WARAKA WA CHACHA WANGWE.
UTANGULIZI.
Jumamosi, June 28 mwaka huu wajumbe
kadhaa wa Kamati Kuu ya CHADEMA walidai
kuwa wamesitisha Umakau Mwenyekiti wangu
katika kikao kilichofanyika mjini Dodoma siku
hiyo. Kesho yake Mwenyekiti wa CHADEMA
Taifa, Mhe. FREEMAN MBOWE akaitisha
mkutano wa waandishi wa habari na kutaja
sababu za kunisimamisha uongozi.
Inatosha tu kusema kuwa sababu zote alizotoa
ni za uzushi kama ile inayodai kuwa mimi
navujisha siri za chama kwa viongozi wa CCM
bila hata kutaja siri hizo, au kusema nimezitoa
lini, wapi, na kwa kiongozi yupi?Kikao hicho
kinachosemekana kunisimamisha uongozi,
kilikuwa na wajumbe 31 ambao takribani nusu
hawakuwa na uhalali wa kupiga kura kinyume
cha katiba na kanuni za CHADEMA kwa vile
walikuwa wameandaliwa kwa kazi hiyo.
Wajumbe 7 walikataa kushiriki njama hizo.
Kufuatia jaribio hilo la kunivua uongozi
kutokubalika kwa wanachama walio wengi wa
CHADEMA , Mwenyekiti MBOWE na wafuasi
wake wameendelea kuhaha kwa kuongeza
sababu nyingine mbalimbali ili kuhalalisha
njama zao. Sasa hivi wameingia hatua ya
kuwashawishi wanachama wa Tarime eti
wanifukuze uanachama.Kwa kuzingatia katiba,
kanuni na taratibu za CHADEMA, nilichokifanya
mimi baada ya kubaini njama zao ni kukata
rufaa kwa Baraza Kuu la Chama, kupinga
upotoshaji unaofanywa chini ya uongozi wa
Mhe. MBOWE anayeonekana kutaka kuendesha
chama kinyume na matarajio ya wanachama
walio wengi.Hivyo basi zipo habari za uhakika
kuwa kikao hicho cha Baraza Kuu
hakitaitishwa ama kabisa, au kitacheleweshwa
kwa makusudi, kwa visingizio mbalimbali
ikiwemo kutokuwa na fedha za kukidhi
gharama za kikao hicho.
Naomba nikiri kuwa ninakerwa sana na
mtiririko mzima wa sakata hili linalozua
mgogoro unaokiyumbisha chama. Ukweli ni
kwamba mimi niligombea Umakamu
Mwenyekiti nikiwa na agenda ya kufufua uhai
wa chama kwa kukaripia vitendo visivyostahili
katika kuendesha chama. Agenda yangu
haijabadilika. Yote niliyoyasema wakati
nagombea nafasi hii yanafahamika kwa wana
CHADEMA wote.
Walikuwepo walioyalalamikia na walikuwepo
walioyapongeza matamshi yangu hayo.Mwisho
wa yote wana CHADEMA waliridhika kuwa
ajenda yangu ilikuwa sahihi na hivyo
wakanichagua kuwa Makamu Mwenyekiti.
Hivyo basi hata kama ni kweli kuwa ulikuwepo
mvutano wakati wa kampeni ile, lakini hilo ni
jambo la kawaida katika uchaguzi. Nijuavyo
mimi hayo yalitakiwa yawe si ndwele nasi
tugange yajayo kwani wanachama walikwisha
fanya uamuzi halali kupitia kura zao.
Baada ya kuingia kwenye wadhifa wa Makamu
Mwenyekiti Taifa, nilifanikiwa kuzungumza na
Mhe. MBOWE kuhusu mambo, hususan yale,
niliyoyapigania wakati wa kinyang?anyiro kile
na kumuomba tukae chini na kutafuta jinsi ya
kufanikisha azma hiyo.Ni imani yangu kuwa
waraka huu utawasaidia wanaCHADEMA
wenzangu na watanzania wote kwa ujumla,
kuelewa vizuri ukweli wa mambo
niliyoyapigania kabla ya kuwa Makamu
Mwenyekiti, na ninayoendelea kuyasimamia
hivi sasa nikiwa Makamu Mwenyekiti, na
inshallah nitakayoyatekeleza baadae kama
Taifa Mwenyekiti wa CHADEMA.
