Wapemba Waanza Kukamatwa

Wapemba Waanza Kukamatwa

MAELFU ya wanchi wa Kisiwa cha Pemba, wametishia kuwa kesho kutwa wataanza kujisalimisha katika vituo mbalimbali vya polisi nchini, kushinikiza wazee saba waliopeleka barua Umoja wa Mataifa (UN) kuomba kisiwa hicho kiwe na serikali yake, wafutiwe mashtaka ya uhaini.
Wananchi hao ambao wanaunga mkono harakati zilizoanzishwa na wazee hao, wanatarajiwa kujisalimisha katika vituo ambavyo wazee hao wamekuwa wakiripoti baada ya kuamriwa na polisi kufanya hivyo kila Alhamisi.
Amri hiyo ilitolewa na polisi baada ya wazee hao, kukamatwa na kushikiliwa kwa siku tano katika vituo tofauti vya polisi kwa tuhuma za uhaini.
Katibu wa Wazee hao, Hamad Ali Mussa, alithibitisha suala hilo na kuvitaja vituo ambavyo wananchi hao wanatarajiwa kujisalimisha keshokutwa, kuwa ni pamoja na Makao Makuu ya Polisi, yaliyoko Madungu, Mkoa wa Kusini na Makao Makuu ya Kilimandege, yaliyoko Wete, Mkoa wa Kaskazini, kisiwani humo.
Hamad ambaye alizungumza na mwandishi katika ofisi za gazeti hili jana alisema, watu hao ni miongoni mwa wananchi waliojiorodhesha na kuweka saini zao kwenye barua na nyaraka walizozipeleka UN.
''Tunachowaomba polisi wasiwaue tu, kwa sababu baadhi ya watu siku hiyo watakwenda katika vituo polisi na watoto wao wachanga,'' alisema Hamad.
Alisema uamuzi huo umefikiwa, kwa vile 'kosa' linalodaiwa kutendwa na wazee waliokamatwa, lilikuwa ni maelekezo waliyopewa na wananchi hao.
Alisema wanapinga amri ya kuwataka wazee hao kuendelea kuripoti polisi kila Alhamisi, kwa sababu kosa wanalotuhumiwa kulitenda halipo.
Naye Dk Gharib ambaye ni mmoja wa wazee waliokamatwa alisema, mbali mateso mengi waliyoyapata walipokuwa wakishikiliwa kwa siku tano mfululizo, walinyang'anywa pasi zao za kusafiria pamoja na vitambulisho vingine.
 
Sahihi nyengine 50,000 kuongezwa

Pemba bado yatokota
na Saada Said

WAWAKILISHI wanne wa Chama cha Wananchi (CUF) ambao waliitwa na polisi juzi wamekataa kutoa maelezo yoyote wakati wakihojiwa katika Kituo cha Polisi cha Madema, Mjini Magharibi.
Uamuzi wa wawakilishi hao kukataa kusema lolote hasa baada ya kuambiwa kuwa wanachunguzwa kwa tuhuma za uhaini, ulitangazwa na wao wenyewe mbele ya wana habari jana.

Wawakilishi hao ambao walifika kituoni hapo saa 4:00 asubuhi kama walivyoagizwa, wakifuatana na Ussi Khamis, ambaye ni wakili wao ni Mohammed Salim Mulla (Mkoani), Said Ali Mbarouk (Gando), Hamad Masoud Hamad (Ole) na Assah Othman Hamad (Wete).

Akizungumza jana, Mbarouk alisema waliamua kukaa kimya wakati wa mahojiano kwa kuwa sheria inawaruhusu kufanya hivyo na kujibu maswali watakayoulizwa wakati watakapofikishwa mahakamani.

"Kuna mambo matatu, ukitaka unakaa kimya, ukitaka unajibu na ukitaka unakataa kujibu chochote mpaka utakapopelekwa mahakamani, kwa hivyo sisi tumetumia hiyo option ya tatu ya kutaka kujibu tutakapopelekwa mahakamani," alisema Mbarouk.

Alisema walipofika Makao Makuu ya Polisi Madema, walitakiwa kuingia mmoja mmoja ndani ya chumba maalumu kwa ajili ya mahojiano, lakini kila aliyeingia humo aliingia na wakili wao na alipotoka waliulizana na kubaini kuwa hakuna aliyejibu swali lolote.

Walisema kuwa maofisa wote waliowakuta katika chumba hicho cha mahojiano wanatoka Tanzania Bara.

Wawakilishi hao wakati wanakwenda Makao Makuu ya Polisi Madema kwa ajili ya mahojiano walikuwa tayari wameshajitayarisha kwa kuchukua vitu muhimu, vikiwemo dawa za viungo, miswaki na sabuni za kuogea, wakidhani kuwa wanaweza kuwekwa ndani.

"Hawaaminiki hawa na ndiyo tuliona tuchukue vitu muhimu, kwa sababu wangetuweka ndani. Mimi ni mgonjwa wa miguu, nimechukua dawa zangu za misuli kabisa," alisema Mulla.

