'Niambieni usanii wake ni upi? alishazalisha mke wa mtu,alishaua watu? alishatembea na waumini zake? alishavaa pete za ajabu? alishalewa hadharani?'
Huyu jamaa alikua anawaambia waumini wake wakiingia kanisani kwake na vitu vya dhahabu kama Pete,Mikufu,heleni wanamkabidhi avichome mote maana ni vitu vya shetani hivyo.
Siku anahojiwa na Pasco Mayalla akaombwa aonyeshe wapi hua anachomea hivyo dhahabu za waumini wake,aling'aka hatari saaana.
ASKOFU KAKOBE: SIJAWAHI HATA MARA MOJA KUPORA AU KUCHUKUA AU KUKUSANYA MAPAMBO YA DHAHABU YA WANAWAKE KANISANI AU POPOTE PALE WALA KANISA LA FGBF HALIJAWAHI KUFANYA HIVYO KATIKA IBADA YOYOTE
MWANDISHI BZKIM: Mtumishi wa Mungu, Askofu Mkuu Zachary Kakobe; kwanza kabisa, asante kwa muda wako. Mtumishi, kumekuwa na madai yanayojirudia-rudia kila baada ya miaka kadha, yanayodai kwamba, wewe binafsi, na pia Kanisa la FGBF unaloliongoza, mmekuwa mkipora, au kukusanya katika Ibada za Kanisa, mapambo mbalimbali ya wanawake, kama heleni, bangili, vikuku, pete, au mikufu ya dhahabu au vito vya aina mbalimbali; katika vyombo vya sadaka, na kisha kuvichukua na kuviuza; na kwamba hicho ndicho chanzo cha utajiri wako. Wanaodai hivyo, wanasema kwamba, ndiyo maana wanawake wote ambao ni waumini wa Kanisa la FGBF, hawana mapambo hayo. Je, kuna ukweli wowote katika madai haya? Najua fika, kwamba, umewahi kujibu kwa ufasaha tuhuma hizi, mara nyingi sana huko nyuma, hata hivyo, kama ikikupendeza, ninakuomba usichoke kujibu madai haya tena leo, kwa kina, mapana na marefu; kwa faida ya watu wengine, ambao hawakuwahi kusikia au kusoma majibu yako, miaka ya nyuma.
ASKOFU MKUU ZACHARY KAKOBE: Mimi sijawahi hata mara moja, kupora, au kuchukua heleni, bangili, vikuku, pete, mikufu au mapambo yoyote ya dhahabu au vito vingine vyovyote, vya mwanamke au mwanaume yeyote, Kanisani, au popote pale. Vilevile, tangu Ibada ya Kwanza ya Kanisa hili la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF), iliyofanyika Ukumbi wa Shule ya Msingi Jamhuri, Mnazi Mmoja, Dar-Es-Salaam; Jumapili tarehe 30.4.1989; hadi leo, katika IBADA YOYOTE ILE, hatujawahi kukusanya, wala kuwaambia waumini waweke katika vyombo vya sadaka, au vyombo vyovyote vingine; heleni zao au bangili, vikuku, pete, au mikufu ya dhahabu au vito vya namna nyingine yoyote; halafu eti tukavichukua na kuviuza! HUU NI UZUSHI WA MCHANA KWEUPE! Wala siyo ajabu kuwepo kwa wazushi wa jinsi hii, nyakati hizi; maana katika 2 PETRO 2:1-3, Biblia imetuonya juu ya kuwepo kwao: "Lakini kuliondokea manabii wa uongo katika wale watu, KAMA VILE KWENU KUTAKAVYOKUWAKO waalimu wa uongo, watakaoingiza kwa werevu UZUSHI WA KUPOTEZA .... Na wengi watafuata ufisadi wao, NA NJIA YA KWELI ITATUKANWA. Na katika kutamani watajipatia faida kwenu KWA MANENO YALIYOTUNGWA ..."
