Posted Date::10/25/2007
Rais Kikwete aongoza mamia kupokea mwili wa Salome Mbatia Dar
Na Salim Said, MUM
Mwananchi
RAIS Jakaya Kikwete, jana aliongoza mamia ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam kuupokea mwili wa aliyekuwa Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Salome Mbatia aliyefariki kwa ajali ya gari iliyotokea juzi wilayani Njombe, Iringa.
Ndege ya serikali 5H-TGF iliyobeba mwili wa marehemu ilitua katika Uwanja wa Ndege wa Zamani majira ya saa 7:45 mchana ikitokea Iringa.
Baada ya kuwasili uwanjani hapo mwili huo ulishushwa kutoka katika ndege hiyo na Mawaziri na Manaibu Naibu Waziri wa Habari Utamaduni na Michezo, Daniel Nsanzugwanko na kusogezwa karibu na viongozi mbalimbali waliokuwa uwanjani hapo kuupokea akiwamo Rais Kikwete, Makamu wake Ali Mohamed Shein Waziri Mkuu Mkuu wa Edward Lowassa na viongozi mbalimbali na wananchi walisimama kwa dakika chache ikiwa ni ishara ya kutoa heshima zao.
Wengine ni Naibu Waziri wa Usalama wa Raia, Mohamed Aboud, Naibu wa Mambo ya Ndani, Lawrence Masha, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Ludovic Mwananzila, Naibu Waziri wa Mipango, Uchumi na Uwezeshaji, Gaudence Kayombo na Nibu Wziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Joel Bendera .
Wengine waliofika uwanjani hapo ni Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), John Malecela, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abass Kandoro na Kamishina wa Kanda Maalumu Alfred Tibaigana.
Baada ya zoezi hilo mwili huo ulingizwa katika gari maalum la wagonjwa (ambulance) la Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na kupelekwa kwa msafara katika Hospitali ya Jeshi Lugalo.
Akizungumza na waandishi wa habari uwanjani hapo, Mwenyekiti wa Kamati ya Mazishi, Andrew Chenge alisema mwili wa marehemu utapelekwa nyumbani kwake saa 1.30 asubuhi leo kwa ibaada ya maalumu ya kuuaga na wananchi kutoa heshima za mwisho kabla ya kusafirishwa kwenda mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro kwa mazishi yanayotarajiwa kufanyika kesho.
Hali katika uwanja wa ndege ilikuwa ya huzuni ambapo vilio na nyimbo za maombelezo kutoka kwa kikundi cha akina mama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), zilitawala uwanjani hapo.
Kututoka Iringa, Hakimu Mwafongo, anaripoti kuwa mamia ya wananchi wa mkoa wa Iringa jana waliojitokeza kuuaga mwili wa Naibu Waziri wa Maendeleo ya Wanawake, Jinsia na Watoto, Salome Mbatia aliyefariki juzi katika ajali ya gari wilayani Njombe.
Hata hivyo, wengi wao hawakufanikiwa kuuga kutokana na muda kwuwa mfupi.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa, Bernard Nzungu aliwaambia wananchi waliokuwa wamekusanyika nje ya nyumba ya kuhifadhi maiti katika hospitali ya Mkoa wa Iringa jambo hilo haliwezi kufanyika kutona na muda kutotosha.
Mwili wa marehemu na wa dereva wake Anakleti Mogella ambaye pia alikufa katika ajali hiyo ilisafirishwa kwa ndege kuelekea Dar es Salaam jana, majira ya saa 6:30 mchana.
Baadhi ya viongozi waliokuwa katika msafara huo ukiongozwa na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Tamisemi, Selina Kombani ni pamoja na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani Dk Lawrance Masha na Naibu Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, Dk Emanuel Nchimbi.
Wengine waliokuja ni pamoja na mume wa marehemu, Dk Mbatia, mtoto wake wa kiume na baadhi ya wanafamilia wa waziri huyo.
Mwakilishi wa Jeshi la Polisi Tanzania, aliyemuwakilisha Inspekta wa Polisi, Said Mwema,
Kamishna wa Polisi Pualo Chagonja alisema ajali zinazoendelea kutokea sehemu mbalimbali zinaendelea kuwakumbusha watumia barabara kuzingatia sheria za matumizi ya barabara.
Katika ajali hiyo, gari la Waziri huyo aina ya Nissan Patrol liligongana uso kwa uso na gari No T 299 AFJ Mitsubishi Fuso mali ya Jackson Kilagwa (30) wa Rujewa Mbeya.
Alisema pamoja na Naibu Waziri na dereva wake kufariki papo hapo, msaidizi wa dereva wa loli hilo, Castory Kilangwa pia alikufa papo hapo. Dereva wa lori hilo, anayedaiwa kuwa mkazi wa Makambako wilayani Njombe aliyenusurika katika ajali hiyo alitoroka baada ya ajali hiyo na Polisi limeahidi kumsaka mpaka apatikane.
Wengine waliokufa kwenye ajali hiyo Nicholaus Lubuva (33) Mkazi wa Mufindi na Dastun Gonze (26) ambaye ni mkulima wa Igowole wilayani Mufindi woliokuwemo katika lori hilo walijeruhiwa vibaya kwa kuvunjika miguu na mikono ambapo walipelekwa katika Hospitali ya Kibena Njombe.
Naye Tausi Mbowe anaripoti kuwa, Makao Mkuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) jana yalikuwa katika hali ya utulivu tofauti na siku nyingine huku baadhi ya wanachama wa chama hicho wakionekana wenye huzuni kufuatia msiba huo.
Mwandishi alishuhudia baadhi ya wanachama hao wakiwa katika makundi makundi wakijadili juu ya msiba huo, huku wakionyesha huzuni kubwa.
Baadhi ya wanachama hao walionekana wakiwa wamevalia nguo nyeusi kuashiria hali ya maombolezo huku wengine wakiwa wamevalia nguo za rangi ya chama hicho.
Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu, Katibu Mwenezi na Itikadi wa CCM Taifa, Agrrey Mwanri alisema chama kimepoteza mtetezi wa wanyonge, mpiganaji, mwanamapinduzi na kiongozi mchapa kazi.
Mwanri alisema alikuwa karibu sana na Mama Mbatia na akaongeza kwamba chama kimepokea msiba huo kwa majozi makubwa
"Mbatia alikuwa mtetezi wa wanyonge mwanamapinduzi, kada, na mpenda maendeleo," alisema Mwanri.