Serikali: Hatumchunguzi Warioba
Exuper Kachenje
SERIKALI imesema haina taarifa za kuchunguzwa na mpango wa kufikishwa mahakamani kwa waziri mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba na kwamba wala haihusika na suala hilo.
Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe alisema hayo jana alipokuwa akijibu maswali ya waandishi wa habari katika mkutano maalum aliouitisha kuelezea mafanikio ya wizara yake katika miaka mitatu ya serikali ya awamu ya nne.
Warioba amekuwa akibashiriwa na vyombo vya habari kuwa angefikishwa mahakamani kuhusu kampuni ya Mwananchi Gold ambayo inahusishwa na usafidi na ubashiri ulipozidi, kiongozi huyo wa zamani aliitisha mkutano na waandishi wa habari na kufafanua kuhusu kampuni hiyo.
Warioba alisema alilazimika kuzungumzia suala hilo baada ya kuona uvumi unazidi kukomaa huku hadhi yake kwenye jamii ikitetereka, lakini Waziri Chikawe aliripotiwa baadaye akihoji sababu za waziri huyo mkuu wa zamani kuwa na wasiwasi kama anajiona hana hatia.
Jana, Waziri Chikawe alisema: "Sijui lolote kuhusu tuhuma za Jaji Warioba. Wizara yangu haijatamka wala haijamtuma mtu ama taasisi yoyote kumchunguza au kumtisha wala haihusiki na upelelezi.
"Kwa sasa mimi sina taarifa kuhusu hilo na kwanza ofisini kwangu hatuna utaratibu wa kutisha watu."
Alisema kuwa anamfahamu na kumheshimu Jaji Warioba kwa kuwa ndiye alimpokea na kufundisha kazi alipojiunga na Wizara ya Sheria mwaka 1975, wakati huo Warioba alikuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Alisema kuwa hajawahi kumkejeli Jaji Warioba na kwamba hiyo si tabia yake maishani akisisitiza kuwa hajawahi kumkejeli mtu, kama ilivyoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari mapema wiki hiii.
Waziri Chikawe alisema kuwa taarifa zinazomhusu yeye kuzungumzia Jaji Warioba zilizoandikwa na gazeti moja la kila siku (si Mwananchi) kuwa si za kweni na zimejaa ushabiki.
Hata hivyo, alisema si jukumu lake kumchunguza mtu bali vipo vyombo vinavyohusika, ambavyo vinastahili kuulizwa kuhusu suala la Jaji Warioba kuchunguzwa, na kwamba iwapo vitafanya hivyo Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), ndiye mwenye mamlaka ya kuamua kumfikisha mtu mahakamani ikiwa ataridhishwa na ushahidi alionao.
Wakati huohuo, Waziri Chikawe amesema serikali itatoa taarifa kuhusu ufumbuzi wa suala la kuwepo au kutokuwepo kwa Kadhi Mkuu hivi karibuni.
"Kuhusu suala la kuwepo au kutokuwepo Kadhi Mkuu, utafiti tayari umefanyika na umekabidhiwa serikalini. Serikali itatoa taarifa yake punde," alisema Chikawe katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana.
Alisema hatua hiyo itatoa ufumbuzi kuhusu suala hilo lililogonga vichwa vya viongozi wa serikali, kisiasa na kidini huku Waislamu wakidai kuwepo kwa Kadhi Mkuu ni haki yao ya msingi kiimani.
Chikawe alisema kuwa mbali na suala hilo serikali ipo katika mchakato wa kutoa waraka wa serikali namba moja kuhusu marekebisho ya Sheria ya Ndoa na Sheria ya Mirathi na kwamba wizara yake imekuwa ikifanya kazi kutekeleza matamko ya ilani ya Chama Cha mapinduzi katika sekta ya sheria.
Alisema Sheria ya Ndoa, Sheria ya Mirathi na Urithi na Sheria ya Makosa ya Kujamiiana zimefanyiwa utafiti na kujadiliwa katika katika ngazi mbalimbali za kijamii na kiserikali.
Alisema ni jukumu la wizara yake kuhakikisha mfumo wa sheria uliopo unatoa fursa na haki sawa kwa raia wote mbele ya sheria na kwamba mfumo huo unatakiwa kuweka mazingira muafaka kwa taasisi zote za umma na za kiraia kuziwezesha kutekeleza majukumu yao.
Sheria nyingine zilizofanyiwa utafiti ni pamoja na Sheria ya Ulinzi wa Haki za Watu Wenye Ulemavu, Sheria ya Haki ya Ushindani wa Kibiashara, Sheria ya Usimamizi wa Haki za Ugunduzi na Uhamishaji wa Teknolijia na Sheria ya Kusimamia Matumizi ya Teknolojia ya Chembe za Asili za Urithi (DNA).
Source:
Mwananchi Read News