Maafisa wa upelelezi kutoka Kituo cha Polisi Kabete wamewakamata watu wawili wanaodaiwa kutengeneza na kusambaza juisi bandia katika eneo la Muthua, Kabete.
Washukiwa hao, Alex Mwaruta na James Munala Inyangala, walikamatwa wakiwa katika mchakato wa kutengeneza juisi hiyo baada ya polisi kupata taarifa kutoka kwa mwananchi.
Katika operesheni hiyo, polisi walikamata takriban chupa 1,400 za mililita 200 na 300 zilizokuwa tayari zimejazwa, pamoja na makasha 56 ya chupa tupu, vifuniko vitano vya chupa, mapipa mawili na mabeseni matatu.
Vitu vingine vilivyopatikana ni pamoja na gundi ya ofisi, mihuri na wino, vibandiko mbalimbali, pamoja na cheti kilichokwisha muda cha matumizi ya Alama ya Ubora (Standardisation Mark) ya chapa maarufu ya juisi.
Polisi pia walipata unga na vitu visivyo na rangi vilivyokuwa vimehifadhiwa kwenye mifuko ya plastiki na chupa mbalimbali. Vitu hivyo vimechukuliwa kama ushahidi na wachunguzi wa eneo la uhalifu (CSI).
Washukiwa hao kwa sasa wako chini ya ulinzi wa polisi huku uchunguzi ukiendelea.
Source: Citizen digital