Kuna tafiti za hivi karibuni zimethibitisha kwamba hata wanaume hupata hedhi, ingawa wanaume hawana alama za nje za kuwaonesha kwamba wako kwenye hedhi, kama walivyo wanawake ambao hutoka damu siku zao za hedhi zinapofika na kukamilika.
Dalili za mwanaume aliye kwenye hedhi ziko akilini zaidi, mwanamke asili yake ni kimwili zaidi, kihisia zaidi. Lakini mwanaume anapata usumbufu ule ule anaopata mwanamke anapokuwa kwenye hedhi.
Tofauti ni moja tu, kwamba mwanaume hatoki damu. Lakini kila mwezi, baada ya siku 28, hali fulani ya kiakili na kihisia itakuwa inajirudia.
Dalili za mwanaume aliye kwenye hedhi ziko akilini zaidi, mwanamke asili yake ni kimwili zaidi, kihisia zaidi. Lakini mwanaume anapata usumbufu ule ule anaopata mwanamke anapokuwa kwenye hedhi.
Tofauti ni moja tu, kwamba mwanaume hatoki damu. Lakini kila mwezi, baada ya siku 28, hali fulani ya kiakili na kihisia itakuwa inajirudia.
- Tunachokijua
- Hedhi ni tendo la kibaiolojia linalotokea kila mwezi kwenye maisha ya mwanamke aliyevunja ungo. Tendo hili huhusisha utoaji wa damu na tishu za mwili kutoka kwenye mji wa uzazi kupitia uke.
Mfumo wa homoni za mwili ndio huongoza mzunguko wa hedhi ya mwanamke. Japokuwa mzunguko huu unaweza kuchukua siku zozote kati ya 21-35, wanawake wengi huwa na mzunguko wa wastani wa siku 28 ambao kwa lugha rahisi hufahamika kama mzunguko wa kawaida.
Wastani wa siku 7 kabla ya kutokea kwa hedhi, namba kubwa ya wanawake huingia kwenye kipindi kinachotawaliwa na mabadiliko makubwa ya kimwili na kihisia.
Mabadiliko haya kitaalam huitwa premenstrual syndrome.
Dalili zake
Kipindi hiki huambatana na dalili za kuvimba na kuwasha kwa matiti, maumivu ya kiuno na mgongo, hasira, kukosa hamu ya kula, kukosa usingizi, wasiwasi pamoja na msongo wa mawazo.
Dalili zingine ni choo kigumu au kuhara, tumbo kujaa gesi, kiungulia na kichefuchefu, kufumuka kwa chunusi, msongo pamoja na kupungua kwa hamu ya kushiriki tendo la ndoa.
Siyo kila mwanamke hupitia changamoto hizi lakini ni ukweli ulio wazi kuwa namba kubwa ya wanawake huzikabili.
Wanaume hupata hedhi?
Hii ni hoja inayojadiliwa hapa. Inadaiwa kuwa wanaume pia hupata hedhi, lakini tofauti na wanawake wao huwa hawatoki damu, isipokuwa wao huwa na dalili za kihisia zaidi.
Tofauti na wanawake, wanaume huwa hawatoi mayai ya uzazi kila mwezi hivyo hawawezi kuwa na hedhi.
Wanaume huzalisha mbegu za kiume kila siku tofauti na wanawake ambao tendo la kuzalisha ka kukomaza mayai ya uzazi hufanyika kwa mzunguko wa mwezi.
Hata hivyo, tafiti za afya zinabainisha kuwa homoni za kiume huzalishwa kwa wingi kwenye nyakati fulani kuliko nyakati zingine. Mathalani, wakati wa asubuhi, kiasi cha homoni za testosterone huwa nyingi kuliko wakati mwingine wa siku.
Aidha, kama ilivyo kwa wanawake wanaofikia umri wa ukomo wa hedhi, wanaume wakizeeka hukabiiana pia na kipindi cha uzalishwaji mdogo wa homoni za kiume hivyo kuwafanya wapatwe na changamoto ya upungufu wa nguvu za kiume, msongo wa mawazo, sonona na kupungua kwa hamu ya kushiriki tendo la ndoa.
Kitaalam, kipindi hiki huitwa Male manopause.
Pamoja na uwepo wa mabadiliko haya kwenye mwili wa mwanamme, bado hakujakuwepo na uthibitisho wa kuwepo wa hedhi.
Baadhi ya tafiti za afya zinabainisha kuwa wanaume huwa hawapati hedhi, bali hupitia kipindi ambacho kitaalam huitwa “Irritable Male Syndrome” kinachosababishwa na kupungua kwa ya kiasi cha homoni za kiume (testosterone) mwilini. Kwa lugha rahisi, haya ni mabadiliko ya kimhemko na kihisia anayopata mwanaume pindi anapoanza kuzeeka.
Madai ya wanaume kupatwa na hedhi yamekuwepo tangu zamani sana. Mathalani, mnamo karne ya 17, wanaume wa Kiyahudi walihusishwa na hali hii, kwamba kama ilivyo wanawake, wao pia walikuwa wanapata hedhi kila mwezi.
Hii ilitafsiriwa kwa kutoa damu puani, wakati wa kukojoa na pindi mwanaume anapokuwa na bawasiri.
Mwishoni mwa karne ya 19 na mwanzoni mwa karne ya 20, watu wa zama kama vile mtaalamu wa masuala ya ngono na daktari Magnus Hirschfeld, daktari Havelock Ellis, daktari wa neva na mwanzilishi wa uchanganuzi wa kisaikolojia Sigmund Freud wameonyesha imani katika hali ya hedhi ya wanaume isiyo maalum na Freud mwenyewe alidai kuwahi kupata hedhi ya kiume.
Hata hivyo, JamiiForums haijaweza kupata uthibitisho wa kitaalam kuhusiana na uwepo wa hali hii kwa wanaume zaidi ya kubaini mabadiliko yanayohusisha homoni yanayotokea ambayo hata hivyo hayawezi kumaanisha hedhi.
Tafiti za afya zinakubaliana na uwepo wa mabadiliko ya homoni kwenye mwili wa mwanaume lakini hazithibishi uwepo wa hedhi.