JAMES Mbowe, aliyekuwa mgombea ubunge katika jimbo la Hai kwa tiketi ya Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), achutama, ajutia uamuzi wake wa kukihama Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), sasa aomba radhi.
Kupitia mitandao ya kijamii leo tarehe 8 Januari 2026, Mbowe amesema anatambua kuwa hatua yake imewaumiza wengi, hasa waliomlea kisiasa ndani ya Chadema, na hivyo kutumia nafasi hiyo kuomba radhi hadharani.
Mbowe amesema kuwa Chadema ni chama chenye nafasi ya kipekee katika maisha yake ya kisiasa na kwamba anaendelea kukiheshimu licha ya kuondoka kwake.
Licha ya kukiri kuwa anajutia uamuzi huo lakini haukuwa wa pupa na kuahidi kuwa ipo siku ataweka wazi sababu zilizopelekea yeye kuachana na Chadema na kujiunga na Chaumma.
Mbowe alijiunga rasmi na Chaumma tarehe 6 Agosti 2025, akiwa pamoja na kada mwenzake Yeriko Nyerere, katika makao makuu ya chama hicho yaliyopo Kinondoni, jijini Dar es Salaam.