Kimsingi mambo tunayotofautiana na Mhe.
MBOWE ni haya yafuatayo:-
MATUMIZI YA RUZUKU
CHADEMA hupata ruzuku ya Tshs. 66,000,000
kwa mwezi (Milioni sitini na sita). Mimi
nasema si haba hasa tukizingatia chama
kilikotoka. Naamini kuwa kiasi hiki cha fedha
kikisimamiwa vizuri kinaweza kukirahisishia
chama kujieneza katika ngazi zote toka Tawi,
Wilaya, Mkoa na Taifa.
Si kweli kwamba matatizo yote yatamalizwa na
fedha hizi lakini basi hata ofisi za chama
zinaweza kuwa hai nchi nzima kitu ambacho
kwa sasa hakipo. Mahesabu yanaonesha kuwa
mtaji wa laki moja (Tshs.100,000/=) kwa
wilaya moja nchini inatosha, hivyo kwa Wilaya
126 kwa mwezi jumla yake ni Tshs. milioni 12
(Tshs. 12,600,000/= ) zinahitajika ( Wilaya 126
x 100,000 kila wilaya = 12,000,000/=)Hata
tukisema tupeleke kiasi hicho kwa kila jimbo la
uchaguzi jumla yake ni Tshs. Milioni 23 (Tshs.
23,000,000/=) kwa maana ya majimbo 213 x
100,000 = 23,000,000/=.
Mhe. MBOWE anasema hizo ni pesa nyingi
sana kwa uimarishaji wa chama. Mimi nasema
hapana, kiwango hiki kwa kila Wilaya au
Jimbo la uchaguzi ni muafaka kwani haba na
haba hujaza kibaba.Chini ya uongozi wa Mhe.
MBOWE na wafuasi wake hawastaajabu kuwa
kati ya Tshs. 374,144,000.40 zilizopatikana
kama ruzuku katika ya Januari 1 na Juni, 30,
2008, Tshs. 350,000,000/= zilitumika Makao
Makuu ya CHADEMA na Tshs. 25,000,000/= tu
ndizo zilikwenda Wilayani kuimarisha
chama.Mimi naona mgao huu unayatukuza
Makao Makuu ya
CHADEMA isivyostahili wakati huo huo
ukidhalilisha chama nchi nzima.
MADENI YA UCHAGUZI
Kufuatia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005, Mhe.
MBOWE alitufahamisha wanachama kuwa
alikuwa anakidai chama US $ 181,949.00 sawa
na Tshs. 218,338,546. Mpaka sasa chama
kimekwisha mlipa Tshs. 175,000,000/=Baada
ya kupata wadhifa wa Makamu Mwenyekiti, na
kwa kuzingatia takwimu zionekanazo hapo juu
katika kulinganisha matumizi ya fedha
Wilayani na Makao Makuu niliamua kumshauri
MBOWE asitishe kujilipa deni kutokana na
fedha za ruzuku kwani siamini kuwa kulipa
madeni yaliyopita kunaendana na utaratibu wa
usimamizi wa fedha za ruzuku kwa vyama vya
siasa toka serikalini.
Mhe. MBOWE alichachamaa na ndipo
nilipomshauri kuwa kama ni hivyo basi
atuthibishie pesa hizo anazodai alikikopesha
chama ziliingia kwenye akaunti gani ya
CHADEMA, kupitia hundi ipi, na lini?
Nilimuomba pia kutaja ni kikao gani cha
chama kiliidhinisha matumizi ya fedha hizo
kwani kama hakuna ushahidi wa maidhinisho,
ni dhahiri kuwa matumizi hayo hayakudhibitiwa
na chama na kwa mantiki hiyo kuyafanya kuwa
matumizi binafsi ya Mhe. MBOWE.Vilevile,
nilimueleza kuwa matumizi ya fedha hizo
alizodai alikikopesha chama yalikuwa yakinuka
harufu ya UFISADI.