Wawakilishi hao walisema kuwa walipofika kituoni hapo waliambiwa kuwa waliitwa wakihusishwa katika tuhuma zinazohusiana na hatua ya wazee 12 wa Pemba kupeleka waraka Umoja wa Mataifa, wakitaka pamoja na mambo mengine kisiwa chao kuwa na mamlaka ya kuunda serikali yao itakayokuwa sehemu ya Jamhuri ya Muungano.

Hali hiyo ilisababisha suala lao liunganishwe na wazee saba waliokamatwa awali na polisi na kushikiliwa kwa siku kadhaa, wakihusishwa na tukio la kupeleka barua hiyo katika ofisi za Umoja wa Mataifa jijini Dar es Salaam.

Wawakilishi hao waliwakariri polisi wakidai kwamba, majina yao yalitajwa na wazee hao saba.

Hata hivyo, wabunge wawili, ambao nao walipewa barua ya wito wakitakiwa kufika katika mahojiano hayo, hawakutokea makao makuu ya polisi.

Wabunge hao ni wa Mtambile, Masoud Abdallah na Mbunge wa Chambani, Salim Khamis.

"Sisi hatujui kwa nini hawajaja lakini tunachojua ni kuwa leo kikao cha Bunge kimeanza, sasa labda wapo huko kwa hivyo sijui kama watawahoji huko huko au watalazimika kuja huku, lakini wote wawili wamepewa barua kama zetu," alisema Mbarouk.

Hata hivyo, akizungumza na gazeti hili kwa simu kutoka Dodoma anakohudhuria vikao vya Bunge la Bajeti, Salim Khamis alikiri kutokwenda katika mahojiano hayo pamoja na mwenzake.

Alisema kuwa wameshindwa kwenda kwa sababu wao hawajapokea barua hizo za wito kutoka Jeshi la Polisi.

Kutoka Dar es Salaam, Amana Nyembo anaripoti kuwa, wazee kutoka Kisiwa cha Pemba wanaodai kuundwa kwa serikali ya kisiwa chao, wameonekana kutokuwa na hofu na udhibiti wa serikali na wameamua kuendelea na madai hayo.

Katika kuhakikisha kuwa madai yao yanasikilizwa, wawakilishi wa wazee hao juzi walirejea tena katika ofisi za Umoja wa Mataifa jijini Dar es Salaam, kuulizia hatima ya maombi yao waliyoyapeleka siku kadhaa zilizopita na kusababisha wakamatwe na kuhojiwa na Jeshi la Polisi.

Kwa kuonyesha kuwa suala hilo linaungwa mkono na watu wengi, mmoja wa wazee hao, juzi alisikika akiliambia Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) kuwa idadi ya watu waliojiunga katika madai hayo inaweza kufikia zaidi ya 100,000.

Madai ya kikundi hicho cha Wapemba yanajikita kuwa, kisiwa hicho kinatengwa kimaendeleo na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kutokana na chuki za kisiasa kutokana na watu wengi kisiwani humo kukiunga mkono Chama cha Wananchi (CUF).

Pia malalamiko ya wazee hao yanahusisha kupuuzwa, kudharauriwa na kubaguliwa kwa wakazi wa kisiwa hicho, hivyo kujenga hoja ya kutaka kuundwa kwa serikali yao.

Malalamiko hayo ambayo waliyapeleka mwezi mmoja uliopita kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban-ki Moon, kupitia ofisi za Dar es Salaam, bado hayajajibiwa.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, msemaji wa wazee hao, Hamadi Mussa, alisema walipofika katika ofisi za UN, walimkuta mwakilishi wa balozi wa UNDP, aliyemtaja kwa jina la Robert.

"Robert alitupokea na kutueleza turudi baada ya wiki moja… lakini tutakaporudi tutakwenda na sahihi za watu 50,000 zaidi wanaotuunga mkono, tena wengine ni wanachama wa CCM.

"Sisi tunafuata taratibu na kanuni ya ibara ya nane inayohusu madaraka na mamlaka ya serikali… hii ni kwa sababu serikali haiwajibiki kwetu, sisi wananchi hasa Wapemba. Rais wa Zanzibar anatukebehi.

"Eti Rais wa Zanzibar anasema sisi hatustahiki kupewa ajira, kwa madai kuwa hatukumpa kura wakati wa uchaguzi na matokeo yake nafasi za ajira wanapewa vijana wanaotoka Tanzania Bara wasiokuwa na ndugu Zanzibar na wazawa ambao ni wazalendo hawapewi ajira," alisema Musa.

Mzee huyo alitahadharisha kuwa hali inaweza kuwa mbaya visiwani na hivyo akaishauri UN kuchukua hatua mapema kabla mambo hayajaharibika.

Musa alisema hawawezi kukaa kimya na kubaki wanaota ndoto za maendeleo wakati nchi inaendeshwa ovyo na viongozi wanasahau kwamba Wapemba na watu wa Mombasa ndio waliowafukuza Wareno na kusema Wapemba ni watu wa kipekee na wana haki ya kuheshimiwa.
 
Back
Top Bottom