Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi amewaasa wastaafu wa Idara ya Uhamiaji kujiepusha na anasa pindi watakapopata mafao yao, bali wajikite kufanya shughuli za uzalishaji ili kuondoa upweke.
Pia amewataka wastaafu hao kulinda afya zao, kumrudia Mungu na kuwa waaminifu katika ndoa zao.
Ameyasema hayo hivi karibuni jijini Dar es Salaam wakati wa Sherehe ya Kuwaaga Wastaafu Maafisa Uhamiaji Waandamizi na Watumishi Wastaafu wa Idara ya Uhamiaji ambapo amewapongeza wastaafu hao 23 kwa utumishi uliotukuka uliosaidia shughuli za Ulinzi na Usalama wa nchi ya Tanzania na Mipaka yake.
Waziri Katambi ametoa wito kwa uongozi wa Idara ya Uhamiaji kuhakikisha wastaafu wanapata stahiki zao kwa wakati, huku akisema atalisimamia suala hilo.
“Mmekua watumishi wa umma,mmefanya kazi yenu kwa utumishi uliotukuka na Taifa letu liko salama, tunawashukuru sana, tutaendelea kuwa karibu nanyi na sisi tuliobaki kwenye ofisi ya umma mmetuacha na mtihani mkubwa ambao sisi tunao wajibu wakutenda kwa wema ili na sisi tufikie ustaafu uliotukuka na hatimae kufanyiwa sherehe,”aliongeza Waziri Katambi.
Pia Waziri Katambi amewataka watumishi wa Idara ya Uhamiaji kufanya kazi kwa weledi kwa kuzingatia sheria, taratibu na miongozo pasipo upendeleo wala kumuonea mtu mtumishi yoyote.
“Mnafahamu maboresho yaliyofanyika katika Idara ya uhamiaji ikiwemo maslahi ya askari na watumishi katika Idara yetu ya Uhamiaji, maboresho ya maeneo yetu ya ofisi ambayo yanaendelea hata Ujenzi wa Ofisi ya Makao Makuu pale Dodoma na maeneo mengine imekua ni kipaumbele cha Mheshimiwa Rais wetu, Dk Samia Suluhu Hassan ikiwa ni pamoja na maboresho ya makazi lakini pia na vitendea kazi,” amesema Waziri Katambi.