Wizara ya Ardhi
Govt Institution
- May 14, 2024
- 306
- 165
Chunya, Mbeya
Wanawake Wilaya ya Chunya, mkoani Mbeya, wameonesha mwitikio mkubwa na kujitokeza kwa wingi kupata huduma katika Kliniki ya Ardhi inayoendelea wilayani humo.
Kupitia kliniki hiyo, wanawake takribani 130 wamefika na kupata huduma mbalimbali za ardhi ikiwemo umiliki wa ardhi, elimu, ushauri na ufafanuzi kuhusu masuala ya sekta ya ardhi.
Kati ya wanawake hao, 22 wamefanikiwa kupatiwa hati zao za umiliki wa ardhi ndani ya wiki moja tangu kuanza kwa kliniki hiyo Septemba 22, 2026, baada ya kukamilisha taratibu za upatikanaji wa hati hizo.
Takwimu zinaonesha kuwa asilimia 28 ya wanawake nchini Tanzania wanamiliki ardhi, hali inayochangiwa na uwepo wa mazingira wezeshi, yakiwemo Sera ya Taifa ya Ardhi ya mwaka 1995, Toleo la mwaka 2023.
Mmoja wa wanawake ambao wamefika kwenye Kliniki ya Ardhi inayoendelea Wilayani Chunya Bi. Maria Shembiru, mkazi wa Kitongoji cha Itumbi, Kijiji cha Itumbi, Kata ya Matundasi ameshukuru utaratibu na utendaji mzuri wa Wizara na kushuhudia kuwa yeye amepata hati zake nane na kuongeza kuwa Kliniki ya Ardhi imekuwa msaada mkubwa kwa wananchi kwa kuwafikishia huduma karibu na maeneo yao na wanapata hati zao kwa wakati.
“Siku ya leo nimefanikiwa kupata hati zangu nane. Zoezi hili ni jema kwa kuwa sijachukua muda mrefu kwa kweli. Nawashauri wanakijiji wenzangu ambao bado hawajafanikiwa kupata hati wafike kujiandikisha ili wapate hati zao. Huduma hii haina usumbufu na ni nzuri,” amesema Bi. Maria.
Kliniki ya Ardhi Kidijiti inaendelea kuwa jukwaa muhimu la kuwafikishia wananchi huduma zinazohusiana na ardhi kwa urahisi na kwa wakati, kupitia wataalamu wa sekta hiyo.
Kliniki hiyo inafanyika katika mikoa yote ya Tanzania Bara, kuanzia Septemba 22 hadi Oktoba 3, 2026, ikiwa na kaulimbiu inayohimiza “Kliniki ya Ardhi Kidijiti, e-Ardhi: Huduma Popote.”