NI dhahiri kuwa mpumbavu mmoja angejitokeza kujibu makala iliyochapishwa kwenye ukurasa huu wa gazeti hili wiki iliyopita, makala ambayo ililenga kumshutumu Rais Jakaya Kikwete kuwa amekuwa anatumikia udini katika kufanya uamuzi wa kuteua watu kushika nyadhifa mbalimbali katika utawala wake mpya, mpumbavu huyo ni mimi ambaye jina langu linaonekana mwanzoni mwa makala hii.
Nianze kwa kusema kuwa, kwa sababu mbalimbali, sikushangazwa na makala hiyo. Kwanza, uvumi na minongono ya mitaani katika wiki na siku za karibuni imekuwa inatajataja sana suala hilo.
Kwa hiyo, na kwa sababu nyingi na uzoefu wa nchi hii, nilitarajia kuwa suala hilo, kwa namna moja au nyingine, lingeingia magazetini hata kama ingechukua muda.
Hilo lilikuwa lazima kabisa. Sina shaka kuwa kama taasisi za serikali zinafanya kazi vizuri, basi hata Rais Kikwete mwenyewe bila shaka atakuwa pia amejulishwa kuhusu minongono hiyo.
Huo ni mtandao wa kawaida wa jinsi kiongozi wa nchi anavyopewa na kufikishiwa taarifa, hata kama mwenyewe hataki kuzisikia taarifa hizo au hata kama hataki zimfikie.
Pili; niharakishe kusema kuwa ilikuwa lazima kwa kelele hizo za rais kutumia udini kuteua watu kujitokeza, kwa sababu ukweli ni kwamba Tanzania bado inacho kiwango cha kusumbua cha ukabila na udini, hata kama tunajificha chini ya kivuli cha unafiki ili kuficha uozo huo.
Bado wapo viongozi wa shughuli za umma ambao wanaongozwa na ukabila na udini katika uamuzi mbalimbali, ukiwamo wa ajira na kuendeleza watumishi wa taasisi za umma, za binafsi na hata za kidini. Huo ndiyo ukweli halisi wa nchi yetu, hata kama tunataka kujidanganya vinginevyo.
Ukweli kwamba kuna watu; kwa mfano, wanatunza orodha za nani anateuliwa na rais pamoja na dini zao na pengine makabila yao, ni ishara tosha ya jinsi ukabila na udini vinavyoendelea kutusumbua.
Kwa hakika, uteuzi unatakiwa kuwa jambo la rahisi kabisa, kwa sababu ni lazima ufanyike kwa misingi ya sifa, uwezo, uzoefu, ujuzi na ufanisi. Na ukweli kwamba pengine watu wanatumia udini au ukabila kuwanyima watu wengine ajira, au vyeo, wenyewe ni ukabila wa kutosha.
Hakuna shaka kuwa tumefanya vizuri katika kudhibiti mwenendo wa udini, ukabila, rangi ya mwili na ubaguzi mwingine wenye athari za hatari kwa Tanzania. Lakini bado ukabila na udini unabakia.
Kama nilivyosema awali, wapo watu chungu nzima wanaosukumwa na kuongozwa na udini na ukabila katika shughuli za umma, iwe katika ajira au manufaa mengine ya kitaifa, ukiwamo hata upatikanaji wa tenda.
Vinginevyo, tunaelezea vipi malalamiko na ukweli kuwa mashirika kama Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Wizara ya Fedha, au mashirika na wizara nyingine zina watu wa kabila moja? Na bado hakuna anayehoji hali hiyo kwa sababu tunaongozwa na unafiki tu.
Ukweli ni kwamba, pamoja na miaka yote ya kupambana na ukabila, udini na ubaguzi wa aina tofauti, ukiwamo wa rangi, bado tuna tatizo kubwa la mabalaa hayo. Mabalaa yote hayo yapo karibu sana na hisia zetu. Na ukijaribu kuhoji hali hiyo, utaambiwa wewe ni mkabila, mbaguzi wa rangi au mshiriki wa ubaguzi mwingine wowote.
