Stephano Mgendanyi
JF-Expert Member
- May 16, 2020
- 2,833
- 1,301
WAZIRI MHAGAMA: TUWALINDE WATOTO, DUNIA IMEBADILIKA
Wazazi na walezi wametakiwa kuhakikisha wanawalinda watoto dhidi ya vitendo vya kikatili kwa kuhakikisha wanatoa taarifa ili hatua za kisheria zichukuliwe badala ya kuwa sehemu ya kuwaficha watu wanaofanya vitendo hivyo vinavyosababisha madhara makubwa kwa watoto.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Jenista Mhagama wakati akizungumza na wakazi wa Kata ya Kilagano, Kijiji cha Muungano Zomba , Wilaya ya Songea Vijijini katika ziara yake Jimbo la Peramiho mkoani Ruvuma ambapo amesema wazazi na walezi wanapaswa kuwa mfano bora kwa watoto wao.
Mhe. Jenista amesema vitendo vya ukatili vimekuwa vikikithiri kila kukicha maeneo mbalimbali huku baadhi ya vitendo hvyo vikifanywa na wazazi wenyewe, walezi na hata watu wa karibu ambao wanategemewa na jamii kuwa sehemu ya kuwajenga watoto katika malezi bora.
"Dunia imeharibika na wala siyo siri na lazima tuelezane walindeni hao watoto tutadaiwa na Mwenyezi Mungu, lazima tuwe waangalifu jengeni tabia ya kuwafuatilia watoto kila wanapotoka shule mtoto anafananaje, anaonesha na tatizo? msikilize na kina mama wenzangu mjenge urafiki na watoto siyo mtoto anakusogelea unakuwa mkali hutaki kumsikiliza" - Amesisitiza Mhe. Jenista.
Sambamba na hayo amewahimiza Maafisa Maendeleo ya Jamii, Ustawi wa Jamii, Dawati la Jinsia, Polisi, Walimu na Wadau wengine wote kuendelea kutoa huduma ya elimu ya malezi na makuzi ya watoto kwa wazazi na walezi ili waelewe wajibu wao wa kulea watoto katika msingi wa haki na usawa wa kijinsia.
"Ndugu zangu watoto wanapitia vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia, vipigo kutoka kwa wazazi, walezi na walimu, kubakwa, kulawitiwa, mimba na ndoa za utotoni pia wanatumikishwa katika kazi zisizoendana na umri wao na hata kukosa haki zao za elimu kwahiyo ni wajibu wa kila mmoja kupaza sauti" Alieleza.
Katika hatua nyingine, Mhe. Jenista amewaahidi wakazi wa Kijiji cha Maduwalo, Kata ya Maposeni akisema Serikali itaendelea kutatua changamoto zinazowakabili zikiwemo maji na barabara akisema yote yatafanyiwa kazi pamoja na kushirikiana na Mawaziri wenye dhamana ili wananchi wapate huduma hizo muhimu kama lilivyo lengo la Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Aidha, katika ziara hiyo Mhe. Jenista aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa bweni la wasichana katika shule ya Sekondari ya Daraja Mbili iliyopo Kata ya Maposeni, Kijiji cha Maposeni, kukagua maendeleo ya ujenzi wa shule ya Sekondari katika Kijiji cha Lugagara , Kata ya Kilagano, kukabidhi vifaa kwa watu wenye ulemavu, vifaa vya michezo pamoja na kuweka jiwe la msingi ujenzi wa nyumba ya Mganga wa Zahanati ya Mdunduwalo kijijini hapo iliyojengwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).