Stakabadhi zote kuhusiana na matumizi hayo
zilionesha kuwa gharama za aidha ununuzi
na / au ukodishaji wa vifaa hivyo,
hazikutofautiana na viwango wanavyolipishwa
watalii kwa huduma kama hizo, kwa maana ya
gharama ya juu sana.Na kwa kuwa hata baada
ya kuwa Mhe. MBOWE amekwisha lipwa zaidi
ya nusu ya deni alilodai kuikopehsa CHADEMA,
vifaa vyote yakiwemo magari, vipaza sauti na
kadhalika vimebakia kuwa mali yake binafsi,
basi bila kumficha nilimueleza kuwa huko ni
kukinyonya chama kwa kukigeuza kitega
uchumi cha watu binafsi.Kuhusu suala la kulipa
madeni kupitia ruzuku ya serikali, nilimuomba
Mhe. MBOWE afuatilie kwa Msajili wa Vyama
vya siasa ili tupate ufafanuzi kama kweli fedha
za ruzuku ya serikali kwa vyama vya siasa,
inaweza kutumika kulipia madeni ya viongozi
wa vyama hivyo yatokanayo na uchaguzi ili
CHADEMA isiathirike kisheria.
Niseme kweli hapa kwamba, kwa vile
wanaCHADEMA wengi walinichagua kuwa
Makamu Mwenyekiti, na hata mimi mwenyewe
tulikuwa wagombea wa nafasi za ubunge,
udiwani n.k katika uchaguzi wa mwaka 2005
ningefarijika sana iwapo na sisi tungerejeshewa
angalau chochote cha kufidia gharama zetu,
kwa maana kwamba kama chama kimeamua
kurudisha gharama hizo kiwalipe wote badala
ya kulipa madeni kwa wateule wachache.
UTEUZI WA WABUNGE WA VITI MAALUM
Naamini ukweli wa suala hili hauna mjadala.
Kwamba Mhe. MBOWE na wafuasi wake
walighushi orodha ya majina ya viti Maalum
badala ya kupeleka yaliyopendekezwa na
Kamati Kuu sio siri.
Naamini hata Mhe. MBOWE anakubaliana nami
kuwa suala hili si moja ya siri anazodai
nimevujisha! Yamesemwa mengi juu ya
mtafaruku uliojitokeza kuhusu viti maalum
hadi baadhi ya waasisi wa chama wakataka
kujitoa na hivyo kumlazimisha Mwenyekiti
Taifa ( FREEMN MBOWE) na Katibu Mkuu (DR
WILBROAD SLAA) kukiomba radhi kikao cha
Kamati Kuu ya CHADEMA kwa kukiuka katiba,
kanuni na maadili ya chama katika suala hili
la kugushi viti maalum.
Ni ukweli ulio wazi kuwa kitendo hicho cha
upendeleo bado kina iumiza taswira ya
CHADEMA. Chama kinaonekana kuendekeza
ujanja ujanja kiasi kwamba watu na binti zao,
wakwe zao, shemeji zao, waume wenzao,
wachumba wa shemeji zao, wake wenza na kwa
kiwango kikubwa watu wa kabila moja ndiyo
wamekuwa sura ya CHADEMA bungeni.Katika
hili nilichoweza kumueleza Mhe. MBOWE ni
kuwa chaguzi mbalimbali tangu za Mitaa,
Ubunge na Urais zinakaribia ni vizuri tufanye
bidii kusambaza nguvu zetu nchi nzima tuwe
na mtaji wa kura maeneo mengi ili kashfa
kama hii isijirudie. Hii ni kwa msingi kuwa
chama kikijitanua kutakuwa hakuna sababu ya
kuwaona watu wa eneo fulani tu kuwa ndiyo
mhimili wa CHADEMA na hivyo zikitokea fursa
itakuwa rahisi chama kuwakilishwa na
mtandao wake mpana badala ya koo au kabila
fulani.Sasa kwa kuwa kuimarisha chama
kitaifa maana yake ni matumizi ya fedha, nalo
hili likawa nongwa ingawa kwa mtazamo wa
Makao Makuu kulipa madeni kwa wateule
wachache si nongwa.