Kiwango chochote cha kujidai kuwa hakuna ukabila wala udini katika Tanzania, hakitaondoa mabalaa hayo. Kujidai hakuna mabalaa hayo ni kuishi katika dunia ya mbuni, ya kuficha kichwa kwenye mchanga wakati kiwiliwili kilichobakia kiko wazi nje ya mchanga.
Tatu, sikushangazwa na madai hayo kwa sababu kila kiongozi mkuu wa nchi hii, kwa njia moja au nyingine, ameshutumiwa kuendesha nchi kwa misingi ya ukabila, udini, rangi ya mwili na ubaguzi mwingine miongoni mwa binadamu.
Julius Kambarage Nyerere, kiongozi wa kwanza wa nchi hii, alipata kushutumiwa kwa kuwapendelea Wakatoliki katika uteuzi wa nafasi za serikali. Alishangazwa mno na tuhuma hizo kiasi cha kwamba aliwaambia mawaziri katika mkutano wa Baraza la Mawaziri kuwa kabla ya shutuma hizo, alikuwa hajapata hata kuhangaika kuhesabu ni Wakatoliki wangapi alikuwa amewateua katika Baraza la Mawaziri.
Na wala hakuna shaka kwamba Mwalimu Nyerere ndiye kiongozi wa nchi hii ambaye alipambana kufa na kupona kupunguza makali ya udini, ukabila na ubaguzi mwingine. Kwa sababu bila Nyerere, baadhi ya makundi ya watu katika nchi hii wangeonewa sana.
Nne, sikushangazwa na shutuma hizo kwa sababu ya msimamo wa mwandishi mwenyewe wa makala hiyo. Huyu ni mtu ambaye amehama kutoka chama kimoja cha siasa za upinzani kwenda kingine kulingana na matakwa na maslahi yake. Kwa mtu kama huyo, shutuma za udini na ukabila ni mambo rahisi kuyatumia katika kufanikisha malengo ya kisiasa, hata kama ni ya muda mfupi; na yenye athari na hatari za kweli kweli huko tuendako.
Katika hali ya kubanwa mno ambamo wapinzani wa Serikali ya Jakaya Kikwete wamejikuta, baada ya kiongozi huyu wa Tanzania kupata ushindi mkubwa na wa kushangaza katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, unafanya nini kuipinga serikali?
Kwa sababu hakuna hoja yoyote ya msingi ya kupinga serikali kwa sasa, na kwa hakika hali ya sasa ni ya kuwahurumia wapinzani kweli kweli, unafanya nini kama si kupakazia matope kwa kutumia hoja za ubaguzi ambazo nchi hii imepingana nazo tangu uhuru wetu tuliopata 1961?
Kuna hoja gani kwa sasa ambayo wapinzani wanaweza kutumia kuushutumu utawala wa Rais JK zaidi ya ile dhaifu ya ubaguzi wa dini, hata kama ilikwishaelezwa wakati wa mchakato wa kugombea urais kuwa Kikwete ni Mwislamu wa Kijamii (social) kuliko kuwa Mwislamu wa Kiitikadi (ideological) na huo ndio ukweli wa mambo.
Ama kuna hoja gani rahisi ya kuvutia na kuchochea hisia za watu kama kutumia hoja ya ukabila, hata kama mwenyewe rais anatoka kwenye kikabila kidogo cha Wakwere ambacho hata kama angetaka na kudhamiria kweli kweli kukipendelea, hakuna watu wa kutosha, kwa msingi ya elimu na uwezo, kuweza kuteuliwa katika nafasi za uongozi wa umma?
Kwa hakika, udhaifu huo wa kikabila wa Kikwete ulikuwa moja ya nguvu za kumwezesha kuteuliwa kuwa mgombea urais kupitia CCM na hata kuchaguliwa, kwa wingi mkubwa mno wa kura, kuwa Rais wa Tanzania.
Hata hivyo, jambo ambalo lilinishangaza katika shutuma hizo, ni ukweli kuwa kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi hii, Wakristo sasa wanalalamikia kupendelewa kwa Waislamu katika uteuzi wa kushika nafasi za juu za uongozi.
Sikusudii kusema kuwa Wakristo hawajapata kulalamikia udini katika nchi hii.