Kwa mara ya kwanza, uzushi huu ulianza kusikika mwaka 1997; na mwanzoni mwa mwaka 1998, uzushi huu ulimfikia Waziri wa Mambo ya Ndani wa wakati huo, na akautamka katika vyombo vya habari, bila kufanya utafiti wowote ule. Nilikanusha vikali tuhuma hizo, na vyombo vingi vya habari vikiwemo magazeti na Televisheni, vilisambaza majibu yangu nikisema kwamba, kama kuna mtu yeyote yule niliyewahi kumpora heleni, bangili, au mkufu wa dhahabu au vito vingine vyovyote; au aliyeweka vitu vyake hivyo katika vyombo vyovyote Kanisani, aende kutoa ripoti katika kituo chochote cha Polisi, na kutoa ushahidi wake; ili nishitakiwe kwa kesi ya jinai. Nikaviomba pia vyombo vya dola, kuja kunichunguza, au kufanya uchunguzi Kanisani au kwenda popote pale kufanya uchunguzi huo; na nikasema kwamba, hata kama yuko sonara yeyote Tanzania au popote pale duniani, niliyewahi kumwuzia vitu hivi, naye ajitokeze akiwa na ushahidi. Nami niko tayari kabisa kutoa ushirikiano. Gazeti maarufu nyakati hizo, lililokuwa linaitwa "TAIFA LETU", liliandika habari hiyo kwa urefu sana. Hata hivyo, baada ya taarifa hiyo kwenye vyombo vya habari, hakuna mtu yeyote aliyejitokeza katika kituo chochote cha Polisi, bali kila mshirika au muumini wa Kanisa letu, na wote waliowahi kuja katika Ibada zetu, wote walisema huo ni uzushi kabisa, hakujakuweko kitu kama hicho, wakati wowote ule!
Baada ya kisa hicho, uzushi huo ulizimika kabisa, hadi mwaka 2005, ulipoibuka tena kwa nguvu, na safari hii, uzushi huo ukaja na nyongeza kwamba, eti kila mtu anayekuja Kanisani kwetu na gari lake, huwa ninamnyang'anya funguo za gari lake, na kuyachukua magari yote na kuyafanya ya kwangu! Uzushi wa kutisha! Jambo la ajabu, ni kuwa, "pamoja na madai hayo kwamba, magari yote hayo huwa mimi ninayachukua", hakuna hata mtu mmoja aliyeporwa gari, aliyekwenda kuripoti Polisi. Uzushi huu niliupuuza, lakini baadaye nikaona vema kujibu madai hayo kwa ujumbe wa Neno la Mungu, uliokuwa na kichwa, "SHETANI BABA WA UONGO", niliouhubiri katika Kanisa la FGBF DAR-ES-SALAAM, lililoko Barabara ya Sam Nujoma, Mwenge; siku ya Jumapili tarehe 5.3.2006; na ujumbe huo ukarekodiwa katika Video. Sambamba na mahubiri hayo, katika Ibada hiyo, kulikuwa pia na shuhuda za watu wengi wenye magari walioshuhudia na kueleza kwamba, huo ni uzushi, hakuna yeyote aliyewahi kuporwa gari lake. Vilevile, wengi walieleza pia hakuna yeyote aliyewahi kuporwa au kutoa sadaka za heleni, bangili, vikuku, pete, wala mikufu ya dhahabu au vito vyovyote vingine. Nikarudia tena kusema, katika ujumbe huo kwamba, kama kuna mtu yeyote aliyewahi kuporwa vitu hivyo, aende kituo cha Polisi na mimi niko tayari kutoa ushirikiano. Na kadhalika kama kuna sonara yeyote niliyewahi kumwuzia vitu hivyo, naye pia ajitokeze hadharani na kutoa ushahidi. Siku chache baada ya siku hiyo, kupitia katika kipindi changu cha TV, cha "NENO LA UZIMA", wakati huo; ujumbe huo ulirushwa katika Televisheni za CHANNEL TEN na STAR TV, na kurudiwa takribani mara ishirini (20)! Hata hivyo, hakuna hata mtu mmoja aliyejitokeza, katika kituo chochote cha Polisi.
Je, baada ya hapo, uzushi huo ulikoma kabisa? Ulizimika kwa muda mrefu, na baadaye sana, ukawa unaibuka tena mara mojamoja. Hata hivyo, miaka ya hivi karibuni, uzushi mwingine ukajitokeza kwa nguvu, ukidai kwamba eti nimefanya uhalifu, na kuliuza Kanisa na kutoroka nchini, na kuhamia Marekani, na wengine wakasema nimehamia Canada. Washirika wa Kanisa letu la FGBF, walipokuwa wanasikia uzushi huu walikuwa wanashangaa sana, kwa sababu wanaujua ukweli kwamba sijawahi kuhamia nchi yoyote duniani, nimekuwa tu nikienda kuhubiri Injili nje ya nchi, na kurudi, na kuwa pamoja nao Kanisani; na safari ndefu zaidi ya Injili niliyowahi kuifanya nje ya nchi, ilikuwa mwaka 2016, nilipokwenda Australia, na kuhubiri Injili huko kwa wiki saba, kisha nikarudi nchini, kuendelea na huduma Kanisani.
