NADHARIA Wanawake wanaoficha simu zao kwenye matiti, wako na hatari ya kupata saratani ya matiti

NADHARIA Wanawake wanaoficha simu zao kwenye matiti, wako na hatari ya kupata saratani ya matiti

Taarifa hii ni nadharia tu, tumeitolea ufafanuzi kwa kadiri ilivyowezekana
Hoja hii iko vipi kisayansi? Wanawake wanaobana simu zao katikati ya brazia na matiti, ni kweli kuwa wako katika hatari ya kuivaa saratani ya ziwa?

IMG_6758.jpeg
 
Tunachokijua
Saratani ya matiti ni aina ya saratani inayoanzia kwenye matiti ikihusisha titi moja au yote mawili kwa pamoja.

Hutokea baada ya kukosekana kwa udhibiti katika ukuaji wa seli zinazopatikana kwenye maeneo hayo. Kama ambavyo wanawake huugua saratani hii, wanaume pia wanaweza pia kupata saratani.

Sababu za kutokea kwa Saratani ya matiti
Kuna mambo mengi yanayochangia kutokea kwa aina hii ya saratani. Baadhi yake ni;
  • Mtindo wa maisha unaohusisha mlo, vinywaji, uvutaji wa sigara na kutokufanya mazoezi
  • Uwepo wa changamoto kwenye mfumo wa vichocheo (homoni) vya mwili
  • Mabadiliko yasiyo ya kawaida kwenye jini (gene) za mwili
  • Kurithi kutoka kwa wazazi jini (gene) zisizo za kawaida aina ya BRCA (BRCA1 na BRCA2)
Pia, wakati mwingine, saratani hii hutokea kutokana na sababu zisizo wazi sana.

Kuweka simu kwenye bra (sidiria) husababisha saratani ya matiti?
Katika kufuatilia madai haya, JamiiForums imepata maelezo yanayokinzana kutoka kwenye taasisi mbalimbali za afya.

Kwa mujibu wa taasisi ya Saratani ya Matiti, hakuna uhusiano wowote wa moja kwa moja kati ya tabia hii na kutokea kwa saratani ya matiti.

Pia, JamiiForums imebaini mambo yafuatayo;
  1. Utafiti wa Taasisi ya Afya ya Marekani (NHI) uliohusisha watu 420,095 unasisitiza kutokuwepo wa ushahidi wowote wa mionzi ya simu na kusababisha uvimbe wa saratani ya aina yoyote mwilini.
  2. Mionzi inayotolewa na simu huwekwa kwenye kundi la mionzi ya redio. Kwa mujibu wa taasisi ya Chakula na Dawa ya Marekani (FDA), mionzi ya simu ni himilivu na haina uwezo wa kusababisha aina yoyote ya saratani kama inavyodhaniwa na watu.
Waraka wa kituo cha Udhibiti na Kinga ya Magonjwa (CDC) kuhusu usalama wa mionzi inayotolewa na simu unabainisha kuwa hadi sasa hakuna taarifa za kina za madhara yake, lakini tafiti zaidi zinaendelea ili kutoa majibu sahihi.

Kwa upande mwingie, JamiiForums inatambua kuwa zipo tafiti kadhaa japo zimefanyika katika ngazi ndogo, zinazoonesha uwepo wa uhusiano mdogo kati ya kuhifadhi simu kwenye sidiria na kutokea kwa saratani ya matiti.

Mojawapo ya tafiti hizo ni ile yenye kichwa cha habari Multifocal Breast Cancer in Young Women with Prolonged Contact between Their Breasts and Their Cellular Phones” inayobainisha uwezekano wa mionzi ya simu katika kusababisha saratani hiyo.

Pia, utafiti wa Ya-Wen Shilh et al
“ The Association Between Smartphone Use and Breast Cancer Risk Among Taiwanese Women: A Case-Control Study” unatoa picha ya namna ambavyo mionzi ya simu inaweza kusababisha saratani ya matiti.

Hivyo, kwa hatua ya sasa, JamiiForums inachukulia jambo hili kama nadharia inayohitaji kufanyiwa tathimini na uchunguzi zaidi ili kubaini ukweli kutokana na uwepo wa taarifa zinazo kinzana.

Japo ni chache, tafiti zinazoelezea uhusiano wa uhifadhi wa simu kwenye sidiria na kutokea kwa saratani ya matiti hazipaswi kupuuzwa. Zinaweza kuleta taswira mpya inayohitajika kwenye uwanda wa sasa wa sayansi na tiba.
Back
Top Bottom