Wamelalamika sana, kuhusu mihadhara ya Kiislamu, kuhusu matusi ya wahadhiri wa Kiislamu dhidi ya Ukristo, na tuwe wakweli, hasa wakati wa utawala wa Rais Ali Hassan Mwinyi.
Lakini kamwe, sisi Wakristo, mimi nikiwa miongoni mwao, hatujapata kulalamikia Waislamu kupatiwa nafasi kubwa za uongozi wa umma, kwa sababu ni sisi ambao siku zote tumenufaika na nafasi hizo.
Kuna wakati, hasa katika miaka 15 ya mwanzo ya uhuru wa nchi hii, nafasi zote kubwa katika uongozi wa serikali na umma, zilishikiliwa na Wakristo na tena kutoka makabila machache tu. Hali imebadilika kwa kadri Waislamu walivyozidi kupata elimu na watu wa makabila mengine zaidi kujiendeleza.
Kwamba sasa sisi tunalalamika, basi hili ni jambo jipya ambalo linahitaji kuelezwa zaidi na hasa kujibu swali kama kweli Kikwete anawapendeleza zaidi Waislamu katika uteuzi wa nafasi za uongozi wa umma.
Niongeze pia kuwa, sisi Wakristo tulikuwa hatulalamiki kwa sababu tulikuwa tunanufaika na kuneemeka. Na kwa sababu hali hiyo ilizoeleka kiasi cha kukubalika, sasa tunaona ni tatizo kwa Waislamu nao kuteuliwa kushika nafasi hizo. Ni hadithi ile ile ya changu changu, chao changu.
Nianze kwa kusema kuwa, mvutano wa kidini katika uteuzi wa nafasi za uongozi wa umma, ni mvutano wa kijinga na kipumbavu, lakini unaweza kuwa mvutano wa hatari kweli kweli na kusababisha zahma ambazo tumezishuhudia katika nchi nyingine duniani, zikiwamo za Kiafrika kama Ivory Coast, na nchi za maeneo mengine ya dunia, kama nchi iliyokuwa Yugoslavia ambayo sasa imemeguka vipande vipande.
Dalili zozote za kuwapo jitihada za kuupamba na kutumia udini katika uteuzi wa nafasi za madaraka ya umma, ni hatari. Na haziwezi kwa namna yoyote kukubalika au hata kusameheka. Lakini, sasa kauli hiyo inatuleta kwenye swali letu jingine ambalo ni; je, Rais Kikwete anatumia udini katika kuunda utawala wake?
Hata kabla sijaendelea, nataka kusema wazi wazi kuwa jibu la swali hilo ni hapana. Inawezekana vipi, kiongozi ambaye alipata zaidi ya asilimia 80 ya kura zote katika Uchaguzi Mkuu wa Desemba mwaka jana, ambaye alipata kiasi cha zaidi ya kura za Watanzania milioni tisa kati ya milioni 11 waliopiga kura, akatumia udini katika utawala wake?
Kwanza, hahitaji kutumia dhambi hiyo hatari, kwa sababu ni kiongozi ambaye alichaguliwa na kukubalika kwa watu wa dini zote.
Lakini pia, lazima iongezwe kuwa, kwa wale wanaomjua vizuri zaidi na mimi, lazima nikiri haraka haraka kuwa si mmoja wa watu hao waomjua vizuri sana, huyu ni kiongozi ambaye hatamani kwanza kuangalia pasi ya kusafiria ya mtu, kuona cheti chake za kubatizwa, rekodi yake ya kusilimishwa, cheti chake cha ndoa wala rekodi nyingine ya mtu yeyote, ili aweze kumteua mhusika kushika nafasi yoyote.
Tutaangalia rekodi yake ya uteuzi wa watu baadaye, lakini kama kweli kijana aliyelelewa chini ya utawala wa Mwalimu Nyerere, anaweza kusukumwa na ukabila, udini na madhambi mengine yoyote ya ubaguzi ukiwamo wa rangi, basi nchi hii iko katika hatari kubwa mno.