Hizi zote, ni kazi za roho zidanganyazo (1TIMOTHEO 4:1), ambazo ni roho za Ibilisi, baba wa uongo (YOHANA 8:44), audanganyaye ulimwengu wote (UFUNUO WA YOHANA 12:9). Yesu Kristo alipofufuka siku ya tatu, kama alivyosema kabla, mashetani yote yalitaharuki, na kuamua kuzitumia roho hizi zidanganyazo, kutunga uongo na kuusambaza, ili kuupotosha ukweli wa kufufuka kwa Yesu Kristo. Biblia inasema katika MATHAYO 28:12-15, "Wakakusanyika pamoja na wazee, wakafanya shauri, wakawapa askari (walinzi wa kaburi), fedha nyingi, wakisema, Semeni, ya kwamba wanafunzi wake walikuja usiku, wakamwiba, sisi tulipokuwa tumelala. Na neno hilo likisikilikana kwa liwali, sisi tutasema naye, nanyi tutawaondolea wasiwasi. Basi wakazitwaa zile fedha, wakafanya kama walivyofundishwa. NA NENO HILO LIKAENEA KATI YA WAYAHUDI HATA LEO." Hizi ndizo kazi za roho zidanganyazo! Hata hivyo, mtu yeyote "akijiongeza", kama wanavyosema waswahili wa mtaani siku hizi; yaani akiwa tayari kuushughulisha ubongo wake kidogo tu, na kutumia akili tu za kawaida (common sense), anaweza kung'amua kwamba huu ni uongo na uzushi wa mchana kweupe! Kama ni mahakamani, mtu angewauliza walinzi hawa, "Mnasema mlikuwa mmelala, kama mlikuwa mmelala, mliwaonaje waliomwiba, wakati mmelala usingizi; kiasi cha kuwafahamu kwamba ni wanafunzi wake? Na kama mliwaona wakimwiba, kwa nini hamkuwazuia wasiuibe mwili wa Yesu, wakati kazi yenu mliyopewa ni ulinzi wa kaburi?" Maswali hayo tu, yangewaumbua wazushi hawa. Vivyo hivyo, mtu mwenye akili kidogo tu ya kawaida, angeweza kuwauliza wazushi wanaosema Kakobe alitoroka na kuliuza Kanisa, "Makanisa ya FGBF yako zaidi ya 1,000 na yametapakaa kila wilaya Tanzania bara. Je, alimwuzia nani Makanisa yote haya? Mtu anaweza kununua Makanisa yote haya, na asijulikane? Na je, kama alitoroka nchini, kwa sababu ya uhalifu, je, amerudi? Na alivyorudi alikamatwa na Polisi? Na je, mbona hivi sasa baada ya kurudi, bado analiongoza Kanisa lilelile? Je, aliporudi, yule aliyemwuzia Kanisa hilo, alimrudishia tena Makanisa hayo?" Ni uzushi na uongo wa mchana kweupe, na ni aibu tupu kwa mtu aliyeuamini uongo huo! Waingereza wanasema, "Common sense is not so common nowadays!" Yaani, siku hizi hata akili za kawaida zimekuwa adimu! Tukirudi nyuma tena kidogo, nasema kwa msisitizo: Ndugu zangu, mimi ninayaishi mahubiri ya utakatifu, ninayoyahubiri (1 SAMWELI 12:1-5); hivyo, BADO NINARUDIA HATA HIVI LEO, KAMA KUNA MTU YEYOTE NILIYEWAHI KUMPORA AU KUCHUKUA MAPAMBO YAKE, AKATOE TAARIFA KITUO CHOCHOTE CHA POLISI. NIKO TAYARI KABISA KUTOA USHIRIKIANO. KESI YA JINAI HAIFI WALA HAIPITWI NA WAKATI!
