Roving Journalist
JF Roving Journalist
- Apr 18, 2017
- 3,984
- 13,760
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Jerry William Silaa (Mb) amesema kuwa utekelezaji wa mfumo wa Anwani za Makazi nchini umelenga kurahisisha utoaji na upokeaji wa huduma mbalimbali ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Waziri Silaa ameyasema hayo tarehe 06 Februari, 2025 jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari katika hafla ya ufunguzi wa maadhimisho ya kwanza ya wiki ya Anwani za Makazi 2025.
“ Mfumo wa Anwani za Makazi ni endelevu kwa sababu ya mabadiliko ya makazi, wakazi na huduma, hivyo kufanyika kwa maadhimisho haya kutaongeza hamasa kwa Taasisi za umma na Binafsi pamoja na Wananchi kuweza kutambua na kutumia Anwani za Makazi katika shughuli za kijamii na kiuchumi”, alisisitiza Waziri Silaa
Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Mhe. Dkt. Festival Dugange) alisema kuwa Ofisi ya Rais - TAMISEMI ni mdau mkuu katika utekelezaji wa mfumo wa Anwani za Makazi hususan kupitia kwa watendaji wa Kata, Vijiji na Mitaa ambao wana wajibu wa kuwezesha uwekaji wa miundombinu; kuhuisha taarifa; na kukusanya taarifa mpya.
“TAMISEMI ndiyo yenye wananchi na ndiyo mtoa huduma mkuu kwa wananchi, hivyo TAMISEMI inauhitaji sana Mfumo huu na kwa sasa tulifanya majaribio ya kutoa barua kwa njia ya kidijitali ambapo jambo hilo limeonyesha kuwa la mafanikio,”alisema Mhe. Dkt. Dugange.
Maadhimisho haya yanaenda sambamba na maonesho ya Wizara na taasisi zinazotumia Mfumo wa Anwani za Makazi na kilele chake tarehe 8 Februari, 2025 ambapo Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.