Na wale watakuwa ni watu wapumbavu kabisa ambao watatarajia kuwa rais atalazimika kwanza kusoma rekodi za maisha ya wateuliwa kwa maana ya dini, makabila, rangi zao za miili, kabla ya kufanya uteuzi wa watu mbalimbali kushika nafasi za umma.
Lakini vile vile, ni watu wajinga kabisa ambao wanatarajia Rais Kikwete ateue washika nafasi za umma kwa idadi ya sawa kwa sawa, kwa maana ya kwamba kwa kila mteuliwa Mkristo atateuliwa Mwislamu au kwa kila mteuliwa Mwislamu atateuliwa pia Mkristo.
Kwa mtu yeyote kuamini na kutarajia hali hii, ni kujidanganya na kujipumbazisha. Na wala hakuna kiongozi yeyote mwenye busara duniani anayefanya hivyo.
Katika uteuzi wake, hatutarajii kuwa Rais Kikwete atahangaika kuhakikisha kuwa, anateua idadi sawa ya Waislamu na Wakristo kushika nafasi za madaraka ya umma.
Kwanza, ukweli ambao ni mchungu kweli kweli, lakini hiyo ndiyo hali halisi, ni kwamba kama uteuzi wa kushika nafasi za umma unaongozwa na uwezo, ufanisi, elimu na uzoefu, ni dhahiri nafasi nyingi zitakwenda kwa Wakristo kwa sababu wao, kwa bahati nzuri au mbaya ya kihistoria, wamebahatika kupata elimu mapema kabla ya Waislamu na pengine kuliko Waislamu.
Huo ni ukweli wa historia ambao haukusababishwa na rika la sasa la Watanzania, na wa rika hili hawawezi kubeba lawama ya hali hiyo. Huu ni ukweli wa mpindo wa historia ambao si matakwa ya Kikwete wala Mtanzania mwingine yeyote. Hiyo ndiyo hali halisi.
Kwa sababu hiyo basi, hakuna mtu yeyote mwenye kufikiria sawasawa na kuitakia nchi hii mema, anaweza kudai kuwa ni wajibu wa Rais Kikwete, kama ambavyo haikuwa wajibu wa marais waliomtangulia, kuteua idadi sawa ya Waislamu na Wakristo katika nafasi za utumishi wa umma.
Kwa maama hiyo, hatuzungumzii uteuzi wa idadi sawa ya watumishi wa umma, bali tunazungumzia idadi linganifu (not equal but equitable numbers), ambako kila dini, kabila, rangi inapata haki yake ya kuteuliwa watu wake bila uonevu wala kubaguliwa kwa kadiri ya sifa za kazi ambazo wanateuliwa kuzishika.
Hivyo, kama kuna Mhaya ambaye ana sifa zaidi ya kazi ya utumishi wa umma kuliko Mkwere ambaye ameomba kazi hiyo, inatakiwa Mhaya huyo aipate kazi hiyo bila watu kutilia maanani kabila lake, dini yake au hata rangi yake ya mwili. Huu ndio msingi ambao nchi hii imeupigania hata kama hatujaufikia bado.
Naamini pia kwamba, inapokuwa lazima kabisa kwa rais kuangalia dini katika uteuzi wowote, hatasita kufanya hivyo, ilimradi mteuliwa awe na sifa za kuifanya kazi hiyo.
Hakuna anayetarajia kuwa kama rais angekuwa na madaraka ya kuteua Kadhi Mkuu wa Tanzania, angeteua Mkristo. Uteuzi huo ungekuwa ni matusi kiasi gani kwa Waislamu? Kwa bahati nzuri sana, rais, katika teuzi nyingi hachagui viongozi wa dini, bali viongozi wa shughuli za umma.
Shutuma dhidi ya Rais Kikwete katika makala ya wiki iliyopita, ilionekana kuchochewa na uteuzi wa karibuni wa kiongozi huyo wa viongozi wa Sekretarieti ya CCM ikiongozwa na Yusuf Makamba baada ya Kikwete mwenyewe kuwa ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa CCM, na kabla ya hapo uteuzi wake wa mabalozi wa nchi mbalimbali duniani.
