Wasomi wa vyuo vikuu na vyuo vya kati nchini wameeleza dhamira yao ya kushiriki kikamilifu katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 kwa ajili ya kuchagua Madiwani, Wabunge na Rais. Wamesisitiza kuwa kwa umoja wao, hawatapigia kura chama au vyama visivyo na malengo mahsusi au dira ya kuiongoza na kulivusha taifa kimaendeleo.
Akizungumza na vyombo vya habari leo April 14, 2025 Katibu Mkuu Mtendaji wa TAHLISO Godfrey Gilagu amesema ”ziara itaongozwa na Rais wa TAHLISO na malengo yake ni kuainisha miradi na Maendeleo ya sekta ya elimu yaliyofanywa na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania”
Gilagu ameeleza kuwa ziara hiyo ikiongozwa na Rais wa TAHLISO Geoffrey Kiliba ndani yake itatolewa elimu juu ya umuhimu wa vijana kushiriki katika kulinda amani hasa katika kipindi cha uchaguzi Mkuu.
Gilagu ameongeza kuwa kwenye ziara hiyo wataitumia kusikiliza na kutatua changamoto zinazowakumba wanavyuo “tutatumia ziara kusikiliza changamoto za wanafunzi kutatua lakini zile ambazo ziko juu ya uwezo wetu tutazichukua na kuzipeleka sehemu husika.”
Aidha ametoa wito kwa wanafunzi wa vyuo vikuu kutokuwa chanzo cha kuharibu amani katika chaguzi za ndani ya vyuo vyao na hata katika uchaguzi Mkuu bali wawe mabalozi wazuri kuelekea uchaguzi huo.