Cha ajabu ni kwamba Mhe. MBOWE hakukana
kuwa hili la viti maalum na hata upangaji wa
ajira kwa ukabila una leta athari mbaya kwa
mustakabali wa CHADEMA
Katika maongezi yangu nae nilikuwa wazi
nilipotahadharisha kuwa:
1. Watanzania wakiendelea kuona kwamba
CHADEMA inaendeshwa kwa misingi ya
kikabila hawatajiunga na chama chetu na
tutakosa wafuasi.
2. Watanzania wakiona kuwa sisi tumeweka
mbele ukabila kuliko utaifa hawatatupa
madaraka na kutawala kwa kuhofia yale
yanayotokea nchi jirani kama Rwanda, Burundi,
Kenya na kadhalika ambako nafasi za raia
wote zimehodhiwa na kabila moja na hatma
yake watu wamechinjana kama kuku kwa
kupinga hilo.
Pia nilimwambia kwamba, kwa jinsi sura ya
uteuzi wa Wakurugenzi na watendaji wengine
wa Makao Makuu inavyoonekana, sasa tayari
chama chetu kimebatizwa jina la CHAMA CHA
WACHAGA, na hii si kuwatendea haki raia
wengine na makabila yao ambao wataonekana
kama punguani kujihusisha na chama na
ukabila.Yote haya ninayosema kuhusu ukabila,
upendeleo na kadhalika sio dhana tu. Kufuatia
malalamiko mengi yaliyokuwa yakisikika nchi
nzima kuhusu masuala haya, Kamati Kuu ya
CHADEMA ilikwisha unda Tume kutafuta ukweli
wa mambo hayo. Tume hiyo ya watu watano
iliongozwa na Mhe. Merky Lugendo Mziray
ambaye ni mjumbe wa Kamati Kuu ya
CHADEMA nayo imekwisha toa taarifa yake
kwamba Makao Makuu ya CHADEMA
yanatawaliwa na ubaguzi wa kikabila, kidini na
kielimu.
UTENDAJI WA KIBABE
CHADEMA ni chama kilicho njia panda kwa
sasa kutokana na utendaji wa kibabe wa Mhe.
MBOWE. Ninafahamu jinsi vyama vingine vya
upinzani hapa nchini kama vile NCCR ?
Mageuzi vilivyoporomoka haraka haraka mithili
ya nyumba ya mabua. Chama NCCR ? Mageuzi
kilifikia mahali pazuri tu hadi watu wakaanza
kufikiria kuwa kingekuwa chama mbadala kwa
CCM.
kwa bahati mbaya uchu wa madaraka, ulafi wa
ruzuku, na tabia za kimangimeza kwa pamoja
vikakiathiri hadi kupoteza umaarufu wake.Na
hata vyama vingine vya upinzani vina dalili
hizo hizo japo kwa viwango vinavyotofautiana.
Ila badala ya kujichunguza na kujua kasoro
zetu, kila siku vyama vyetu, vimekuwa vikidai
kuwa ni chama tawala ndicho kinachoviroga,
kama ambavyo Mhe. MBOWE ameanza
kuweweseka kupitia vyombo vya
habari.Napenda kuthibitisha kuwa katika
mgogoro unaopaliliwa sasa na Mhe. MBOWE
ndani ya CHADEMA kutokana na ufisadi,
ufuska, ulevi wa madaraka na umangimeza
chanzo chake ni tabia yake ya kuendesha
chama kibabe. Mathalan kumzuia Martin
Mung?ong?o Mkurugenzi aliyechaguliwa kwa
kura kutofanya kazi zake ndani ya chama,
madai ya kupigana na watendaji wa chama
ndani ya baa na vitendo vingine vya aina hiyo
ni ushahidi tosha wa hulka hii.