Nakiri kuwa, katika uteuzi huo, walikuwapo Wakristo wawili tu katika timu nzima ya watu karibu 10 au zaidi. Je, huu ni udini? Jibu langu kwa swali hilo vile vile ni hapana.
Naamini ninayo matatizo kwa watu si zaidi ya wawili katika orodha ya watu hao walioteuliwa na Kikwete. Lakini matatizo yangu si kuhusu sifa zao. Hawa si watu walioteuliwa kwa sababu ya sifa za kuwa wamepata bahati nzuri au mbaya kuingizwa kwenye Uislamu na baba na babu zao, isipokuwa kwa sababu ya uwezo wao.
Kudai kuwa watu hao wameteuliwa na Kikwete kwa sababu ya Uislamu wao, ni matusi makubwa kwa wateuliwa hao na familia zao. Ni matusi yanayohitaji wateuliwa hao kuombwa radhi.
Kwa hakika ni matusi makubwa kwa mtu kuamini kuwa mwanasheria maarufu kama Mwanaidi Sinare Maajar, mtu mwenye sifa kubwa mno za uwakili na uanasheria nchini, anaweza kuwa ameteuliwa kwa sababu ya Uislamu wake.
Vivyo hivyo kwa Adadi Rajabu ambaye amepata kuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Omar Ramadhan Mapuri ambaye alipata kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Ahmed Rweyemamu Ngemera ambaye alipata kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Jumuia ya Afrika Mashariki au Juma Mwapachu ambaye ameshiriki sekta binafsi, ni msomi na amepata kuwa Balozi nchini Ufaransa.
Ni mtu gani asiyekuwa mnafiki na mkweli ambaye anaweza kuamini kuwa watu hawa wameteuliwa kwa sababu ya Uislamu wao? Tuambiwe ni sifa gani ambazo mabalozi Wakristo wanazo zaidi kuliko Waislamu walioteuliwa juzi kuwa mabalozi. Hawa ni wasomi waliobobea ambao wanazo sifa sawa au hata zaidi ya baadhi ya Wakristo ambao wanapiga kelele kuhusu uteuzi wao.
Kadhalika kwenye uteuzi wa Sekretarieti ya CCM. Nani asiyejua sifa za kisiasa za Makamba ambaye sasa amepewa kazi ya siasa ambayo naamini anaiweza zaidi kuliko ile ya ukuu wa mkoa ambayo inahitaji ujuzi na uzoefu zaidi ya kuendesha siasa tu?
Nani asiyejua ujuzi wa Rostam Aziz katika masuala ya uchumi? Unaweza vipi kumtilia shaka mchumi huyu kwa sababu tu ya jina lake kuelekea kwenye Uislamu? Kwa hakika, ni mtu asiyefanya utafiti wa kutosha ambaye atakuwa hajui kuwa Rostam si Mwislamu, bali mfuasi wa dini ya zamani mno ya Kiajemi iitwayo Zoroastrianism.
Zoroastrianism inakubalika kuwa moja ya dini za kale zaidi duniani na yenye asili yake miaka 5,000 iliyopita yenye kufananafanana na dini za kale za Kiafrika. Na kwa kweli unahitaji mchumi gani zaidi ya mtu mwenye sifa kama za Rostam kuendesha shughuli za fedha na uchumi za chama chako? Au mpaka aitwe Salvatory ndipo sifa zake zikamilike?
Naamini pia kuwa ni ukosefu huo huo wa utafiti na haraka haraka ya kushutumu ambavyo vilimsukuma mwandishi wa makala wiki iliyopita kudai kuwa Jaka Mwambi ni Mwislamu. Kasilimishwa msikiti gani huyo? Ama kaifanya shughuli hiyo kwa siri kubwa, kwa sababu ni kweli kwamba binadamu wanao uhuru wa kubadilisha dini zao wakitaka kwani dini ni sifa ambayo sote tunaikuta duniani ili ifungue njia yetu kwenda peponi.
Nani anayekataa dhana kuwa Kikwete ana haki ya kuteua watu ambao anaweza kufanya nao kazi kwa urahisi zaidi, kuliko kuteua watu ambao atavutana nao au wataanza hadithi ile ile ya kawaida ya Watanzania kuhalalisha uzembe kwa hadithi kibao na kuhujumiana?
