JanguKamaJangu
JF-Expert Member
- Feb 7, 2022
- 2,780
- 6,607
Watuhumiwa hao wamekamatwa na nyaraka za bandia mbalimbali zinazohusu kuacha kazi, vyeti vya huduma, taarifa za uongo za ugonjwa, Hati za uongo za kufukuzwa kazi pamoja na fomu za kugushi za kuomba mafao ya NSSF.
Waliokamatwa ni na pamoja na, (1) Diocress Kahwa (35) mkazi wa Mbezi, mwalimu wa Shule ya Msingi Maxmilian ya Segerea (2) Barnabas Bonivencha na wenzake 11 wa kampuni binafsi ya ulinzi ya G4S waliowasilisha taarifa za uongo za kuacha kazi ili wapate mafao wakati bado wapo kazini.
Alikamatwa pia Gregory Rweikiza (44) mkazi wa Goba na Carolina Mushi (37) Mkazi wa Upanga, Ilala, mtumishi wa Benki ya Stanbink kwa tuhuma za kughushi taarifa za hospitali za ugonjwa za ili apate fao la matibabu.
Waliokamatwa wengine ni Michael Mpogolo (38) na Sabato Thomas (27) wakazi wa Madale Mivumoni Dar es Salaam kwa tuhuma za kughushi nyaraka za wafanyakazi wawili marehemu (Servas Tesha na Korodias Shoo) waliokuwa wanafanya kazi katika Mgodi wa Geita (Geita Gold Mine).
Watuhumiwa wote watafikishwa Makahamani haraka iwezekanavyo kujibu tuhuma zinazowakabili, Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linawataka watu waachane na mambo ya udanganyifu au kughushi nyaraka kwani watakamatwa na
kuchukuliwa hatua kali ikiwa ni pamoja na kuwafisha mahakamani kwa hatua za kisheria.
Vilevile, katika kipindi cha kuanzia mwezi Januari hadi Machi 2024, Jeshi la Polisi Kanda maalum ya Dar es Salaam katika kusimamia mifumo ya haki jinai lilifanikiwa kuwafikisha mahakamani watuhumiwa mbalimbali. Akiwemo Joshua Saidi wa Kinondoni ambaye amehukumiwa kifungo cha maisha baada ya kupatikana na hatia ya kulawiti na kubaka wakati huo huo washtakiwa wengine wawili Karmal Mohamed na Mfaume Hassan wa Kigamboni na Ukonga wamehukumiwa kifungo cha maisha baada ya kupatikana na hatia ya makosa ya kutenda kinyume cha maumbile.
Pia mshtakiwa mwingine ni Justine Kasera wa Kinondoni amehukumiwa kifungo cha miaka 60 kwa tuhuma za kubaka na Kulawiti, Meshack Michael wa Kinondoni amehukumiwa miaka 50 kwa tuhuma za kubaka, Babu Ally Mwinyinvua wa Mburahati na wengine wanne wamehukumiwa vifungo vya miaka 30 kila mmoja baada ya kupatikana na hatia ya kubaka. Mashauri mengine yapo kati hatua mbalimbali za kusikilizwa. Tunawaomba wananchi wafike mahakamani kutoa ushahidi.
Vilevile, Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam kwa kipindi cha Januari hadi Machi 2024 jumla ya makosa ya usalama barabarani yaliyokamatwa yalikuwa 221,724 kati ya hayo makosa ya magari yalikuwa 173,190 na makosa ya pikipiki yalikuwa 48,534 na kuchukuliwa hatua mbalimbali za kisheria ikiwemo kupigwa faini za papo kwa hapo na baadhi ya madereva/wapanda pikipiki walifikishwa mahakamani.
Madereva wa pikipiki na magari waliofikishwa mahakamani 89, waliokamatwa kwa ulevi na kupigwa faini 60, waliokamtwa kwa kupita taa nyekundu na kupigwa faini papo hapo 759, madereva wa pikipiki waliokamatwa kwa kuzidisha abiria (mishikaki) ni 3,779, makosa mengineyo 217,034.
Kuhusu shamra shamra za sikukuu ya Eid Al Fitri, madereva wa vyombo vya moto wote wanaelekezwa kutotumia vileo wakati wa kuedesha magari/pikipiki na wazazi wanakumbushwa kuepuka kuwaacha watoto wadogo kutoka peke yao barabarani na maeneo mengine.
Kuhusu sikukuu ya Eid Al Fitri. Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limejipanga kuhakikisha usalama unaimarishwa katika maeneo yote ya Jiji la Dar es Salaam, zikiwemo nyumba za ibada, mitaani, fukwe za bahari na katika makazi ya watu.Jeshi linawatakia kila la kheri katika sikukuu hiyo
Imetolewa na ;
Muliro J. MULIRO - SACP
Kamanda wa Polisi
Kanda Maalum ya Dar es Salaam