Ndugu Mwandishi, nirudi tena kwenye maswali yako. Je, kuuza mapambo hayo ndiyo chanzo cha utajiri wangu au wa Kanisa? Mwaka juzi 2018, TRA walikuja kufanya uchunguzi wa kina kuhusu mapato yangu binafsi, na ya Kanisa. Walitoa hitimisho, wakasema mimi binafsi sifanyi biashara yoyote, na Kanisa pia halifanyi biashara yoyote, fedha yote ya Kanisa inatokana na zaka, changizo, na sadaka. Hitimisho hilo la TRA, ni jibu tosha! Na sasa je, kama hatuchukui mapambo ya dhahabu, ya wanawake; mbona waumini wa Kanisa la FGBF (wanawake na hata wanaume), hawana mikufu, vikuku, bangili, au heleni za dhahabu au vito vingine vyovyote, na mapambo kwa ujumla wake? JIBU NI HILI: Katika Kanisa la FGBF, tunahubiri Injili ya Wokovu isiyoghoshiwa, yaani isiyotiwa maji (2 WAKORINTHO 2:17). Hatuhubiri maneno laini yadanganyayo (ISAYA 30:9-10), ili kujaza umati wa watu Kanisani. Tunahubiri maneno ya uzima, hata kama ni magumu; na yeyote asiyekuwa tayari kulitii na kulitendea kazi Neno la Mungu tunalolihubiri, yuko huru kuondoka (YOHANA 6: 60-61, 66-68). Hatuhubiri wokovu vuguvugu, kwa kuwa vuguvugu watatapikwa (UFUNUO WA YOHANA 3:15-16). Kwa msingi huu, TUNAHUBIRI KWAMBA, MTU ALIYEOKOKA, HAPASWI KUVAA MAVAZI YA KIKAHABA (MITHALI 7:10). Na tunahubiri kwamba, wanawake watakatifu wanatakiwa kuwa mbali na mapambo yoyote, iwe ni heleni, mikufu, vikuku, bangili na kadhalika; kama walivyokuwa wanawake watakatifu wa zamani (1 TIMOTHEO 2:9; 1 PETRO 3:3-6); na kwamba, utakatifu hauzihusu roho zetu tu, bali utakatifu ni kuwa mbali na uchafu wote wa MWILI NA ROHO (2 WAKORINTHO 7:1; 1 WAKORINTHO 7:34). Tunasafisha KWANZA ndani, ILI NJE YAKE NAYO ipate kuwa safi (MATHAYO 23:25-26). Na tena tunahubiri kwamba, mtu atakayeiona Kanaani, au mbingu, ni yule atakayemfuata BWANA kwa KILA NENO (KUMBUKUMBU 1:35-36; ZABURI 119:9). Yeyote ambaye hatayaangalia MAAGIZO YOTE ya Mungu, ataaibika na kudharauliwa katika mauti ya milele (ZABURI 119:6; DANIELI 12:2). Na tena tunahubiri kwamba, sisi tuliookoka, hatupaswi kuenenda kama Mataifa waenendavyo, katika UBATILI WA NIA ZAO (WAEFESO 4:17); hivyo mtu anapotubu dhambi ya ukahaba, hawezi tena kuendelea kuvaa mapambo, ambayo ni vitendeakazi vya ukahaba. Kutubu ni lazima kuambatane na kuacha dhambi (MITHALI 28:13), na kuyatenda matendo yanayopatana na kutubu kwetu (MATENDO 26:20). Mwanamke (au mwanaume) anaposikia Injili ya namna hii isiyoghoshiwa, na kwa hiyari yake, kuamua kukata shauri kutubu ukahaba wake, huyakongoroa mwenyewe mapambo yake ya kikahaba, akiwa nyumbani kwake mwenyewe; na anakoyaweka au anakoyapeleka, hujua yeye mwenyewe; na kisha huja Kanisani akiwa hana mapambo hayo ya kikahaba. Makanisa yetu, siyo madanguro au mapango ya wanyang'anyi (MATHAYO 21:13). Ndugu Mwandishi, natumaini nimejibu maswali yako, kwa kina, mapana na marefu; kama ulivyoomba.
MWANDISHI BZKIM: Naam! Asante sana Mtumishi wa Mungu, kwa majibu mujarabu!
ASKOFU MKUU ZACHARY KAKOBE: Mungu akubariki sana. Karibu tena! ☆☆☆☆