walioandika vitabu vya kutisha. Katika makundi haya manne ni hili kundi la tatu la ‘’Waandishi Mavamizi,’’ ndiyo vitabu vyao vinatisha. Khamis Abdulla Ameir kitabu chake kinatisha lau kama haiwezekani kumjumuisha katika, ‘’Waandishi Mavamizi.’’
Khamis Abdullah Ameir kwa kuwa yeye ni mwanamapiduzi na kama mwanamapinduzi angependa mapinduzi yabaki siku zote, yawepo daima lakini mapinduzi ya neema yenye manufaa kwa Wazanzibari.
Kauli ya Khamis Abdulla Ameir iliyotawala kitabu hiki ni kuwa mapinduzi na muungano vimetokea kuwa janga kubwa kwa Wazanzibari.
Kwa ajili hii basi Khamis Abdulla Ameir amefungua mlango mpya wa kundi jipya la ‘’Waandishi Mtambuka,’’ anaeingia katika makundi yote ya waandishi.
Kinachomtofautisha yeye ni kule kusema kuwa mapinduzi ya Zanzibar ya 1964 hayajawanufaisha Wazanzibar bali yamewatwisha dhiki kubwa.
Kitabu ili kiwe kitabu ni lazima kiwe na elimu mpya ambayo haikuwapo kabla.
Vitabu vingi vilivyoandikwa kuhusu harakati za kudai uhuru wa Zanzibar vimepita kijuujuu katika kueleza mchango wa vyama vya wafanyakazi katika kupigania uhuru wa Zanzibar.
Msimamo wa Khamis Abdulla Ameir ni kuwa wakulima na wafanyakazi wawe ndiyo msingi wa mapinduzi na maendeleo ya Zanzibar.
Katika kitabu hiki Khamis Abdulla Ameir anaeleza mtanziko uliokuwapo baina ya vyama vya wafanyakazi vilivyokuwa vinaunga mkono ASP na ZNP.
Wakati ZNP ilikuwa imejikita katika kudai uhuru, ASP ilikuwa na msimamo tofauti wa kuukataa uhuru hadi pale Wazanzibar watakapokuwa wameelimika vya kutosha.
ASP ikiamini kuwa kulikuwa na Wazanzibar ambao walibaguliwa katika elimu. Wazanzibari gani walibaguliwa na Wazanzibari gani waliokuwa wakibagua?
Khamis Abdulla Ameir hakika ni mwandishi mgumu na jasiri.
Kwa ajili hii inahitaji mtu jasiri pia kufanya pitio la kitabu chake.
Katika dibaji ya kitabu hiki Ahmed Rajab anamueleza Khamis Abdulla Ameir kuwa ni mtu asiyesema, mtu mkimya.
Hili mimi nimeliandika katika mitandao ya kijamii niliposikia kuwa Khamis Abdulla Ameir ameandika kitabu.
Mimi niliyasema maneno hayo kwa kuzungumza na yeye kwa muda mfupi sana siku nilipokutana na mwandishi.
Muda wote mimi ndiye nilikuwa nazungumza yeye ananisikiliza na kutabasamu.
Hasemi ila maneno machache kitu nadra kwa wanasiasa.
Nilifurahi kuwa tathmini yangu ya Khamis Abdulla Ameir ilikuwa sawa kabisa.
Imekuwaje mtu asiyesema kasema sana katika kitabu chake?
Au ndiyo kile kisa cha bubu kusema kwa ajili ya uchungu wa mwanae?
Kitabu hiki ni kitabu cha kasi ni kitabu ambacho msomaji atajihisi yuko kwenye chombo kinachokwenda kwa mwendo mkali sana na kinaposimama kwenye kituo kimoja hakikawii haraka kinaondoka kwenda kituo kingine.
Mara yangu ya kwanza kumsikia Khamis Abdulla Ameir ilikuwa kutoka kwa Ahmed Rajab ambae aliniandikia na kunieleza historia yake akanitajia lakabu yake, ‘’Theoretician,’’ ambayo sikupata kuisikia kabla.
Ahmed Rajab alikuwa ananitahadharisha kuwa Khamis Abdulla Ameir ni mtu muhimu sana katika historia ya mapinduzi ya Zanzibar.
Wakati ule nilikuwa naandika pitio la kitabu cha Hashil Seif, ‘’Mimi Umma Party na Mapinduzi ya Zanzibar.’’
Kalamu ya Khamis Abdulla Ameir haina simile si kwa kwa kuhadithia matendo yatishayo yaliyotendeka Zanzibar wala kwa uchaguzi wa lipi aliseme na lipi aliache.
Mwandishi hakujifanyia uhariri yeye mwenyewe na inaelekea mchapaji na yeye hakuona sababu ya kuhangaika na mkasi wake wa kukata karatasi zenye yale yaogopwayo kusemwa khasa hadharani.
