McLaren
JF-Expert Member
- Feb 19, 2025
- 1,170
- 3,743
Amesema Doria za mtandaoni zitasaidia kuondoa utapeli pamoja na kukamata wahalifu ambao wanania ya kuvunja amani
=========
BASHUNGWA AMUAGIZA IGP KUDHIBITI WAHALIFU WANAOTUMIA MITANDAO KUVURUGA AMANI.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa, amemuagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Camillus Wambura, kuhakikisha Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama linaimarisha doria mtandaoni (online patrol) kwa lengo la kudhibiti baadhi ya wahalifu wanaotumia mitandao kuvuruga amani na utulivu wa nchi, pamoja na kukabiliana na uhalifu unaofanyika kwa njia ya mtandao.
Bashungwa ametoa agizo hilo leo, tarehe 6 Agosti 2025, wakati wa hafla ya uzinduzi wa Kituo kipya cha Polisi cha "Daraja B" kilichopo Sanya Juu, Wilaya ya Siha, mkoani Kilimanjaro, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali kuboresha miundombinu ya majengo na vitendea kazi ndani ya Jeshi la Polisi.
Aidha, Waziri Bashungwa amelielekeza Jeshi la Polisi kuendelea kutekeleza maagizo mbalimbali ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, yanayohusu kupambana na uhalifu, udhibiti wa madereva wazembe, pamoja na kuondoa vyombo vya moto visivyokidhi viwango vinavyosababisha ajali barabarani.
Bashungwa amelitaka Jeshi la Polisi kushirikiana na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kubaini maeneo hatarishi katika barabara kuu ambazo zimekuwa zikiripotiwa kusababisha ajali mara kwa mara, ili yafanyiwe upembuzi yakinifu na kutengewa bajeti kwa ajili ya kutafutiwa suluhisho la kudumu.
Kadhalika, Bashungwa ameviagiza vyombo vyote vya usalama vilivyo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kuendelea kushirikiana katika kuimarisha amani, usalama na utulivu, hasa katika kipindi cha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 na baada ya uchaguzi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Camillus Wambura, ametoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi ili kudumisha amani na utulivu, huku akiwatoa hofu Watanzania kwa kuwahakikishia kuwa nchi ipo salama na itaendelea kuwa salama.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, amesema kuwa kituo cha Polisi cha Wilaya ya Siha kimejengwa kwa fedha za Serikali kupitia Jeshi la Polisi, kwa kushirikiana na michango ya wananchi wa wilaya hiyo.