China na nchi za Afrika zimekuwa na urafiki wa jadi ambao umedumu kwa miongo mingi. Urafiki huu unagusa sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya utamaduni.
Hivi karibuni, onyesho lililopewa jina la “Masikilizano ya Ngoma na Muziki” lilifanyika Dakar, mji mkuu wa Senegal, ambapo wapiga ngoma kutoka China na wale wa Senegal walivutia kwa mdundo wao na ufundi unaoendana, na hivyo kuleta pumzi mpya katika midundo ya ngoma wakati wa tamasha hilo la kuvuka mpaka wa kitamaduni.
Onyesho hilo lililofanyika katika Jumba Kuu la Kitaifa la Doudou Ndiaye Coumba Rose hivi karibuni, lilivutia karibu watazamaji 1,000, ambao walikuwa na shauku ya kushuhudia uratibu wa kuvutia kati ya wasanii wa China na wale wa Senegal.
Profesa mshiriki kutoka Chuo cha Muziki cha China Yin Fei anasema, tukio hilo ni zaidi ya onyesho, na kulitaja kuwa ni mabadilishano ya kiroho. Profesa Yin aliongoza kundi la wajumbe tisa la wapiga ngoma kwenye ziara ya kitamaduni nchini Senegal, ambako walifanya uratibu wa moja kwa moja na kundi maarufu la ngoma la Senegal linaloitwa Doudou Ndiaye Rose.
Kutoka dansi ya Simba ya China mpaka ngoma ya sabar ya Senegal, makundi hayo mawili, kila moja likiwa na umaalum wake, walipata mwafaka katika mdundo na moyo, na kuonyesha umoja wa mdundo wa ngoma kama lugha ya pamoja ya kitamaduni.
Katika ufunguzi wa tamasha hilo, kundi la ngoma la Doudou Ndiaye Rose lilionyesha umaarufu wa ngoma ya sabar. Wachensa dansi hao ambao walivalia mavazi ya jadi ya Kisenegal, walicheza sambamba na mdundo wa ngoma, na kusimulia hadithi ya urithi wa Senegal na jamii kupitia ngoma na uchezaji wao.
Baada ya tumbuizo hilo, kundi la Chuo cha Muziki cha China lilipanda kwenye jukwaa na kuwasilisha mfululizo wa ngoma za Kichina zenye umaalum wa kitaifa, na kuamsha urithi mkubwa wa kitamaduni wa ustaarabu wa China kupitia midundo yake.
Ngoma ya Sabar, ambayo ni alama ya utamaduni wa ngoma wa Afrika, ni majadiliano kati ya wapiga ngoma na wachezaji. Mpiga ngoma anabadili mdundo kutokana na mwendendo wa mchezaji, huku mchezaji anajibu mwendo wa ngoma.
Kwa Mustapha Ndiaye, mkuu wa Kundi la Ngoma la Doudou Ndiaye Rose, onyesho hilo liligusa sana hisia zake, na lilikuwa kama heshima kwa marehemu baba yake, Doudou Ndiaye Rose, ambaye alitambulisha ngoma ya jadi ya Wolof. Ngoma hii mwanzo ilikuwa ikichezwa katika harusi na matamasha ya huko, lakini sasa imeingia katika anga ya kimataifa.
Ndiaye anasema, mabadilishano hayo ni fursa kubwa ya kuingiza uhai mpya kwa wasanii, kwani kwa kupitia ngoma, hadithi nyingi zinasimuliwa. Anaielezea ngoma kwamba ni zaidi ya kifaa cha muziki, na kuiita ni chombo cha kitamaduni na moyo halisi. Ameeleza matarajio yake kwamba, iko siku anatumai kupeleka utamaduni wa ngoma ya Senegal nchini China.