Nina hakika kabisa mkasi haukuwa katika zana zake za mhariri wa kitabu hiki.
Nimedokezwa kuwa wachaji wa ndani walikiogopa kitabu hiki.
Hili msomaji ataliona mapema kabisa mwanzo wa kitabu.
Mhariri alimwachia mwandishi uwanja wote atambe apendavyo.
Khamis Abdulla Ameir hakujali ikiwa anaemweleza yu hai au kafa, mtu mkubwa wa cheo au raia wa kawaida.
Mwandishi hakugeuza shingo yake kuangalia nyuma au kufikiria vipi ataonekana au kesho yake itakuwaje.
Khamis Abdulla Ameir amenyanyua shingo yake juu anatazama mbele kuangalia achangie kipi chenye manufaa kwa Wazanzibari na nchi yao kuwatahadharisha na makossa ya nyuma ili wasiyarejee tena.
Khamis Abdulla Ameir alishughulishwa na kuusema ukweli kama aujuavyo.
Hapa nitarudia kusema kuwa kitabu hiki si kitabu chepesi kukifanyia pitio hadharani.
Mwandishi hakujifanyia uhariri yeye binafsi lakini upendeleo huu unakoma kwake.
Mchambuzi w kitabu hawezi kuikanyaga ardhi aliyokanyaga Khamis Abdulla Ameir kwani yeye, mosi hana ujasiri aliokuwanao Theoretician na pili hana mbavu za kuubeba huu mzigo mzito alioubeba yeye kwani ni gunia zito lililojaa misumari yenye ncha kali.
Kitabu hiki si kitabu cha kawaida unachokikuta Masomo Bookshop.
Kitabu hiki ni kamusi la historia ya Zanzibar kuanzia pale siasa za kudai uhuru wa Zanzibar zilipoanza miaka ya 1950 hadi kufika utawala uliokuwako sasa.
Kitabu hiki, ‘’Maisha Yangu Miaka Minane Ndani ya Baraza la Mapinduzi Khaini au Mhanga wa Mapinduzi?’’ ni kitabu tofauti sana na vitabu vyote vya historia ya mapinduuzi vilivyopata kuandikwa.
Inawezekana tofauti hii imesababishwa kwanza na umri wa mwandishi na pili kuwa yeye hakuwa mchezea pembeni.
Khamis Abdulla Ameir yeye alikuwa mchezaji wa katikati.
Amenza siasa za ukombozi akiwa kijana mdogo mjini London katika miaka ya 1950.
Kaanza kushiriki harakati za kupigania uhuru wa Afrika Uingereza akisuhubiana na wazalendo wengine kama Peter Mbiu Koinange mmoja wa washirika sita wa Kenyatta maarufu kwa jina la ‘’Kapenguria Six,’’ waliofungwa Kapenguria kama wafuasi wa Mau Mau.
Kipindi hiki cha maisha ya Khamis Abdulla Ameir Uingereza ni kipindi muhimu kwa yale yatakayokuja kutokea Zanzibar hadi kufikia mapinduzi.
Ilikuwa Khamis Abdulla Ameir alipokuwa London ndipo alipofahamiana na Abdulrahman Babu na Ali Sultan.
Maisha ya vijana hawa watatu yatafungamana hadi Zanzibar itakapopata uhuru wake tarehe 10 December 1963 na kisha mapinduzi kutokea tarehe 12 Januari, 1964 mwezi mmoja baada ya uhuru huo kupatikana.
Vijana hawa watatu wote watajikuta jela wakishitakiwa kwa mauaji ya Karume mwaka wa 1972.
William Shakespeare alikuwa na ‘’Three Weird Sisters,’’ katika Macbeth.
Katika kitabu hiki tunao ukipenda, ‘’The Three Weird Brothers,’’ katika historia ya Zanzibar.
Kama Weird Sisters walivyokuwa burudani katika Macbeth, halikadhalika historia ya Khamis Abdulla Ameir, Abdulrahman Babu na Ali Sultan ni mkasa wa kutosha ndani ya kitabu hiki.
Vijana hawa wote watatu walishiriki kwanza katika kupigania uhuru wa Zanzibar kisha katika mapinduzi na mwishowe katika uendeshaji wa serikali ya Zanzibar baada ya mapinduzi.
Tofauti baina yao ni kuwa wale waliokuwa Scotland walikuwa wachawi hawa wa Zanzibar ni wanamapinduzi wa Kisoshalisti.
Hawa wote watatu wakaja kuhusishwa na mauaji ya Abeid Amani Karume.
Khamis Abdulla Ameir akiwa Memba wa Baraza la Mapinduzi kwa miaka minane.