Hadi sasa Mhe. MBOWE amefanikiwa kukizuia
chama hiki kisifanye kazi ya siasa mkoa wa
Dar es salaam kwa miaka minne.Ninavyoongea
hivi sasa CHADEMA imekuwa ikikimbia vikao
vya Democratic Union of Afrika (DUA),
Muungano wa Vyama Vya Upinzani,
uliofanikisha CHADEMA kujuana na
Conservative Party ya Uingereza na Republican
ya Marekani. Vyama dada hivi vyote
vinaulalamikia uongozi wa CHADEMA kwa
kufuja fedha ya misaada na kuwasilisha kwao
risiti za kugushi, kama ilivyofanyiwa
Conservative Party baada ya kutoa msaada wa
Tshs. 78,000,000 kwa ajili ya ununuzi wa
baiskeli na pikipiki ambazo
hazikununuliwa.Katika mkutano wa Kamati Kuu
ya CHADEMA huko Dodoma hivi majuzi tu,
Mhe. MBOWE kwa kauli yake aliwatisha
wajumbe kuwa alikuwa amethibiti uwezekano
wowote wa wajumbe kujisikia huru kwa kutoa
mawazo ambayo yangepingana na ajenda yake
aliyoitoa ghafla kikaoni kunisimamisha
Umakamu Mwenyekiti.
Mhe. MBOWE Alikifahamisha kikao kuwa alitoa
taarifa kwa IGP, SAID MWEMA kuwa kuna
wahuni ambao walitaka kuuchafua mkutano
wake, naye IGP akahakikisha kuwa mkutano
ule unalindwa kwa kiwango cha kushtua kama
ambavyo hata vyombo vya habari
vimethibitisha.Hayo ni baadhi tu ya mambo
yanayobainisha Mhe. MBOWE ni kiongozi wa
aina gani.
HITIMISHO
Kama nilivyokwisha sema hapo awali, sijaacha
na sintoacha ajenda yangu ya kufufua uhai wa
CHADEMA kwani ndiyo ahadi iliyofanikisha
kuchaguliwa kwangu kuwa Makamu Mwenyekiti
Taifa. Nilipopata wadhifa huo nilianza
kuitekeleza ajenda hiyo kupitia mahojiano na
Mwenyekiti MBOWE kuhusu matumizi ya
ruzuku, madeni ya uchaguzi, uteuzi wa
wabunge wa viti maalum, nafasi za ajira
Makao Makuu, na kuhusu mwenendo wa chama
Mkoa wa Dar es salaam.
Nilijikuta katika mvutano mkubwa kila
nilipogusa eneo lolote katika haya. Nakiri kuwa
kwa kiwango kikubwa sikuwa na uwezo wa
kubadili mambo hayo yaliyokuwa yakiratibiwa
kwa ukaribu na Mhe. MBOWE na wafuasi wake
kwani sikupewa ushirikiano wa aina yoyote na
chama pale Makao Makuu.
Ni vigumu kuamini, lakini ni kweli kuwa
sikuwa na ofisi Makao Makuu, sikupewa
vitendea kazi kama magari, vipaza sauti na/au
vyombo vya habari, na sikuwahi kupata taarifa
yoyote ya kiutendaji toka Makao Makuu.Kwa
kuzingatia yote hayo, naomba nichukue fursa
hii kuwashukuru kwa dhati wanachama wa
CHADEMA mkoa wa Dar es salaam ambao kwa
pamoja tulisimama kidete kufufua uhai wa
chama hapa jijini. Niseme tu ushirikiano wao
wa hali na mali uliniwezesha kushughulikia
masuala muhimu ya kitaifa na kimataifa.
Rai yangu kwa wana CHADEMA na wale wote
wanaokitakia mema chama chetu na nchi yetu
kwa ujumla ni kwamba kazi ya kupigania
demokrasia ya kweli ndani na nje ya chama,
kukiepusha chama na vitendo vya ukabila,
migogoro, ubadhirifu, umangimeza, ufisadi na
ubaguzi wa aina yoyote bado inaendelea na
nawaombeni mniunge mkono kwa hali na mali
katika vita hii. Naamini tutashinda.Mungu
Ibariki CHADEMA Mungu Ibariki TANZANIA
Mungu Ibariki AFRIKA