Mwandishi wa makala ya wiki iliyopita, pia alionekana kukerwa na ukweli usiopingika kuwa, mabalozi wote walioteuliwa majuzi, wamepelekwa katika vituo muhimu na vikubwa kwa maana ya hadhi ya shughuli za kidiplomasia.
Nakubaliana na hoja hiyo kuwa vituo vya London (Uingereza), Paris (Ufaransa), Berlin (Ujerumani) ni vituo vikubwa kidiplomasia. Lakini hoja hiyo haiwezi kukamilika bila kwanza kuangalia vyeti vya ubatizo vya mabalozi wetu wa Washington (Marekani), Umoja wa Mataifa (New York), Ottawa (Canada), Pretoria (Afrika Kusini), Umoja wa Mataifa (Geneva), vituo vyenye ukubwa ule ule wa kidiplomasia kama vile ambako wanakwenda Maajar, Ngemera, Kibelloh na wengine.
Sikutaka kuingia kwenye takwimu, lakini ngoja tuangalie takwimu kidogo. Kwa sababu makala ya wiki iliyopita, ilitumia takwimu kujenga hoja, naomba na mimi nitoe takwimu chache kuhusu uteuzi wa Kikwete katika miezi saba iliyopita kuonyesha kuwa huyo si rais ambaye anaingia msikitini kuomba kwa Uislamu wake ili apate mwongozo wa kutosha wa kiroho kuweza kupata mawazo ya akina nani ni Waislamu ili awateue kushika nafasi za uongozi na madaraka ya umma:
Tunao mawaziri kamili 14 ambao ni Waislamu, na tunao mawaziri 15 ambao ni Wakristo, akiwamo Katibu Mkuu Kiongozi na Mkuu wa Utumishi Serikalini, Philemon Luhanjo. Rekodi zipo kuthibitisha takwimu hizo. Kuhusu manaibu waziri, tunao Waislamu 11 na Wakristo 20.
Kuhusu wakuu wa mikoa, tunao Waislamu wanane katika mikoa ya Arusha, Kigoma, Kilimanjaro, Lindi, Morogoro, Tabora na Tanga na Dar es Salaam ambako Yusuf Makamba alikuwa mkuu wa mkoa na sasa ameondoka, wengine 13 waliobakia ni Wakristo.
Kuhusu makatibu wakuu ni kwamba, makatibu wakuu kamili wa wizara 21 ni Wakristo kulinganisha na Waislamu saba tu. Kwa naibu makatibu wakuu, kuna Wakristo 11 na Waislamu watatu tu ambao ni Omar Chambo wa Wizara ya Miundombinu, Ramadhan Khijjah, mmoja wa naibu makatibu wakuu wawili wa Wizara ya Fedha na Mohammed Muya wa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika.
Lakini vile vile angalia uteuzi wake mwingine katika taasisi nyeti za ulinzi na usalama na hata uchumi. Chunguza uteuzi wake katika Jeshi la Polisi, na ni majuzi tu ambapo alimteua Luteni Jenerali Davis Mwamunyange kuwa Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Mwislamu.
Mkuu wa Usalama wa Taifa anabakia Mkristo. Na bado wakuu wa taasisi kubwa za uchumi kama vile Benki Kuu, TRA na nyingine nyingi tu wanabakia Wakristo. Sasa hoja iko wapi, kama si kuzusha tatizo ambalo halipo?
Madai ya upendeleo wa Waislamu ni utani wa kiwango cha juu, lakini vile vile wa hatari inayoweza kuzaa zahma yenye athari kubwa. Awali, niliposoma makala ile ya wiki iliyopita, nilidhani kuwa Mhariri wa gazeti hilo alikuwa anashiriki kuzusha hoja hewa na za hatari.
Lakini, sasa naamini kuwa amefanya kazi nzuri kufungua mjadala wa jambo muhimu ambalo tumekuwa tunajidai kulipuuza na kujitia kuwa halipo kwa sababu ya unafiki wetu.